Unyanyasaji kingono wapaa kwa asilimia 80

Dar es Salaam. Wakati Mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ukilenga kupunguza matukio hayo (ya kingono) kutoka asilimia 17.2 hadi asilimia 8 ifikapo Juni 2022, imebainika katika kipindi cha miaka mitano matukio hayo yameongezeka kwa asilimia 80, huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiwa kinara.

Hayo yamebainika kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22 ya ufanisi katika usimamizi wa hatua za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini, ambayo ilikuwa sehemu ya ripoti ambazo ziliwasilishwa bungeni Jumatano.

Ripoti hiyo inaonyesha katika mikoa sita iliyotembelewa kwa ajili ya ukaguzi mwaka 2022, Dar es Salaam yameripotiwa matukio 1,656 kutoka matukio 326 ya mwaka 2018.

Hilo ni ongezeko la asilimia 407, ikifuatiwa na Arusha yenye matukio 1,457 kutoka 625 ya mwaka 2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 133.

Mkoa wa Tabora ambao mwaka 2018 uliripoti matukio ya ukatili wa kingono 22 umeingia kwenye orodha ya mikoa yenye matukio mengi ambapo mwaka 2022 yalirekodiwa 250, sawa na ongezeko la asilimia 1,036.

Matukio hayo yameonekana pia kujitokeza kwa wingi mkoani Mara, ambapo jumla ya matukio 462 yalirekodiwa Juni 2022 ikilinganishwa na 97 yaliyorekodiwa mwaka 2018, ikiwa ni ongezeko la asilimia 376.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa), Dk Rose Reuben alisema jamii, Serikali na wanaharakati kwa pamoja wanapaswa kujiuliza kwa nini lengo limeshindwa kufikiwa, badala yake vitendo hivyo vimeongezeka.

“Tukae chini tujiulize, kwa nini hatujafikia lengo. Inakuwaje badala ya kupunguza vitendo hivi vya ukatili vinaongezeka, vyombo vya dola na mahakama vinafanya nini katika hili?

“Serikali nayo inapaswa kuongeza kasi kushughulikia matukio yaliyopo kwanza kwa kuzuia na kuchukua hatua kwa yaliyokwisha tokea. Kuachiwa asasi za kiraia pekee hatuwezi, lazima tuunganishe nguvu,” alisema.

Alisema Serikali kupitia idara za ustawi wa jamii zilizopo kwenye halmashauri, inapaswa kuhakikisha inashuka zaidi kwenye jamii ambako matukio haya yanatokea.

Dk Rose alieleza kwa upande wa wadau wanaopigia kelele ukatili wa kijinsia wataendelea kutimiza wajibu wao wa kukemea vitendo hivyo na kuhamasisha jamii kupaza sauti yanapotokea matukio ya aina hiyo ili hatua zichukuliwe.

Mikoa mingine

Kulingana na ripoti hiyo, ongezeko dogo la matukio ya ukatili wa kingono limerekodiwa pia mkoani Iringa, ambapo takwimu zinaonyesha kwa mwaka 2022 kulikuwa na matukio 291 kutoka matukio 274 ya mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 6.

Ripoti hiyo imeweka wazi kuwa kuongezeka kwa matukio hayo ni matokeo ya juhudi zisizotosheleza za Serikali katika utambuzi wa hatua za kutosha, uhamasishaji wa rasilimali na utekelezaji duni wa shughuli za kupunguza ukatili wa kijinsia katika maeneo mbalimbali.

Ni mkoa wa Ruvuma pekee ambao umeonekana kupunguza matukio hayo kwa asilimia 7 kutoka 23 ya mwaka 2018 hadi 21 mwaka 2022.

“Hata hivyo, katika mkoa wa Ruvuma data iliyokusanywa inaonyesha kupungua kwa kesi za unyanyasaji wa kijinsia. “Ni muhimu kutambua katika mkoa huu mratibu wa mpango huu hakuwa na takwimu za ukatili wa kijinsia. Kwa hali hii, mkoa unategemea taarifa kutoka kwa polisi dawati la jinsia,” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo.

Mbali na hilo, ripoti hiyo imebaini mpango wa kupambana na ukatili kijinsia umeshindwa kufikia lengo la kupunguza ukatili wa kimwili kwa wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 kutoka asilimia 39 hadi asilimia 10 ifikapo Juni 2022.

Badala ya kupungua, matukio hayo yameongezeka kwa asilimia 50 katika kipindi cha miaka mitano kutoka mwaka 2018 hadi mwaka 2022.

Katika ripoti hiyo matukio ya ukatili wa kimwili yaliyoripotiwa ni 45,580 mwaka 2018, 2019 (48,372), 2020 (58,182), 2021 (69,572) na mwaka 2023 matukio 68,306.

Mkoa wa Mara umekuwa kinara katika eneo hilo ukirekodi matukio 874 kwa mwaka 2022 kutoka 79 ya mwaka 2018, ikiwa ni ongezeko la asilimia 1,006, ukifuatiwa na Tabora yenye matukio 884 kutoka 90 ya mwaka 2018 sawa na ongezeko la asilimia 882.

Arusha imeendelea kuongeza matukio hayo ya ukatili wa kimwili kutoka 1,147 ya mwaka 2018 hadi matukio 3,259 mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 184.

Licha ya kupunguza matukio haya kwa asilimia 2.2, Dar imeendelea kurekodi matukio mengi ya ukatili wa aina hii ambapo takwimu inaonyesha kwa mwaka 2022 yalirekodiwa matukio 5,273 kutoka 5,396 ya mwaka 2018.

Kufuatia hilo, Ofisi ya CAG imeitaka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kuwa na usimamizi wa kutosha wa hatua inazoziweka katika utekelezaji wa mikakati na mipango kazi ya kuondoa ukatili dhidi ya wanawake na watoto.