Ukiugua maradhi ya mfumo wa upumuaji zingatia haya

Ukiugua maradhi ya mfumo wa upumuaji zingatia haya

Muktasari:

  •  Watu wanaougua maradhi ya mfumo wa upumuaji ikiwemo nimonia, wameshauriwa kufuata taratibu za namna ya upumuaji na staili za kulala kama sehemu ya tiba mazoezi ili kupona haraka.


Dar es Salaam. Watu wanaougua maradhi ya mfumo wa upumuaji ikiwemo nimonia, wameshauriwa kufuata taratibu za namna ya upumuaji na staili za kulala kama sehemu ya tiba mazoezi ili kupona haraka.

Mazoezi hayo yanayohusisha namna ya kukaa, kulala na kupumua ambayo yametajwa kusaidia uondoshaji wa maji na makohozi yanayokaa kwenye mapafu ya mgonjwa.

Mtaalamu wa fiziotherapia ‘tiba mazoezi’ kutoka hospitali ya Aga Khan, Christopher Nyoni alisema mazoezi hayo yanawafaa wagonjwa waliopata changamoto za upumuaji majumbani au wakiwa hospitali.

“Kuna huduma ya aina fulani ya mazoezi ya kifua kwa ajili ya kumsaidia mtu kupumua vizuri au kutoa yale majimaji yaliyokaa katika mapafu, kwa hiyo kuna namna ambayo tunafanya au tunamshauri mtu aliyekuwepo nyumbani nini afanye ili apumue vizuri.

“Mara nyingi wagonjwa wanaopata nimonia zile sehemu katika mapafu ambazo hewa pamoja na damu zinabadilishana, eneo ambalo damu inapata hewa safi zinakuwa zinajaa maji au makohozi kwa hiyo ndiyo zinasababisha mtu anashindwa kupumua,” alisema.

Nyoni alisema mgonjwa hushindwa kupumua kwa kuwa sehemu za chini za mapafu ndiyo huwa zinapata shida na muda wote hutumia sehemu za juu, hivyo hewa hushindwa kufika sehemu za chini za mapafu kutokana na maji au makohozi hukaa humo, hivyo kumfanya mtu aheme juu juu.

Alisema mgonjwa anatakiwa kufundishwa na kusimamiwa avute pumzi nyingi ndani kwa sekunde tatu na kuitoa vivyo hivyo kama zoezi la dakika kadhaa.

“Tunamfundisha atulie na avute hewa ndani kwa nguvu na kwa muda wa sekunde tatu na aitoe kwa muda ule ule, zoezi hili litamfanya mgonjwa apate ahueni kwa haraka,” alisema.

Nyoni analitaja zoezi jingine kuwa ni kumwekea mto na alale kifudifudi kwa staili ya kunyanyua tumbo juu na kichwa kiwe chini huku mto ukipita kifuani.

“Zoezi hili linasaidia kuondoa maji na makohozi na wakati huo wote anatakiwa aendelee kuvuta pumzi ndani na kuitoa nje. Unaweza pia kutumia fursa hiyo kugonga kifua chake taratibu pale unakuwa unatengeneza mfumo ili huyu mtu akohoe na ayatoe yale maji au makohozi na akishayatoa unakuta anaanza kupumua vizuri. Kama mtu yupo nyumbani unaweza kumwelekeza,” alisema Nyoni.

Alisema zoezi la kupumua linatakiwa kuanza taratibu na katikati ya zoezi inahitajika kasi na mwishoni kabla ya kumaliza lifanyike taratibu.

Akionyesha namna ya kuyaondoa makohozi au maji kwenye mapafu kwa mgonjwa aliyezidiwa, Nyoni alisema, “Anakaa kwa kupiga magoti, unainamisha kichwa chake chini anabinuka, kisha aanze kupumua kuingiza hewa ndani na kuitoa kwa kipindi cha nusu saa au zaidi, inasaidia maji kutoka nje na atapona haraka.”

Aliitaja zoezi jingine kuwa mgonjwa anatakiwa alale kifudifudi kama anaogelea, “Unachukua mto unaulalia kwa kuweka kifuani, kisha avute hewa ndani kwenda nje kwa muda mrefu, kwa kuwa sehemu ya mapafu ipo zaidi nyuma kuliko mbele inasaidia kuachia mapafu yaweze kufunga na kufungua. Pia staili nyingine anauweka mto kichwani.

“Pia unaweza kulalia ubavu kwa pembeni na ukaweka mto kama mama ana mimba kuna staili anazoweza kuzitumia kuhakikisha anakua sawa.”

Mgonjwa asilale chali

Wataalamu wanasema mtu anayeugua maradhi ya nimonia na mengine ya mfumo wa mapafu si salama kwake kulala chali.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mfumo wa hewa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Elisha Osati alisema mgonjwa anavyolala chali upumuaji wake unakuwa si mzuri.

“Hii staili hatuiruhusu kulala kwa mgonjwa mwenye matatizo ya kupumua. Katika kulala inategemea mgonjwa anajisikia yupo comfortable kiasi gani, mara nyingi pafu la kulia huanza kushambuliwa zaidi la kushoto, hivyo mgonjwa mwenyewe ataona alale upande gani,”alisema.

Dk Osati alisema ni vema mgonjwa akatumia mto au kitanda kiwe kimenyenyuliwa angalau nyuzi 45 na ikiwezekana kinyanyuliwe juu zaidi, kwani inamsaidia kunyanyua mapafu hewa iweze kupatikana vizuri.