Ukuta wakatisha uhai watoto wa familia moja

Ukuta wakatisha uhai watoto wa familia moja

Muktasari:

  • Watoto wawili wa familia moja wamefariki baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba chanzo kikitajwa kuwa ni mvua inayoambatana na upepo iliyonyesha wilayani Geita juzi Jumapili Januari 24, 2021.

Geita. Watoto wawili wa familia moja wamefariki baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba chanzo kikitajwa kuwa ni mvua inayoambatana na upepo iliyonyesha wilayani Geita juzi Jumapili Januari 24, 2021.

Waliofariki  ni Asheri Malima(4) na Laurencia Malima (2) waliokuwa wakiishi kijiji cha Kasesa kata ya Kaseme.

Akizungumza leo Jumanne Januari 26, 2021 baba wa watoto hao, Malima Kengere amesema aliwaacha wanae  tisa nyumbani na kwenda kuuza mahindi ya kuchoma lakini mmoja wa watoto wake alimfuata na kumueleza kuwa nyumba yao imeanguka.

Ukuta wakatisha uhai watoto wa familia moja

Amesema wakati ukuta ukianguka watoto hao walikuwa wenyewe nyumbani.

“Walipoona ukuta unaanguka walikimbia lakini hawa wawili walikuwa wadogo hawakuweza, walifukiwa na kifusi,” amesema akibainisha kuwa siku hiyo mvua ilinyesha kuanzia saa nane mchana hadi saa 10 jioni.

Mmoja wa watoto walionusurika, Leokadia Malima amesema akiwa sebuleni alisikia kishindo cha jiwe alikimbia na aliwaona wadogo zake lakini baada ya ukuta kuanguka alibaini kuwa wapo waliokuwa wamebaki ndani.

Kamanda wa polisi mkoani Geita,  Hendry Mwaibabe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wazazi kuwa waangalifu hasa nyakati za mvua ili kuepuka majanga yanayoweza kuzuilika.