Ukusanyaji kodi ya majengo kufanyika kwenye manunuzi ya Luku

Ukusanyaji kodi ya majengo kufanyika kwenye manunuzi ya Luku

Muktasari:

  • Serikali imesema itafanya marekebisho kwenye Sheria ya kodi ya majengo  sura 289 ili ukusanyaji wa kodi ya majengo ufanyike kwa kutumia mfumo wa ununuzi na utumiaji wa umeme kupitia mashine za Luku.

Dar es Salaam. Serikali imesema itafanya marekebisho kwenye Sheria ya kodi ya majengo  sura 289 ili ukusanyaji wa kodi ya majengo ufanyike kwa kutumia mfumo wa ununuzi na utumiaji wa umeme kupitia mashine za Luku.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Juni 10, 2021 na Waziri wa Fedha na Mpango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bungeni bajeti kuu Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Amesema kila mita ya umeme ina uhusiano na mmiliki wa jengo au mtumiaji wa mita, na kwa kuwa sheria ya kodi ya majengo inataka kodi hiyo ikusanywe kwa mmiliki au mtumiaji wa jengo, hivyo anapendekeza kodi ya majengo ya kiwango cha Sh1,000 kwa mwezi kwenye nyumba za kawaida zenye mita moja na itakatwa kwenye ununuzi wa umeme Luku.

“Napendekeza kiwango cha Sh5,000 kwa mwezi kwa kila ghorofa au apartment zenye mita moja na itakatwa kwenye ununuzi wa umeme (Luku). Serikali itaweka utaratibu kwenye nyumba za kawaida na za ghorofa zinazochangia mita moja na zinazotumia mita zaidi ya moja,” amesema.