Makosa ya mahakimu yageuka neema kwa wabakaji

Muktasari:

  • Makosa ya kiufundi yanayofanywa na mahakimu, waendesha mashtaka na wapelelezi yamegeuka neema kwa watu wengi waliotuhumiwa hata kufungwa kwa kubaka au kulawiti, kwani huwasaidia kushinda pindi wakatapo rufaa, uchunguzi wa Mwananchi umebaini.

Dar es Salaam. Makosa ya kiufundi yanayofanywa na mahakimu, waendesha mashtaka na wapelelezi yamegeuka neema kwa watu wengi waliotuhumiwa hata kufungwa kwa kubaka au kulawiti, kwani huwasaidia kushinda pindi wakatapo rufaa, uchunguzi wa Mwananchi umebaini.

Wafungwa wengi wamechoropoka kirahisi kutoka kwenye mkono wa sheria kwa sababu tu mahakimu waliosikiliza kesi dhidi yao walikiuka utaratibu ulioainishwa kisheria wa namna ya kuchukua ushahidi wa mwathirika.

Zipo kesi ambazo zilikuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha ubakaji au ulawiti, lakini Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani imejikuta ikilazimika kuwaachia huru warufani kwa sababu tu hati za mashitaka zilikosewa na waandaaji kwa kushindwa hata kunukuu vifungu vya sheria vinavyounda kosa linalojadiliwa.

Haya yanatokea huku uchunguzi wa gazeti hili ukionyesha mahakama nchini zinakabiliwa na ongezeko kubwa la kesi za ubakaji, ulawiti na udhalilishaji mwingine wa kingono kwa watoto wenye umri kati ya mwaka mmoja na miaka 15.

Kwa mfano, waomba rufaa 20 kati ya 37 waliokuwa wakikabiliwa na kesi za ubakaji, ulawiti au udhalilishaji wa kingono waliachiwa huru na Mahakama ya Rufani mwaka 2021 baada ya kubaini makosa ya namna hiyo.

Kutozingatiwa kwa kifungu cha 127(2) cha Sheria ya Ushahidi na uandaaji mbovu wa hati za mashtaka ndio umekuwa uchochoro mkubwa wa waliofungwa kwa kosa la kubaka au kulawiti kujipatia kirahisi uhuru waliopaswa kuupoteza kwa makosa waliyoyatenda.

Kifungu hicho kinatamka kuwa mtoto mdogo anaweza kutoa ushahidi pale mahakama itakapojiridhisha kuwa anaelewa maana ya kiapo, na kama haelewi jambo hilo, inaweza kufanya hivyo kama ana maarifa ya kutosha kuelewa umuhimu wa kusema ukweli.

Kwa sheria hiyo, lazima maoni ya mahakama kuhusu uwezo wa mtoto kutoa ushahidi yaandikwe katika kumbukumbu ya shauri lenyewe.

Maoni hayo lazima yatokane na mahojiano kati ya hakimu na shahidi mtoto anapotaka kujua iwapo shahidi huyo anaelewa maana ya kiapo au ana maarifa ya kutambua umuhimu wa kusema ukweli.

Kifungu hicho kinalazimisha kuwa mahojiano hayo lazima yafuatwe na kurekodiwa waziwazi katika mwenendo wa shauri husika ili kulinda haki ya kila upande.

Pamoja na umuhimu huu ulioainishwa kisheria, mahakimu wengi wamejikwaa katika kukitekeleza kifungu hiki, ama kwa kutokizingatia kabisa, kwa kutorekodi mahojiano na mtoto au kuuliza maswali yanayoshindwa kuthibitisha uelewa wa mtoto kuhusu wajibu wa kusema ukweli kama sheria inavyoelekeza.

Mahakama ya Rufani ambayo imejibainisha kwa kutovumilia makosa ya kiufundi huishia kuuondoa ushahidi wote wa mtoto ikiwa mahojiano baina ya hakimu na shahidi mtoto yalifanywa bila kuzingatia matakwa ya kifungu hicho.


