Uhaba wa walimu katikati ya wahitimu lukuki mitaani

Muktasari:

  • Shule za msingi na awali Tanzania zimeendelea kulia na uhaba wa walimu jambo ambalo linaongeza mzigo kwa walimu waliopo, huku takwimu zikionyesha kuwapo kwa wahitimu wengi wa kozi hiyo kwa miaka mitatu mfululizo.

Dar es Salaam. Serikali imepanga kuajiri walimu 12,000 katika mwaka wa fedha 2024/2025, lakini madarasa ya awali na msingi pekee yanahitaji walimu zaidi ya 116,885 ili kuweka sawa uwiano wa walimu kwa wanafunzi.

Hata hivyo, wakati shule zikiendelea kukabiliana na uhaba wa walimu, ripoti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) inaonyesha ualimu ndiyo kozi inayoongoza kwa kutoa wahitimu wengi vyuoni kwa miaka mitatu mfululizo.

Kwa mujibu wa Kitabu cha hali ya Uchumi wa Taifa 2023 kilichotolewa na Wizara ya Fedha, Juni 13, 2024, madarasa ya awali yalihitaji walimu 52,884 na shule za msingi zilihitaji walimu 64,001 ili kuwa na uwiano uliopangwa na Serikali.

Kufuatia hilo, wadau wa elimu wameitaka Serikali kufanya jitihada za makusudi ili kukabiliana na uhaba huo, wakidai kuwa haukupaswa kuwepo kwani kuna walimu wengi wanazagaa mitaani.

Takwimu zinaonyesha, madarasa ya awali mwaka 2023 yalikuwa na walimu 9,608 pekee ikilinganishwa na uhitaji wa walimu 62,491 katika mwaka 2023 ambao walipaswa kufundisha wanafunzi 1,562,286.

Kwa mujibu wa uwiano wa Serikali, walimu waliokuwapo walifundisha wanafunzi 163 ndani ya darasa moja ikiwa ni mara sita zaidi ya kiwango kilichowekwa na Serikali cha kufundisha wanafunzi 25.

Hata hivyo, idadi ya walimu wa madarasa ya awali waliokuwapo mwaka 2023 ni pungufu kwa asilimia 4.8 kutoka wanafunzi 10,093 waliokuwapo mwaka 2022. Idadi hiyo ya walimu ilishuka katikati ya ongezeko la wanafunzi kwa asilimia 8.8.

Hiyo ni baada ya wanafunzi katika shule za awali za Serikali waliodahiliwa kufikia 1,562,286 kutoka wanafunzi 1,435,735 mwaka 2022.

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 93 ya wanafunzi wote walioandikishwa katika madarasa hayo kwa shule za Serikali na binafsi.

Shule za msingi

Kitabu hicho cha hali ya uchumi kinaeleza idadi ya wanafunzi katika shule za Serikali ilikuwa milioni 10.82 mwaka 2023 ambayo ilikuwa ikihitaji zaidi ya walimu 240,541 ili kuweka uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45.

Badala yake shule hizo zilikuwa na walimu 176,540 ambayo ni pungufu ya walimu 64,001 kufikia uwiano halisi.

Idadi ya walimu waliokuwapo mwaka 2023 ilikuwa ni ongezeko la asilimia 1.8 ikilinganishwa na walimu waliokuwapo mwaka 2022.

Ongezeko hilo lilitajwa kuchochewa na kuimarika kwa mazingira ya kujifunzia na kufundishia ikiwemo utekelezaji wa programu ya elimu bila ada pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu.

Mitazamo ya wadau

Akizungumza na Mwananchi, mdau wa elimu, Mwalimu Richard Mabala amesema kama nchi inapaswa kufanya jambo la dharura ili kuinusuru elimu kwa kutafuta fedha zinazoweza kujaza pengo la walimu.

Amesema kinachofanyika sasa ni sawa na kuweka matone wakijaribu kuziba pengo, huku wakijikita katika ujenzi wa miundombinu iliyopo bila walimu haina faida.

