Unicef yataka hatua kuwasaidia watoto wenye magonjwa sugu
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Unicef magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) yanaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya vijana duniani, takwimu za mwaka 2019 zinaonyesha takribani asilimia 20 ya vifo vya vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 19 vilisababishwa na magonjwa hayo.
Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (Unicef) limeitaka Serikali za Afrika pamoja na wadau wa afya, kuunganisha huduma za afya ya mama na mtoto, vijana na huduma za magonjwa yasiyoambukiza (NCDs).
Limesema mifumo ya huduma iliyogawanyika inaendelea kuwanyima watoto wanaoishi na magonjwa sugu fursa ya kupata uchunguzi wa mapema, matibabu stahiki na ufuatiliaji endelevu unaohitajika ili kuishi maisha yenye afya na tija.
Wito huo umetolewa leo Jumatano, Juni 24, 2026 ikiwa ni siku ya pili ya Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa PEN-Plus unaoendelea jijini Dar es Salaam, ambapo wataalamu wa afya, watunga sera, mashirika ya maendeleo na wawakilishi wa wagonjwa wanajadili namna ya kuboresha huduma za magonjwa sugu yasiyoambukiza katika ngazi za wilaya na mikoa.
Kumbuka PEN-Plus ni mpango wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaolenga kusogeza huduma za matibabu ya magonjwa sugu yasiyoambukiza kama kisukari aina ya kwanza, selimundu na magonjwa ya moyo karibu na wananchi kupitia hospitali za wilaya na mikoa.
Akizungumza katika kikao kilichojadili magonjwa yasiyoambukiza yanayoanza utotoni, Mwakilishi wa Unicef, Raul Bermejo amesema magonjwa yanayoonekana kuwa ya watu wazima huanza tangu utotoni, hivyo mifumo ya afya inapaswa kubadilika ili kuwahudumia watoto hao mapema.
Amesema watoto wanaoishi na magonjwa kama selimundu, kisukari aina ya kwanza, magonjwa ya moyo na saratani za utotoni huhitaji matibabu na uangalizi wa muda mrefu, lakini mara nyingi hukumbana na mifumo ya afya iliyogawanyika, ambapo huduma za afya ya mtoto na huduma za magonjwa yasiyoambukiza huendeshwa kama programu tofauti.
“Watoto hawa wanahitaji huduma endelevu katika maisha yao yote, tnaposhindwa kuunganisha huduma, tunasababisha ucheleweshaji wa uchunguzi, rufaa zisizo na ufanisi na kukatizwa kwa matibabu, hali inayoongeza madhara kwa afya zao,” amesema Bermejo.
Amesema huduma za afya za msingi zina nafasi kubwa ya kuunganisha kinga, uchunguzi wa mapema, matibabu, ufuatiliaji na msaada wa kijamii kwa wagonjwa wenye magonjwa sugu.
Kwa upande wake, Arafa Salim Said, mwanaharakati anayepambana na ugonjwa wa selimundu, amesema uzoefu wake wa kuishi na ugonjwa huo umeonyesha umuhimu wa utambuzi wa mapema na huduma bora za afya kwa watoto wenye magonjwa sugu.
Arafa amesema watoto wengi bado wanakabiliwa na changamoto za kuchelewa kugundulika na magonjwa sugu, kukosa mwendelezo wa matibabu na mifumo ya huduma isiyounganishwa, jambo linalowafanya baadhi yao kukosa fursa ya kuishi maisha yenye ubora.
“Watoto wanaoishi na magonjwa sugu wanahitaji mifumo ya afya inayowaona, inayowasikiliza na inayokua pamoja nao, sauti za wagonjwa zinapaswa kusikilizwa wakati wa kupanga sera na huduma za afya,” amesema.
Akieleza changamoto zinazowakumba watoto, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Homoni na Kisukari kwa Watoto Edna Majaliwa, amesema changamoto inayochangia watoto kufika hospitalini wakiwa na madhara makubwa ya ugonjwa ni uelewa mdogo wa baadhi ya wahudumu wa afya kuhusu magonjwa sugu yanayoanza utotoni.
Amesema kwa muda mrefu mifumo mingi ya afya imejikita zaidi kutibu magonjwa ya muda mfupi kuliko kusimamia magonjwa yanayohitaji uangalizi wa maisha yote.
"Hali hiyo husababisha baadhi ya watoto kuchelewa kugunduliwa au kupewa rufaa kwa wakati," amesema.
Dk Majaliwa amesema bado kuna changamoto za upatikanaji wa vifaa vya uchunguzi, dawa muhimu na mfumo rasmi wa kuwahamisha wagonjwa kutoka huduma za watoto kwenda huduma za watu wazima wanapofikisha umri husika.
Kwa upande wa Serikali, Mkurugenzi wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto wa Wizara ya Afya, Dk Felix Bundala amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kutumia huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kufanikisha mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kutokana na idadi kubwa ya wananchi wanaofikiwa na huduma hizo kila mwaka.
Amesema mamilioni ya wanawake huhudhuria kliniki za wajawazito, huduma za kujifungua na kliniki za watoto, jambo linalotoa fursa ya kufanya uchunguzi wa mapema wa magonjwa kama shinikizo la damu, kisukari na saratani ya mlango wa kizazi.
Dk Felix amesema Serikali tayari imeanza kuingiza huduma za uchunguzi wa magonjwa hayo katika programu za afya ya mama na mtoto pamoja na uchunguzi wa watoto wachanga kwa magonjwa mbalimbali ikiwemo selimundu.
“Tunapozungumzia ujumuishaji wa huduma, tunapaswa kuwaweka wagonjwa katikati ya mfumo wa afya. Tukifanya hivyo tutakuwa tumejenga mfumo wenye uwezo wa kutoa huduma bora, endelevu na zinazomfikia kila anayezihitaji,” amesema.