Mifano halisi

Mfano wa jinsi makosa ya mahakimu au waendesha mashtaka yanavyowanufaisha wafungwa wa ubakaji na ulawiti ni uamuzi wa rufaa iliyokatwa na Denis Joram Masenga, akipinga kutiwa hatiani kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumlawiti mvulana wa miaka 10 eneo la Buguruni Mivinjeni jijini Dar es Salaam, Machi 2017.

Mama wa mwathirika aligundua mwanaye alikuwa akipata taabu kukaa na alikuwa akitumia muda mrefu kila mara aingiapo chooni. Vilevile, alikuwa akichelewa kurudi nyumbani kutoka shule hivyo akalazimika kumdadisi.

Baada ya kumbana, mtoto huyo alimtaja Masenga kuwa alikuwa akimshika atokapo shule na kumpeleka kwenye kibanda ambako alimpaka mafuta sehemu za siri na kumlawiti zaidi ya mara 10, huku akimtishia kwa kisu endapo angepiga kelele au kusema kwa watu.

Uchunguzi wa daktari ulithibitisha kuwa kijana huyo alikuwa na michubuko na maambukizi ya bakteria sehemu ya haja kubwa na kwamba tayari alikuwa ameambukizwa Virusi vya Ukimwi (VVU) na magonjwa mengine ya ngono.

Rufaa ya kwanza ya Masenga kupinga kifungo ilikataliwa na Mahakama Kuu, lakini alipokwenda Mahakama ya Rufani aliachiwa huru baada ya mahakama hiyo ya juu kabisa nchini kukubaliana naye kuwa Kifungu cha 127(2) cha Sheria ya Ushahidi hakikuzingatiwa aliposhtakiwa kwa mara ya kwanza.

Kwa kosa hilo, Stella Mugasha, Mwanaisha Kwariko na Panterine Kente ambao ni majaji wa Mahakama ya Rufaa walikubaliana na hoja yake kuwa ushahidi wa mtoto huyo ulipoteza uzito wa kisheria na kuuondoa kwenye ushahidi utakaotumika kuthibitisha kosa, hivyo kumwachia huru.

Katika kesi nyingine, Furaha Shabani Chuga, aliyeshitakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa kosa la kumlawiti msichana wa miaka minane na kufungwa maisha aliachiwa huru na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada ya kuridhika kuwa hakimu aliyesikiliza kesi hiyo hakuzingatia kifugu cha 127(2) cha Sheria ya Ushahidi.

Mwathirika alikuwa akiishi eneo la Kiwalani na bibi yake kabla ya kuhamia kwa shangazi yake alikobakwa na mrufani ambaye alikuwa akiishi eneo hilo. Ilidaiwa kuwa siku ya tukio mrufani alimtuma binti huyo akamnunulie sigara na aliporudi alimpeleka kwenye bonde lililo jirani na alipoishi na kumlawiti.

Mama wa mwathirika ndiye aliyegundua tatizo baada ya kumwona mtoto wake akitembea kwa shida na baadaye kugundua kinyesi kilikuwa kikitoka sehemu ya haja kubwa bila hiari ya binti yake.

Baada ya kumhoji, mwanaye huyo alimtaja Chuga kuwa ndiye aliyemfanyia kitendo hicho mara kadhaa na kumpa Sh1,000.

Ushahidi wa daktari ulithibitisha mtoto huyo aliingiliwa kinyume na maumbile na ulipokewa mahakamani kama kielelezo cha ushahidi hatimaye Chuga kufungwa maisha.

Wakati wa usikilizaji wa rufaa yake, wakili wa Serikali alikiri kuwa mahakama iliyosikiliza kesi dhidi ya Chunga mwanzo ilichukua ushahidi wa mwathirika bila kuzingatia Kifungu cha 127(2) cha Sheria ya Ushahidi hivyo Jaji wa Mahakama ya Kuu, Immaculata Banzi alimwachia mrufani huru baada ya kuridhika kuwa ushahidi wa mwathirika ulichukuliwa bila kukizingatia kifungu hicho.


