Ujumbe wa Tabwa kwa wanawake

Dar es salaam. Uongozi wa Chama cha wafanyabiashara Wanawake Tanzania  (Tabwa) umewapongeza wanawake wote waliojitokeza kutangaza bidhaa zao kwenye maonesho  yaliyofanyika  Mlimani City kuanzia Machi 4 hadi 7, 2021.

Pongezi hizo zilitolewa Dar es Salaam leo Jumatatu Machi 8, 2021 na mkurugenzi wa Tabwa, Noreen Mawalla ikiwa ni siku moja imepita baada ya kufungwa rasmi kwa maonesho hayo yaliyofanyika kwa siku tatu na  kuwakutanisha washiriki 120 wazalishaji kutoka sekta mbalimbali ikiwemo usindikaji wa nafaka.

Amesema ushiriki wa maonesho hayo isiwe mwisho kwa mahusiano yao na kwa sasa wanachokifanya ni kulegeza masharti ili wanawake wote wenye biashara ndogondogo wajiunge na Tabwa ambacho malengo yake ni kuwainua wanawake kiuchumi.

Amesema maonesho hayo yatakuwa yanafanyika kwa mwaka mara mbili, Machi  na Novemba na kuanzia msimu ujao itakuwa kama sehemu ya kutangaza utalii wa ndani ambapo yatafanyika nje ya mkoa wa Dar es Salaam.

"Tabwa kwa kushirikiana na wadhamini wetu mipango yetu ni kuwafikisha wafanyabiashara wanawake mbali kwanza maonesho yetu yatakuwa sehemu ya kutangaza utalii wa ndani, lakini pia baada ya kuisha janga la ugonjwa unaosababisha na virusi vya corona tutaandaa kongamano la kupeleka bidhaa zetu nje ya nchi kama omani,” amesema Noreen.

Noreen amesema washiriki waliopeleka bidhaa zao kwenye maonesho hayo watakuwa changuo la kwanza ingawa bado wanahamasisha na wanawake wengine wajitokeza kujiunga na chama hicho.

 Consolanta Shayo ambaye ni meneja mahusiano wa benki ya NBC iliyokuwa mdhamini mkuu wa maonyesho hayo amewapongeza wanawake kwa kujitokeza kwa wingi," nawapongeza mnaweza lakini mnachotakiwa ni kuhakikisha bidhaa zenu zinakuwa bora na safi kuendana na mahitaji ya walaji.”

“Tutengeneze vitu ambavyo hata vikinunuliwa na watu wa nje  huko viendako vikawe mabalozi wazuri na hiyo itatufanya kuteka soko kirahisi," amesema Shayo