“Mwalimu bila darasa anaweza kufundisha lakini miundombinu bila mwalimu haiwezekani, kupanga ni kuchagua sijui tumechagua nini, V8 moja (gari zinazotumiwa na Serikali) inaweza kulipa walimu wangapi kwa mwaka,” amesema Mabala.

Mhadhiri Dk Luka Mkonongwa amesema inasikitisha kuona hadi sasa shule zinazungumzia uhaba wa walimu wakati wapo mitaani wameandaliwa na wenye uwezo wa kufundisha ngazi zote.

“Hakuna hoja ya msingi wanayoweza kusema zaidi ya kuajiri, vyuo vimefundisha wahitimu wapo wengi mitaani ajira hakuna, siyo kwamba tuna uhaba wa walimu ila walimu wapo mitaani, idadi ya walimu waliopo wangetosha kuziba pengo na wengine kwenda kufanya kazi nje ya nchi,” amesema Dk Mkongongwa.

Amesema kinachokwamisha nchi ni vipaumbele kutengwa kisiasa huku suala la elimu likikosa umuhimu.

“Nchi haiwezi kuendelea kwa sababu kila sekta inahitaji mtu aliyepikwa vizuri, ili mtu apikwe anahitaji mwalimu, bila kufanya hivi tunajiandaa kutengeneza nchi ya wajinga na kubaki tukitegemea watu kutoka nje watusaidie kufanya kila kitu,” amesema Dk Mkonongwa.

Wahitimu waliopo

Kuhusu kuzalisha walimu wa kutosha, Ripoti ya Tume ya Vyuo vikuu Tanzania 2023 (TCU) iliyotolewa Mei 2024 inaonyesha kozi hiyo imekuwa ikiongoza kwa kutoa wahitimu wengi kuliko nyingine.

Ripoti za miaka tofauti za TCU zinaonyesha mwaka 2023, walimu waliohitimu walikuwa 15,103, mwaka 2022 walikuwa 15,335 huku mwaka 2021 wakiwa 14,050.

Idadi ya wahitimu inaakisiwa na wingi wa wanaodahiliwa na mwaka 2023/2024 kati ya wanafunzi 106,570 waliodahiliwa kuanza mwaka wa kwanza katika kozi 17 zilizoainishwa, waliochagua ualimu walikuwa 27,731.


Walimu wazungumza

Mwalimu kutoka moja ya shule wilaya Morogoro vijijini aliyeomba hifadhi ya jina lake ameiomba Serikali kuangalia namna inavyoweza kuboresha mazingira ili walimu wasikimbie vituo vya kazi.

“Hapa ninavyokuambia tupo watatu, nyumba zenyewe ambazo mwalimu anaweza kukaa hakuna, tunaishi umbali mrefu, kuifikia shule ni kazi unafika umechoka na mzigo wa wanafunzi kuanzia darasa la awali hadi la saba ni mkubwa,” amesema mwalimu huyo.

Mwalimu mwingine kutoka wilaya Buhigwe, Mkoa wa Kigoma amesema mbali na uhaba walionao pia wanakumbana na changamoto ya watoto wa maeneo husika kutojua Kiswahili jambo linaloongeza kazi.

“Kabla ya kuwa na vipindi vingi lazima uone utashughulika vipi na lugha gongana, mzigo ni mkubwa, inafika wakati tunapoingia Julai  nguvu kubwa tunahamishia madarasa ya mitihani pekee ili tupate matokeo mazuri,” amesema mwalimu huyo.


Kauli za Serikali

Kwa nyakati tofauti bungeni jijini Dodoma, Serikali imekuwa ikiweka bayana mpango wake wa kuajiri walimu 12,000 katika mwaka wa fedha 2023/24 ili kukabiliana na upungufu uliopo.

Hayo yamekuwa yakielezwa na viongozi kutoka ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ikiwa ni mwendelezo wa ajira zilizoanza kutolewa kila mwaka tangu 2020/2021.