Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ufaulu Shule ya Sheria bado majanga

Dar es Salaam. Matokeo ya mtihani wa uwakili yameendelea kuwa mwiba kwa wahitimu wa Shule Kuu ya Sheria (LST), hatua inayoibua hoja mpya za ugumu wa maisha kwa wanafunzi hivyo kushindwa kutulia shuleni hapo, ikiwa ni tofauti na mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti iliyowasilishwa mwaka jana.

Matokeo ya Oktoba mwaka jana, katika muhula wa 33 yaliyoibuliwa na gazeti hili yalionyesha wanafunzi 26 (sawa na asilimia 4.1) pekee ndio walifaulu, 342 wakitakiwa kurudia baadhi ya masomo, huku wengine 265 sawa na asilimia 41.9 wakifeli na kukatishwa masomo.

Ikiwa ni miezi sita imepita baada ya Serikali kuunda kamati ya kuchunguza na kutoa mapendekezo, gazeti hili limepata matokeo mapya ambayo ni wanafunzi 23 tu kati ya 821 waliofaulu katika kundi la 34, ambayo yanahusisha wanafunzi wa kipindi cha masomo Januari hadi Desemba mwaka jana.

Katika matokeo hayo yaliyotoka Aprili, wanafunzi 497 wanatakiwa kurudia baadhi ya masomo na 301 kukatishwa masomo yao. “Ni kweli hayo ni matokeo yetu, lakini sio rahisi kuona matokeo ya utekelezaji wa maagizo ya kamati hiyo kwa sababu ni muda mfupi sana, ili kufanikisha utekelezaji wa maagizo ya kamati hiyo tunawajibika kwa vyuo, wanafunzi na wengine waliotajwa,” alisema Ofisa habari wa LST, Fatma Salumu.

Miezi sita iliyopita Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro aliunda kamati hiyo yenye wajumbe saba kwa lengo la kutafuta chanzo cha kufeli kwa wanafunzi wengi kwenye mitihani ya LST.

Hatua hiyo ilikuja baada ya malalamiko na kelele za wanafunzi na wananchi kufuatia hoja iliyoibuliwa na gazeti hili kuhusu idadi kubwa ya waliofeli mitihani ya mwisho ya kumaliza mafunzo hayo, yanayowapa sifa ya kuwa mawakili. Kamati hiyo iliwasilisha mapendekezo kadhaa, ikiwamo kuanzishwa mtihani maalumu wa kuingia LST kama ilivyo katika mataifa mengine ya Afrika Mashariki, huku ikielekeza kushughulikia changamoto kutoka kwa wanafunzi, LST na vyuo vinavyotoa shahada ya sheria nchini.

Jana, akiwasilisha bungeni bajeti ya wizara yake, Dk Ndumbaro alisema miongoni mwa vipaumbele vya wizara kwa mwaka 2023/24 ni kuimarisha mfumo wa elimu ya sheria.

Dk Ndumbaro alisema katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi, 2023, LST ilidahili wanafunzi 1,348 sawa na asilimia 89.9 ya lengo la udahili wa wanafunzi 1,500 kwa kundi la 35 na 36. Aidha, alisema katika kipindi hicho, taasisi imetoa wahitimu 363 wanaostahili kusajiliwa kuwa mawakili na kufanya idadi ya wahitimu waliopata mafunzo kupitia taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 kufikia 8,255.

Alisema idadi ya wahitimu katika kipindi husika imeongezeka kwa asilimia 23.9 ikilinganishwa na wahitimu 293 wa kipindi cha Julai, 2021 hadi Machi, 2022. Akizungumzia hali hiyo, Dk Onesmo Kyauke alisema siyo rahisi kuanza utekelezaji wa mapendekezo hayo kwa sasa.

“Ni mapendekezo ya muda mrefu, kwa hiyo huenda yanapita kwenye hatua kadhaa, changamoto iliyosahaulika katika mapendekezo hayo ni maisha yao.

“Nimefundisha Sheria miaka takribani 20, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo cha Lushoto. Wanafunzi wengi hawasomi darasani na wakiingia hawatulii kwa sababu ya ugumu wa maisha, wengi wana msongo wa mawazo kuhusu ada na mlo wa siku, Serikali iwapatie mikopo ya ada na kujikimu,” alisema Dk Kyauke ambaye pia ni wakili.

Dk Kyauke alisema hatua hiyo itapunguza changamoto za wanafunzi wengi kufeli masomo hayo, akitolea mfano kama ilivyokuwa kozi za uhasibu NBAA.

“Hata ukifanya utafiti leo utapata majibu sehemu kubwa ni ugumu wa maisha, kwa hiyo kama kamati hawakuona hilo, basi watizame upya.

Kwa upande wa Wakili Jeremiah Mtobesya, aliyehitimu LST katika muhula wa tano, alisema alifaulu katika mazingira magumu sana baada ya kugundua makosa ya kutokwenda kujifunza kwa vitendo katika ofisi za mawakili mahakamani. Alikuwa miongoni mwa wanafunzi 32 kati ya 195 waliofaulu huku 91 wakitakiwa kurudia baadhi ya masomo.

“Ile shule inafunza masomo kwa vitendo katika mfumo wa nadharia, kama ningekuwa nina uzoefu wa kazi kwa miaka mitatu kabla ya kwenda kusoma hapo ningefaulu vizuri zaidi.

“Lakini tulikomaa sana, ukicheza kidogo wanapita na wewe, walimu wako makini sana.
“Kwa mfano unaletewa swali kwenye mtihani linalokutaka umsaidie mteja mahakamani kuhusu changamoto zake kwa nyaraka za mahakamani, sasa kama hujui asili ya tatizo lake huwezi kujua ni nyaraka gani utumie na mahakamani gani ukafungue kesi yake. Hii inahitaji vitendo zaidi.

“Tatizo la chuoni hapo muda wa nadharia ni mwingi kuliko wa kwenda kujifunza kwa vitendo, kwa hiyo nashauri waongeze muda tu wa wanafunzi kujifunza,” alisema.