Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uingizaji gesi ya kupikia nchini wapaa

Muktasari:

  • Ripoti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura),  inaonyesha kuwa, mikoa ya kanda ya Pwani inatumia asilimia 44 ya gesi yote, huku Oryx Gas, Taifa Gas, na Manjis Gas zikiongoza katika soko.

Dar es Salaam. Ongezeko la mahitaji ya gesi ya kupikia nchini lililochochewa na kampeni ya nishati safi, linatajwa kukuza uingizaji wake kutoka nje ya nchi kwa zaidi ya asilimia 100 ndani ya miaka sita.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ya mwaka ulioishia Juni 2023, uingizaji wa gesi nchini umeongezeka hadi kufikia futi za ujazo 293,167 mwaka 2022/23 kutoka futi za ujazo 120,961 mwaka 2017/18.

Kiwango cha gesi kilichoingizwa mwaka 2022/23 kwa mujibu wa Ewura ni ongezeko ikilinganishwa na futi za ujazo 252,023 zilizoingizwa mwaka uliotangulia.

 “Kukua kwa uingizaji huu kumetokana na kuongezeka kwa uelewa wa matumizi ya gesi katika kupikia dhidi ya njia asili zilizokuwa zikitumika kama nishati ya kupikia,” inaeleza sehemu ya ripoti ya Ewura.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wakati uingizaji wa gesi ukizidi kupaa, umechochea ongezeko la sehemu za kuhifadhia kutoka kuwa na uwezo wa kutunza futi za ujazo 8,050 mwaka 2017/18 hadi futi za ujazo 15,750.

“Katika matumizi, mikoa ya kanda ya Pwani inayojumuisha Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Mtwara, Lindi na Ruvuma inatumia asilimia 44 ya gesi yote inayoingizwa nchini ikifuatiwa na mikoa ya kaskazini inayojumuisha Arusha, Kilimanjaro na Manyara iliyo na asilimia 23,” inaeleza ripoti.

Kanda ya ziwa inayojumuisha Mwanza, Mara, Geita, Shinyanga, Kagera na Simiyu na kanda ya kati yaani Dodoma, Singida, Kigoma na Tabora zikiwa na asilimia 11 na 12 mtawalia. Huku mikoa inayobakia ikitumia asilimia nane.

Oryx Gas ndiyo inabeba asilimia 38 ya soko lote, Taifa Gas ikiwa na asilimia 26 na Manjis Gas ikiwa na asilimia 18, huku Lake Gas, O Gas, Orange Gas, Cam Gas, Mount Meru Gas na Puma Gas zikimiliki soko kwa asilimia 11, 4, 2, 1, 0.4 na 0.1 mtawalia.

“Uingizaji gesi unaweza kuwa unaongezeka lakini bei bado zinatuumiza, iangaliwe namna ya kupunguza bei. Mkaa unaweza kupata wa Sh1,000, Sh2,000 lakini gesi bado hadi uwe na Sh25,000 na kuendelea,” anasema Lydia Koka, mkazi wa Tabata.

Kwa upande wake, Nicolas David anasema bei ya gesi inaongeza gharama za uendeshaji biashara yake.

“Gesi yangu ikiisha bila Sh50,000 hupati, itafutwe namna, maana wametuvuta kutoka kwenye kuni, watufanye sasa tusipate sababu ya kurudi huko,” anasema David.

Tanzania imedhamiria kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanaachana na matumizi ya kuni na mkaa ifikapo mwaka 2030.

Ili kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia, Meneja Mkuu wa Kampuni ya O Gas, Usama Mohammed Sheikh ametaka kuondolewe kodi ya baadhi ya vifaa vinavyosaidia matumizi ya gesi, yakiwamo majiko.

“Mitungi haina kodi ila majiko na vifaa vingine vinavyopaswa kutumika vina kodi, endapo itaondolewa gharama kwa watu wanaoanza kutumia gesi zitapungua,” anasema Sheikh.

Pia, anataka kuwapo unafuu wa kodi kwa watu wanaotaka kuwekeza katika miundombinu ya ujazaji gesi nchini ili kuwavutia wengi.

“Itolewe ahueni kwao, soko la gesi ni kubwa kutokana na mahitaji yake, hivyo uwekezaji unahitajika na hii ndiyo njia inayoweza kuwavutia wengi,” anasema Sheikh.


Gesi asilia

Kukosekana fedha za uhakika kunatajwa kuwa moja ya sababu inayochangia usambazaji gesi asilia majumbani kufanyika kwa kasi ndogo.

“Hata hivyo, baada ya kuzinduliwa mkakati wa uwezeshaji nishati safi na sisi tumeandaa mpango utakaowezesha kuunganisha asilimia 50 ya nyumba zilizopo Jiji la Dar es Salaam ndani ya miaka 10,” anasema Antony Karomba, Mhandisi wa gesi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Anasema kupitia mkakati huo, fedha za mfuko wa nishati safi zitakuwa zikitumika na bajeti itakuwa ikitengwa kuchochea usambazaji wa gesi asilia.

Tayari nyumba 1,514 zimeunganishwa na huduma hiyo jijini Dar es Salaam, huku nyingine 980 zikiwa katika hatua za kuunganishwa katika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani na Mkoa wa Lindi. Mradi umefadhiliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).

Katika mwaka huu wa fedha, nyumba 1,899 zilizoko Ikwiriri, Mkuranga na Mtwara zinatarajiwa kuunganishwa na gesi asilia.

“Mtu akiunganishiwa gesi hii anakuwa ananunua kama anavyonunua Luku kwa kutumia mitandao ya simu na atatumia kwa kiwango alichonunua,” anasema Karomba.

Akizungumzia matumizi ya nishati safi, mtaalamu wa uchumi,  Oscar Mkude anasema Tanzania ina vyazo vingi vizuri vya nishati hiyo kama vile jua, upepo na joto ardhi lakini kwa sasa vyanzo hivyo vinachangia kidogo kwenye uzalishaji umeme.

“Wawekezaji wapo wengi wanaotamani kuja kuwekeza kwenye sekta hii. Muhimu ni kuweka mazingira yanayovutia. Kwa mfano, wawekezaji wengi hutaka government guarantee ili kukopesheka kwa bei nafuu na taasisi za fedha,” anasema.

Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Haji Semboja anasema ukuaji wa matumizi ya gesi unaashiria kukua kwa ufahamu juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na athari ambazo watu wanaweza kuzipata wakitumia nishati nyingine zikiwamo kuni na mkaa.

“Uelewa unakua lakini kwa wakati huu tunaweza kutumia gesi ya kupikia kutoka nje katika kipindi cha mpito kwa sababu tunayo gesi asilia ya kutosha ikishakaa vizuri Tanzania hatupaswi kuagiza kutoka nje,” anasema.