Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uhitaji wanaotafuta huduma CCBRT Moshi wazidi uwezo

Geradina Matuba akiwa na mdogo wake Gracious Matuba katika kituo cha huduma za utengamao kwa watoto cha CCBRT kilichopo Kaloleni, Moshi.

Muktasari:

  • Maelfu ya watoto nchini huzaliwa kila mwaka na changamoto za kiafya ambazo zinaweza kutibika ikiwa watapata huduma kwa wakati, lakini wengi hukosa matibabu kutokana na changamoto za kifedha zinazozikabili familia zao.

Moshi/Dar. Kituo cha Utengamao cha CCBRT Moshi, kinachohudumia mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara, kinapokea zaidi ya watoto 1,000 wenye ulemavu kila mwaka, huku mahitaji ya huduma yakiongezeka kuliko uwezo wa rasilimali zilizopo.

Katika ziara ya Mwananchi iliyofanyika Juni 29, 2026, katika kituo hicho kilichopo Kaloleni, nje kidogo ya mji wa Moshi, ilibainika kuwa ongezeko la uelewa kwa wazazi kuhusu umuhimu wa kuwapeleka watoto wenye ulemavu mapema limechangia idadi kubwa ya watoto kufikishwa kituoni kwa ajili ya huduma za mazoezi ya utengamao, vifaa tiba saidizi na huduma nyingine za urekebishaji.

Hali hiyo inajitokeza wakati ambapo Hospitali ya CCBRT ilizindua kampeni ya kitaifa ya kuchangisha Sh3 bilioni Juni 3 mwaka huu, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na upungufu wa fedha baada ya kupungua kwa ufadhili wa wafadhili wa nje, hali iliyodhoofisha uwezo wa kutoa huduma kwa watoto wasio na uwezo.

Geradina Matuba akiwa na mdogo wake Gracious Matuba katika kituo cha huduma za utengamao kwa watoto cha CCBRT kilichopo Kaloleni, Moshi.

Mkuu wa Huduma za Utengamao wa CCBRT Moshi, Sabas Kimario, amesema tofauti na miaka ya nyuma, sasa wazazi wengi wameelimika na wanawaleta watoto wao mapema, jambo linaloongeza nafasi ya watoto hao kupata maendeleo bora zaidi ya kiafya na kiakili.

Amesema kituo kinatoa huduma mbalimbali ikiwemo mazoezi maalumu ya utengamao, utoaji wa vifaa saidizi kama viti mwendo na vifaa vya kusimamia na kutembea, pamoja na kliniki ya watoto wenye tatizo la nyayo zilizopinda (clubfoot) inayotolewa bure kila Ijumaa. Aidha, kituo kimeanzisha mtandao wa vituo 30 vya huduma katika vituo vya afya vya Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ya Moshi, pamoja na kufanya ziara za kuwafikia watoto katika jamii kupitia huduma za ‘outreach’.

Hata hivyo, Kimario amesema changamoto kubwa iliyopo sasa ni upungufu wa fedha kutokana na baadhi ya wafadhili kupunguza au kusitisha misaada yao kufuatia athari za changamoto mbalimbali za kimataifa ikiwemo COVID-19, hali inayoathiri uendelevu wa huduma.

Mtoa huduma za utengamao katika jamii wa CCBRT Moshi, Eltruda Materu, amesema changamoto nyingine ni ugumu wa kuwafikia watoto wanaoishi vijijini kutokana na miundombinu duni na gharama za usafiri kupanda. Amesema mara nyingi hulazimika kutumia usafiri wa umma na wakati mwingine kutembea zaidi ya kilomita sita kufikia familia zinazohitaji huduma, hasa kipindi cha mvua.

Aidha, amesema bado jamii ina mitazamo potofu kuhusu ulemavu, ambapo baadhi ya familia huamini watoto wenye ulemavu, hususan wenye mtindio wa ubongo, wamerogwa badala ya kuelewa kuwa hali hiyo inaweza kusababishwa na matatizo ya kiafya wakati wa ujauzito au kujifungua.

Mkazi wa Moshi, Rosen Kiwelu akiwa na mtoto wake Michael Leonardo katika kituo cha CCBRT Moshi wakati wa huduma za utengamao.

Kwa upande wake, mtaalamu wa tiba kwa vitendo na vifaa saidizi, Neofilta Kiringitwa, amesema kila mtoto hupimwa kabla ya kutengenezewa kiti mwendo maalumu kinachokidhi mahitaji yake. Amesema matumizi yasiyo sahihi ya vifaa hivyo yanaweza kusababisha madhara kama kupinda kwa mgongo, kufupika kwa misuli na vidonda vya mgandamizo.

Amesema gharama ya kiti mwendo ni zaidi ya Sh500,000, jambo linalowafanya watoto wengi kushindwa kuvipata bila msaada wa wafadhili au wadau wa maendeleo.

Licha ya changamoto hizo, baadhi ya watoto wameendelea kunufaika na huduma za CCBRT, ambapo wameweza kuendelea na masomo hadi vyuo vikuu na wengine kujitegemea katika maisha yao ya kila siku.

Mlezi Geradina Matuba amesema mtoto wake Gracious Matuba amebadilika baada ya kupata huduma hizo, akieleza kuwa sasa anaweza kukaa vizuri, kwenda shule ya kawaida, kucheza na watoto wengine na kushiriki shughuli za kijamii ikiwamo kwenda kanisani.