Zaidi ya watoto 200,000 huajiriwa majumbani – 1

Muktasari:

Asilimia kubwa ya watoto 300,000 wanaoshindwa kuendelea na masomo ya sekondari au ufundi kila mwaka wanaishia kufanya kazi za nyumbani ambako hukutana na matukio ya ukatili wa kingono, kimwili na kudhulumiwa haki yao, uchunguzi wa gazeti hili umebaini.

  

Dar es Salaam. Asilimia kubwa ya watoto 300,000 wanaoshindwa kuendelea na masomo ya sekondari au ufundi kila mwaka wanaishia kufanya kazi za nyumbani ambako hukutana na matukio ya ukatili wa kingono, kimwili na kudhulumiwa haki yao, uchunguzi wa gazeti hili umebaini.

Uchunguzi wetu umebaini idadi kubwa ya wasichana wanaopata mimba wakiwa shule za msingi na sekondari pamoja na wale wanaoacha masomo hayo kwa sababu nyingine mbalimbali, wamekuwa wakiingia katika ajira hiyo.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 2020 unaonyesha asilimia 65 ya wafanyakazi wa nyumbani waliwahi kuripoti kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji.

Hata hivyo, Chama cha Wafanyakazi wa Hoteli, Migahawa na Majumbani (Chodawu) kimeiambia Mwananchi kuwa asilimia 70 ya malalamiko yaliyofikishwa katika chama hicho yalihusu kutolipwa mishahara na kukopwa, huku kukiwa na usiri mkubwa miongoni mwa wafanyakazi hao kuhusu vitendo vya unyanyasaji kingono.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini wafanyakazi hao, ambao asilimia kubwa ni watoto chini ya umri wa miaka 18, wamekuwa wakitumikishwa katika kazi hizo, huku baadhi yao wakitendewa vitendo hivyo na waajiri wao, watoto wa waajiri au ndugu wengine wa familia husika.

Vitendo hivyo ni unyanyasaji wa kingono kwa waajiri wa kiume, kupigwa na waajiri wanawake, malipo duni na malimbikizo ya mishahara, unyanyasaji wa maneno, kuzuiwa kutoka na ukosefu wa uhuru wa kujadili, kupumzika au kuwasiliana.

Masaibu yote hayo huikumba sehemu kubwa ya wahitimu takriban 300,000 wanaokosa fursa ya kuendelea na masomo, kwa mujibu wa Godfrey Boniventura, Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa HakiElimu.

Boniventura anasema mimba shuleni bado ni changamoto na kwa miaka kadhaa nyuma wasichana walipokuwa wakijifungua waliacha watoto nyumbani na kwenda kutafuta kazi za ndani mijini.

“Mimba zimeendelea kuwa changamoto, kumekuwa na ongezeko la asilimia 90 kutoka mwaka 2015 hadi 2020 (kutoka 3,439 hadi 6,533). Jumla ya wasichana 27,091 waliacha shule, takwimu ambazo hazikuhusisha mwaka 2018; msingi walikuwa 4,002 na sekondari 23,015,”
alisema Boniventure.

Uchunguzi uliofanywa wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma na Manispaa ya Iringa umebaini kinachowasukuma wasichana kutafuta kazi za ndani ni umasikini wa kipato cha familia.

Kazi za ndani hutoa fursa kwa vijana walio na elimu ndogo kuingia katika ajira ya kulipwa si tu ili kukidhi mahitaji yao ya kimsingi, bali pia kutoa msaada wa kifedha kwa familia zao.

Ilibainika kuwa watoto ambao hutafuta kazi hizo mara nyingi ni wasichana wadogo ambao hushindwa kukabili shinikizo la wazazi wao na kuanza kazi badala ya kuendelea na masomo.

Wadau mbalimbali, ikiwemo wazazi wamependekeza viongozi wa Serikali na Jeshi la Polisi kuchukulia kwa makini kundi hilo kwa kuunda chombo kitakachosimamia sheria na masilahi yao.