Kesi za ubakaji, ulawiti zafurika

Uchunguzi umebaini kuwa kati ya rufaa 67 zilizosikilizwa na kuamuliwa na Mahakama ya Rufani, Dar es Salaam mwaka 2022 na kuwekwa kwenye tovuti ya Tanzlii, 29 zilikuwa za ubakaji na ulawiti, udhalilishaji wa kingono na chache zilihusisha watoto kubakwa na wazazi wao.

Idadi hii ni sawa na asilimia 43 ya mashauri ya rufaa za jinai zilizosikilizwa na mahakama hiyo na ni asilimia 7.4 ya jumla ya rufaa 390 zilizosikilizwa na mahakama hiyo mwaka 2022.

Kwa upande mwingine, mwaka 2018 mahakama hiyo ilisikiliza rufaa mbili tu za ubakaji kati ya 15 za makosa tofauti ya jinai ilizosikiliza. Jumla ya rufaa 78 zilisikilizwa mwaka huo.

Mwaka 2017, mahakama hiyo ilisikiliza rufaa moja tu iliyohusu ubakaji kati ya jumla ya rufaa sita za uhalifu wa aina hiyo.

Ongezeko la kesi za ubakaji mahakamani linaelezwa kuwa baya zaidi katika mahakama za mwanzo, hakimu mkazi na zile za wilaya ambazo kesi hizo husikilizwa kwanza kabla ya upande unaoshindwa kukata rufaa.

“Hicho unachokiona ni tone tu la maji katika bahari. Nenda mahakama za mwanzo au za hakimu mkazi, huko kesi nyingi ni za kubaka. Huko (Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani) ni chache sana. Asilimia 70 ya kesi zipo mahakama za chini,” anasema Dk Rugemeleza Nshalla, mwanasheria mkongwe nchini.

Ingawa kwa kiasi fulani kusikilizwa kwa kesi hizo kunachangiwa na kuongezeka kwa majaji, mahakimu na kasi ya usikilizaji kesi, anasema “haiweza kuondoa ukweli kuwa kesi za aina hiyo zinazofikishwa mahakamani zimeongezeka sana.”

Hali hiyo pia imeongeza mzigo wa kiutendanji kwa mahakama ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikikabiliwa na upungufu wa majaji na mahakimu uliosababisha mrundikano wa kesi.

Pia, inaaminika kushusha hadhi na heshima ya vyombo vya kusimamia na kutafsiri sheria na mfumo mzima wa haki jinai nchini.


Mazingira ya kubakwa

Uchunguzi unaonyesha kuwa wengi wa watoto wanaobakwa ni wale wenye umri wa kati ya mwaka mmoja hadi miaka 15.

Mwananchi limepitia kesi hizo na kugundua kuwa watoto wengi wamekuwa wakipatwa na madhila hayo katika mazingira ya kutokuwa karibu na wazazi au walezi wao hivyo kuwapa mwanya wabakaji kutekeleza unyama wao.

Kumekuwapo pia na matukio ya watoto kubakwa na ndugu wa karibu ambao wazazi wa watoto waliwaamini na kuwapa wawalinde.

Wengine walibakwa wakielekea au kutoka shuleni, wanapokwenda au wanaporudi kuchota maji na wengine wakibakwa na walimu, walinzi wa nyumbani au wahudumu katika magari ya shule.

Mapitio ya kesi hizo yanaonyesha mazingira ya nyumba ya kupanga inayohusisha wapangaji wengi kwamba ni hatari kwa watoto, kwani wapo wanaobakwa na wapangaji.

Kesi ya Adam Shango inatoa mfano mzuri wa hatari ya kuwaacha watoto bila usimamizi wa wazazi au walezi.

Shango alifungwa maisha baada ya kudaiwa kumwingilia kinyume na maumbile mtoto wa kiume wa mwaka mmoja na nusu huko Mkundi Bwawani, katika Manispaa ya Morogoro.

