Ummy: Imani za kishirikina kiini wajawazito kutoanza kliniki mapema


Muktasari:

  • Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema licha ya Serikali kupunguza vifo vya mama na mtoto, pamoja na mimba za utotoni, bado kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wajawazito kutowahi kliniki.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema licha ya Serikali kupunguza vifo vya mama na mtoto, pamoja na mimba za utotoni, bado kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wajawazito kutowahi kliniki.

Waziri Ummy ameyasema hayo wakati akihitimisha mafunzo ya siku tatu yaliyowaunganisha waandishi wa habari, watafiti na wadau wengine wa masuala ya haki ya afya ya uzazi kupitia mradi wa uchechemuzi wa masuala hayo mijini na Vijijini.

Kwa mujibu wa waziri huyo mwenye dhamana ya afya, imani za kishirikina zinachangia wajawazito wengi kutoanza kliniki mapema kwa hisia kwamba wakijulikana kuwa wameshika ujauzito, basi wanaweza kulogwa.

"Mjamzito kuanza kliniki mapema ni muhimu sana, maana kuna kufanyiwa vipimo, kuingizwa katika mchakato wa dawa za folic acid pamoja na dawa za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa wale watakaogundulika kuishi na Virusi vya Ukimwi (VVU)," amesema.

Naye Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi Mkoa wa Dar es Salaam, Agness Mgaya amesema moja kati ya changamoto ambazo wamekuwa wakikumbana nazo katika utoaji wa huduma hizo, ni pamoja na wajawazito kuchelewa kuanza kliniki.

Mgaya amesema kitaalamu inashauriwa mwanamke anapogundua tu ni mjamzito anapaswa kuanza kliniki mapema chini ya wiki 12.

Hata hivyo, mratibu huyo amebainisha kuwa, kwa Mkoa wa Dar es Salaam, ni asilimia 23 ya wajawazito; ndiyo hufika katika vituo vya afya kwa ajili ya kuanza kliniki, pale mimba inapokuwa chini ya wiki 12, japo malengo ya serikali ni kufikia asilimia 60.

"Kuchelewa kuanza kliniki kunaweza kusababisha kupoteza mimba na hata watoto, hivyo niwaombe waandishi wa habari kutusaidia kuendelea kuelimisha jamii kuhusu masula ya afya ya uzazi," amesema.

Aidha, Agnes amesema kuwa, hata wanaowahi kuanza kliniki, wamekuwa wakigundulika na upungufu wa damu, na kwamba wengi wao hukutwa wakiwa na damu gramu 8.

Na kwamba baadhi ya wajawazito, pia wamekuwa hawazingatii matumizi ya dawa za folic acid pamoja na zile za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, hasa kwa wajawazito ambao wanaishi na maambukizi ya VVU.

Ameongeza kuwa pamoja na Serikali kufanya jitihada ya kujenga vituo vya afya na kuongeza vifaa tiba, baadhi ya vituo vimekuwa changamoto kufikika kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara, akitolea mfano wa hospitali ya Kivule iliyopo Wilayani Ilala na Mavulunza iliyopo Kimara, Ubungo.