Umasikini

Umasikini unatajwa kuwa chanzo cha wazazi wengi kuwaruhusu watoto wao kufanya kazi za ndani wakiwa na umri mdogo hata kama wapo katika umri wa masomo.

Peres Batoni ni miongoni mwa wasichana wadogo waliomaliza elimu ya msingi mwaka 2021 na kutafutiwa kazi za ndani jijini Dar es Salaam baada ya wazazi wake kushindwa kumpeleka shule zaidi.

“Mpaka sasa nimefanya kazi maeneo matatu tofauti, nilichukuliwa na mtu ambaye nikipata changamoto yoyote namtumia ananitafutia kazi sehemu nyingine,” alisema Peres (16) ambaye pia alikiri kuwahi kupigwa na mwajiri wake.

“Sehemu ya kwanza nilifanya kazi miezi minne bila kulipwa, nikahamishwa na ile hela sikuipata zaidi ya Sh50,000 nilizopewa kama mshahara wa mwezi mmoja,” alisema.

Familia ya Sanga inayopatikana katika Kijiji cha Semtema, Kata ya Kihesa mkoani Iringa imepitia changamoto kadhaa za kimaisha, hali iliyosababisha watoto wa kike wawili kushindwa kumaliza elimu ya msingi na kwenda kufanya kazi za ndani.

Wingi wa majukumu uliomzidi mama wa familia, Schola Mgombelwa (37), ulimlazimu kutoa ruhusa kwa watoto wake, Nesia (15) na Anna Sanga (13) ili waweze kupata chakula chao cha kila siku na mahitaji mengine madogo madogo.

Anasema watoto wake hawajapata changamoto yoyote wakifanya kazi hizo, ila kwa upande wake alikutana na changamoto kadhaa zilizompa wakati mgumu.

“Wazazi wangu walifariki nikiwa mdogo sana, nilitafutiwa kazi za ndani,” alisema Schola ambaye alianza kufanya kazi akiwa na umri wa miaka 14.

Alianzia Chunya mkoani Mbeya mwaka 1997 kwa mshahara wa Sh2,500 na hali ilikuwa ngumu kwake, kwani alipitia manyanyaso mengi pamoja na kupata kipigo kilichomwachia majeraha ya kudumu katika mguu wake wa kushoto.

“Nilijifunza kwamba waajiri wametofautiana na kila nyumba ina changamoto zake,” alisema.

Anasema alikwenda kufanya kazi jijini Dar es Salaam katika familia nyingine ambayo baba hakuwa na tatizo, lakini mama alikuwa mkali na alimnyima chakula akitaka ale kilichobaki na hakutaka washiriki nao meza moja.

Unyanyasaji kingono

Suzy Mgaya ni miongoni mwa wasichana wa kazi za ndani ambao walipitia changamoto nyingi za unyanyasaji wa kingono.

“Nilifanya kazi mtaa wa Kijiweni, mtoto wa mwajiri wangu alianza kunitaka kimapenzi, lakini kila nikimwambia mama yake hachukulii kwa uzito, hivyo nikaamua kuacha kazi.”

Alisema baada ya kukaa kwa muda mfupi kijijini aliona maisha magumu, hivyo aliamua kutafuta tena kazi ambayo aliipata kwa watu wenye asili ya Kihindi ambako kulikuwa na balaa zaidi.

“Kule niliona kazi ni nyingi, sikuwa napumzika na sikupata muda wa kula na hata nilipoumwa sikuweza kutibiwa. Nilipoona hali inazidi kuwa mbaya ilibidi niondoke, kwa kipindi cha miaka miwili sasa ninafanya kazi katika kituo cha redio Iringa mjini ‘Shamba FM’ kama mfanya usafi na mpishi,” alisema Suzy.


Itaendelea kesho