Maeneo 14 kuleta mapinduzi Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji amewasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026 jijini Dodoma leo Mei 23, 2025
Dodoma. Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2025/26, yenye jumla ya Sh476.65, bilioni imepangwa kutekelezwa katika maeneo makuu 14, yakiwemo kukamilisha ujenzi wa Bandari ya Uvuvi katika eneo la Kilwa Masoko.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji, amewasilisha ombi kwa Bunge la kuidhinisha bajeti ya Sh476.65 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26, huku zaidi ya asilimia 78 ya fedha hizo (Sh375.13 bilioni) zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Amesema shughuli zilizofanyika kwa mwaka 2024/25 ni ujenzi wa gati lenye urefu wa mita za mraba 315, jengo la utawala asilimia 95 na kuzalishia barafu.
Dk Kijaji ametaja shughuli nyingine zilizofanyika ni ujenzi wa eneo la kuhifadhia, kuandalia samaki pamoja na soko la kuuzia samaki, vituo vya kusambazia maji safi, zimamoto, cha kupozea umeme na kuzalishia gesi ya naitrojeni.
Nyingine ni ujenzi wa miundombinu ya kuegesha magari, tanki za kuhifadhia mafuta na karakana ya kutengenezea meli.
“Katika Mwaka 2025/2026, Wizara itaendelea kuboresha miundombinu ya uvuvi ikiwemo kukamilisha Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko na kufanya upembuzi yakinifu pamoja na Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (ESIA) kwa ajili ya Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Bagamoyo,” amesema.
Ametaja shughuli nyingine ni zitakazofanyika katika mwaka 2025/26 ni kuanzisha kanzidata kwa ajili ya usajili na kutoa vitambulisho vya kidigitali kwa wadau wa Sekta ya Uvuvi wanufaike na kupata fursa mbalimbali za masoko.
“Wizara inaomba kupatiwa ikama yenye jumla ya nafasi 183 kwa ajili ya ajira mpya 89, uteuzi 3 upandishwaji vyeo 80, na ubadilishwaji wa kada 11,”amesema Dk Kijaji.
Shughuli nyingine ni kukamilisha kwa kukamilisha ujenzi wa minada 23, kuendelea kutekeleza Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa kwa kuzingatia Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP) na kuongeza uzalishaji wa mbegu za malisho kutoka tani 222.54 hadi kufikia tani 333.54 kwa kujenga miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba.
Pia, ametaja shughuli nyingine ni kuendelea na kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa na kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kuwezesha vijana kujiajiri kwa kuwekeza katika shughuli za ufugaji, uvuvi na ukuzaji viumbe maji kupitia programu ya kilimo biashara kwa vijana (BBT).
Amesema shughuli nyingine ni ununua na kusambaza pikipiki 200 kwa maofisa ugani na ununuzi wa boti 110 kwa ajili ya kukopeshwa kwa walengwa (hawakutajwa) kwa masharti nafuu.
Dk Kijaji amesema katika mwaka huo wa fedha, wizara hiyo itahuisha mwongozo wa utoaji huduma za ugani wa mifugo na uvuvi pamoja na kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za Uvuvi kwa kununua ndege nyuki mbili na kuweka maboya 79 ya kuonesha mipaka.
“Katika mwaka 2025/2026, Wizara itaendelea kuimarisha uzalishaji wa vifaranga na utoaji wa huduma bora za ugani kwa kusimamia na kuendesha vituo,”amesema Dk Kijaji.
Amesema pia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) itafanya tathmini ya kimazingira kwa ajili ya kuweka vizimba katika Bwawa la Mwalimu Nyerere na Ziwa Nyasa na Tangayika.
Amesema pia katika mwaka 2025/2026, Wizara imepanga kuwezesha mikopo yenye thamani ya Sh680 bilioni kwa sekta ya mifugo na uvuvi na kuendelea na mazungumzo na wafugaji pamoja na wavuvi na taasisi inayotoa dhamana ya mikopo (PASS).
