Ugonjwa wa kizunguzungu watesa wafugaji, waomba msaada serikalini

Muktasari:
- Ugonjwa huo unaosababishwa na minyoo aina ya taenia multiceps, ambao hutoa mayai yanayokua kuelekea kwenye ubongo wa mbuzi na kondo kisha kutengeneza uvimbe, mpaka sasa hakuna dawa ya kuudhibiti.
Arusha. Wafugaji wa Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, wameiomba Serikali kupitia taasisi zake husika kufanya utafiti wa kina kuhusu ugonjwa wa kizunguzungu, unaojulikana kitaalamu kama coenurosis.
Ugonjwa huo unasababishwa na minyoo aina ya taenia multiceps, ambao umekuwa ukisababisha vifo vya mbuzi na kondoo zaidi ya 40 kwa mfugaji mmoja kila mwaka.
Wakizungumza mbele ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashantu Kijaji wakati wa uzinduzi wa kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo wilayani humo leo Jumamosi Julai 5, 2025, wafugaji hao wamesema ugonjwa huo umekithiri, hasa kuelekea kipindi cha mvua za masika zilizonyesha kuanzia Februari hadi Machi.
“Katika lugha ya Kimasai ugonjwa huo hujulikana kama Ormilo, ukiashiria hali ya mnyama kupatwa na kizunguzungu, kukosa hamu ya kula, kudhoofika na hatimaye kufa ndani ya siku tatu hadi nne,”
Aliyekuwa Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Shangai amesema: “Tunaiomba Serikali kuharakisha juhudi za kutafuta tiba ya ugonjwa huu kwani kila mwaka tunapoteza mifugo wengi kipindi ambacho tunatarajia kunufaika na malisho ya kutosha.”
Aidha, akizungumzia ugonjwa huo, mfugaji Altapwai Mayanga amesema wasiwasi wake ni kuhusu athari zinazoweza kuwapata watumiaji wa nyama.
Amesema baadhi ya wafugaji akibaini mfugo wake unaumwa, huamua kuchinja na kuwauzia watu nyama au kupeleka kwenye mabucha.
Hivyo, amtoa tahadhari na kuiomba Serikali kuwa makini kwa kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji na kuchukua hatua ya kuudhibiti ugonjwa huo.
ameishukuru Serikali kwa kutoa chanjo, lakini ameiomba mwakani muda wa kuchanja upangwe mapema kati ya Februari na Machi kipindi ambacho mlipuko wa ugonjwa huo huanza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania, Dk Benezeth Lutege amesema ugonjwa huo hauna tiba hadi sasa na unaweza kuua mnyama ndani ya siku saba hadi 14 baada ya kuonyesha dalili za kizunguzungu.
Amesema minyoo hao huingia kwenye utumbo wa mnyama, kutaga mayai ambayo husambaa hadi kwenye ubongo na kusababisha uvimbe unaoleta kizunguzungu hadi mnyama anakufa. Amesisitiza umuhimu wa kuwapatia mifugo dawa za minyoo mara kwa mara ili kuzuia madhara hayo.
Dk Kijaji akizindua kampeni hiyo ya chanjo amesema mpango huo wa miaka mitano (2025–2029) unaogharimu Sh216 bilioni unalenga kuboresha afya ya mifugo, kuongeza usalama wa bidhaa za mifugo na kufungua fursa za masoko ya kimataifa.
Amesema utambuzi wa mifugo utasaidia kupata takwimu sahihi na kuongeza thamani ya mifugo na uchumi wa nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi amewataka wafugaji wote kujitokeza kuchanja mifugo yao ili kuepuka milipuko ya magonjwa na kuinua thamani ya mifugo yao na uchumi wa mkoa kwa ujumla.