Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ukimwi bado tishio, kinara kusababisha vifo nchini

Dar es Salaam. Wakati magonjwa 20 yakitajwa kuwa chanzo cha zaidi ya nusu ya vifo vyote nchini Tanzania, magonjwa ya mfumo wa upumuaji, kukosa hewa baada ya kuzaliwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi ni kinara.

Hiyo ni kwa mujibu wa takwimu za matukio muhimu ya binadamu 2023 zilizotolewa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita) zilizotolewa Septemba 2024.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, kiwango cha vifo kinachotokana na magonjwa 20 kimeongezeka kutoka asilimia 63.5 mwaka 2020 hadi asilimia 63.5.

Hiyo inatajwa huenda inachochewa na ongezeko la mzigo katika baadhi ya magonjwa hususani mwaka 2023 katika upande wa ugonjwa wa kukosa hewa, kiwewe wakati wa kujifungua na malaria.

Maambukizi ya mfumo wa upumuaji yaliibuka kuwa magonjwa yaliyoongoza kusababisha vifo baada ya kuchukua asilimia 9.9 ya vifo vyote, ikifuatiwa na kukosa hewa baada ya kuzaliwa (7.9) na Ukimwi ambao ulichangia kwa asilimia 6.3.

Magonjwa ya mfumo wa upumuaji yamekuwa chanzo kikuu cha vifo kwa miaka mitatu mfululizo na kupungua kwa asilimia sita, kutoka asilimia 15.9 mwaka 2021 hadi 9.9 mwaka 2023.

Cha kushangaza upungufu wa damu ni kati ya sababu kuu za vifo vya uzazi duniani kote. Lakini haikutajwa kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya vifo mwaka 2023.

Hii inaweza kuwa imetokana na juhudi za Serikali za kupunguza vifo vya uzazi nchini, zilizotokana na ugawaji wa dawa ‘folic acid’ kwa wajawazito.

Ukosefu wa hewa wakati wa kuzaliwa na vifo vitokanavyo kifafa cha mimba vimeendelea katika nafasi mbili za juu kwa miaka minne iliyopita, ikichukua wastani wa asilimia 8.4 ya vifo vyote.

Malaria imesalia katika tano bora tangu mwaka 2020 na kusababisha wastani wa asilimia 4.4 ya vifo katika kipindi hicho. Walakini, ilipungua kutoka asilimia 6 mwaka 2020 hadi asilimia 4.4 kwa mwaka 2023.

Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea amesema Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha inaendelea kudhibiti athari zinazoweza kutokana na magonjwa ya mfumo wa upumuaji na kukosa hewa baada ya kuzaliwa.

Amesema mara nyingi sababu za magonjwa ya mfumo wa upumuaji zinatofautiana kati ya watoto na watu wazima, hivyo jitihada mbalimbali zinafanyika kukabiliana nalo.

 Amefafanua kuwa  kwa upande wa watoto wa umri tofauti ikiwemo kuanzia chini ya mwezi mmoja, miongoni mwa sababu za kupata changamoto hiyo ni nimonia au kuzaliwa kabla ya kufikisha umri au kupata matatizo wakati wa kuzaliwa.

“Ili kudhibiti hali hii hasa nimonia, tumekuwa tukitoa chanjo ili watoto wasiathiriwe, hivyo kufanikiwa kupunguza watoto wanaopata nimonia nchini,” amesema.

Hilo limeenda sambamba na uboreshaji wa huduma ikiwemo uanzishwaji wa wodi maalumu 27 kwa ajili ya matibabu ya watoto wachanga, wagonjwa na waliozaliwa na uzito pungufu (Neo-natal Care Unit –NCU na kuweka wataalamu wanaotoa huduma kwenye wodi hizo.

Hata hivyo, Dk Nyembea pia amesema matumizi ya kambi za madaktari bingwa kwenda katika hospitali za ngazi za chini kuwafundisha namna ya kutoa huduma katika wodi hizo maalumu, imekuwa ikisaidia katika kukabiliana na magonjwa hayo.

“Tunafanya hili kwa sababu takwimu zinaonyesha asilimia 80.5 ya Watanzania wote hivi sasa wanapata huduma za afya ndani ya kilomita tano katika maeneo wanayoishi, ikitokea inahitajika huduma ya ngazi ya juu zaidi kuna gari za wagonjwa zitakazosaidia kuwawahisha kinamama kwenye kituo husika,”amesema Dk Nyembea.

Kwa upande wa changamoto ya mfumo wa upumuaji kwa watu wazima amesema moja ya jambo lililofanywa na Serikali ni kuhakikisha hospitali zote za mikoa zina chumba cha uangalizi maalumu (ICU) cha kisasa na wataalamu sambamba na uboreshaji huduma za dharura.

Kuhusu Ukimwi amesema jitihada mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kudhibiti kuendelea kuenea kwa ugonjwa huo. Kwa sasa uhamasishaji unafanyika hadi ngazi ya kijiji ili watu wajue namna ya kujilinda na kuepuka.

Magonjwa mengine

Magonjwa mengine yaliyorekodi idadi kubwa ya watu waliofariki dunia ni kuzaliwa kabla ya wakati na uzito mdogo wa kuzaliwa iliyokuwa na asilimia 3.9, ajali za barabarani 3.3, magonjwa ya kiharusi asilimia 3.3, Nefriti na nefrosi asilimia 3.2, kisukari 2.9, kifua kikuu 2.4, utapiamlo unaotokana na ukosefu wa protini na nishati asilimia 1.8, matatizo ya homoni 1.7, magonjwa ya kuhara 1.3 na ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo umechukua asilimia 1.2.

Magonjwa kama maambukizi ya njia ya juu ya hewa, matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo, magonjwa ya moyo ya uvimbe, ugonjwa wa ini (cirrhosis) yalichangia asilimia 1.1 kila moja katika vifo vyote vilivyotokea, huku melanoma na saratani nyingine za ngozi zikiwa na asilimia 1.

Sababu za vifo kwa jinsia

Katika mwaka 2023, vifo vilivyotokana na ajali za barabarani vilichangia asilimia 4.9 ya vifo vya wanaume, wakati kwa wanawake vilikuwa asilimia 1.5.

Pia takwimu zilionyesha kuwa vifo vinavyotokana na ajali za barabarani kwa wanaume vilizidi vile vya malaria kwa mara ya kwanza kama sababu kuu ya vifo kwa mwaka 2023.

Asilimia ya vifo kutokana na magonjwa yanayohusiana na maambukizi ya njia ya chini ya upumuaji na ugonjwa wa kisukari pia ilikuwa juu kidogo kwa wanaume  kwa asilimia 9.9 na  asilimia 2.9, ikilinganishwa na wanawake iliyokuwa asilimia 10.1 na asilimia 2.9, mtawaliwa.

Kinyume chake, asilimia ya vifo vinavyosababishwa na Virusi vya Ukimwi  (VVU) na shinikizo la damu ilikuwa juu kidogo kwa wanawake kwa asilimia 7.2 na 5.2, ikilinganishwa na asilimia 5.5 na asilimia 4.1 kwa wanaume.

Asilimia ya vifo vinavyosababishwa na malaria kati ya jinsia zote mbili kwa asilimia 4.3 kwa wanawake na asilimia 4.5 kwa wanaume.

Kifua kikavu cha kuzaliwa na majeraha wakati wa kuzaliwa ni sababu kuu za vifo miongoni mwa watoto walio chini ya miaka 5, zikichangia wastani wa zaidi ya asilimia 20 ya vifo vyote vya watoto walio chini ya miaka mitano.