Kwa upande wa vipaumbele, Dk Kijaji amesema wamepanga kutekeleza vipaumbele vinne katika mwaka 2025/26 ambavyo ni kuongeza uzalishaji, masoko na thamani ya mazao ya mifugo na uvuvi, kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za mifugo na uvuvi.
Vingine ni kuhamasisha uwekezaji katika Sekta za Mifugo na Uvuvi na Kuimarisha utafiti, mafunzo na huduma za ugani kwa sekta hiyo.
Michango ya wabunge
Akichangia katika mjadala huo Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Kenani amesema changamoto katika wizara hiyo ni fedha ndio maana wanashindwa kufanya vizuri na si usimamizi wala siyo makusanyo.
“Hadi kufikia wakati huu wamepata asilimia 28 ya bajeti (ya mwaka 2024/25) ndio wamepata hakuna muujiza unaweza kufanyika. Sekta hii ni muhimu sana sasa sijajua sisi kama Bunge tunatimiza wajibu wetu lakini fedha haziendi,” amesema.
Kenani, ambaye ameunga mkono Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara kuhusu suala hilo, amesema wanataka mapinduzi lakini hakuna mapinduzi yanayoweza kufanyika bila kupeleka fedha na kuwa jambo hilo haliwapendezi.
Mbunge wa Viti Maalumu, Naghenjwa Kaboyoka ameshauri ukubwa wa bajeti hiyo usiwe mbali na bajeti ya kilimo kwa kuwa wanataka lishe bora ambayo inatoka pia katika mifugo.
Aidha, ameshauri wizara hiyo kushughulika na changamoto ya kuzagaa katikati ya miji kwa mifugo, jambo ambalo ameliona jijini Dodoma.
Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM), Francis Mtinga ameshauri wizara hiyo kugawanywa kuwa wizara mbili ili kuleta ufanisi zaidi na kuwa kama Rais Samia Suluhu Hassan atazigawanya sekta mbili zitaleta mafanikio.
“Mimi naomba niwatoe hofu wanaodhani kwa kufanya hivi kutaongeza bajeti tukitenganisha sekta hizi mapato ambayo yatapatikana yatawezesha,” amesema.
Naye Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Constantine Kanyasu amesema vizimba vilivyowekwa katika ziwa Victoria, vimevamiwa na magugu maji na hivyo kusababisha kupungua kwa samaki katika ziwa hilo.
“Kuna upungufu wa karibu tani 700,000 za samaki, zinapungua kwa sababu mazalia ya samaki yanaendelea kupotea. Kadri siku zinavyoenda magugu maji yanatengeneza visiwa,” amesema.
Ameungana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara kwa kuitaka Serikali kufikiria jinsi ya kupambana na magugu maji kwenye ziwa hilo na kuwa katika ziwa Victoria samaki wanazidi kupungua kutokana na mazalia kuvamiwa na magugu maji.
Utitiri wa tozo, ubora, wizi wa mifugo
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, mjumbe wa kamati hiyo, Dk Medard Kalemani ameshauri Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kusimamia suala malisho katika kukabiliana na ubora mifugo nchini.
“Serikali iisimamie TALIRI ili ianzishe mashamba ya malisho katika Wilaya za Kifugaji. Aidha mashamba ya malisho ambayo yametelekezwa yafufuliwe. Serikali iisimamie TALIRI ili ianzishe mashamba ya malisho katika Wilaya za Kifugaji. Aidha mashamba ya malisho ambayo yametelekezwa yafufuliwe,”amesema.
Pia, amesema kamati inaishauri Serikali, kuimarisha doria za mara kwa mara katika vituo vyote vya mipakani ili kudhibiti utoroshwaji na uingizwaji wa mifugo, mazao ya mifugo na Uvuvi bila kulipia tozo.
Aidha, amesema ametaja wingi wa tozo katika Sekta za Mifugo na Uvuvi kuwa unakwamisha ukuaji wa maendeleo ya sekta hizo nchini na kusababisha maisha ya wafugaji na wavuvi kuendelea kuwa duni.