Kabla ya tukio hilo, mama wa mtoto huyo alimwacha mwanaye kwenye mikono ya mjomba wake (kaka wa mama huyo) na kwenda kununua mahitaji ya nyumbani.

Aliporudi alimkuta mwanaye akilia sana na baada ya kumkagua alikuta akitokwa damu nyingi sehemu za siri huku sehemu ya haja kubwa ikiwa imeharibika.

Katika kesi nyingine, mtoto wa kike wa miaka minne alibakwa na mkazi wa Kijiji cha Kisiju wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, Shomari Mkwama baada ya bibi yake aliyekuwa akiishi naye kumwacha nyumbani. Mkwama anatumikia kifungo cha maisha kwa kosa alilolitenda kwa mtoto huyo asiye na hatia.


Takwimu za makosa

Takwimu zinaonyesha watuhumiwa 18 kati ya 68 waliokata rufaa kupinga vifungo vya maisha au miaka 30 kwa kosa la kubaka au kulawiti waliachiwa huru kwa waandaaji kukiuka Kifungu cha 127(2) cha Sheria ya Ushahidi.

Kutokana na ukweli kwamba kubakwa na kulawitiwa ni uhalifu ambao huvuruga kabisa maisha wa waathirika kisaikolojia na kimwili na kuigusa jamii nzima kwa ujumla pamoja na kuacha makovu yasiyotibika kirahisi, wadau wa haki jinai wametaka ufanyike utafiti wa kina kuhusu mienendo ya kesi za aina hiyo nchini na kuja na mapendekezo ya kuhakikisha haki inatendeka bila mizengwe.

Takwimu nyingine zinaonyesha mwaka 2022 Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam ilipokea na kusikiliza mashauri ya rufaa za jinai 68 zilizohusisha makosa ya ubakaji, ulawiti na unyanyasaji wa kingono kati ya rufaa za jinai 227 ilizopokea na kuziamua.

Warufani zaidi ya 30 kati ya 68 wa rufaa zilizohusisha makosa ya kubaka na ulawiti waliachiwa huru kutokana na makosa ya kiufundi yaliyofanywa na mahakama za chini au waendesha mashtaka.

Mwaka 2021 mahakama hiyo iliamua kesi 24 za ulawiti na ubakaji kati ya rufaa za makosa mbalimbali ya jinai 160 ilizozipokea na mwaka 2017 ilipokea kesi nne tu za jinai na kati ya hizo hapakuwa na kesi iliyohusisha ubakaji na ulawiti.

Miaka mitano nyuma (2018), Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam iliamua rufaa 42 za ubakaji na ulawiti kati ya rufaa za makosa ya jinai 165 ilizopokea.

Rufaa nyingine zilihusisha makosa ya ujambazi wa kutumia silaha, wizi, uvunjaji nyumba na shambulizi la kudhuru mwili.

Mwaka 2021, Mahakama ya Rufani kanda ya Arusha ilipokea na kusikiliza rufaa 34 za makosa mbalimbali ya jinai na 11 kati ya hizo zilihusisha makosa ya ulawiti na ubakaji. Mwaka uliofuata (2022) rufaa tisa kati ya 33 za jinai ilizozisikiliza zilihusisha ulawiti na ubakaji.

Mwaka 2022, Mahakama ya Rufani Dar es Salaam iliamua kesi 37 za ubakaji, ulawiti na makosa mengine yanayoendana na hayo kati ya rufaa 126 ilizosikiliza.


Mahakama yafafanua

Mahakama imekiri ongezeko la kesi za ubakaji na ulawiti, hali inayoongeza mzigo kwa majaji na mahakimu.

“Hali hii pia inaeleza why (kwa nini) tunahitaji majaji na mahakimu zaidi. Ndio maana kila wakati kuna juhudi za kuongeza majaji na mahakimu,” anasema Katibu wa Msajili Mkuu wa Mahakama Tanzania, Jovine Bashanga.

Akizungumza kwa niaba ya Msajili Mkuu wa Mahakama Tanzania, Wilbert Chuma, Bashanga alitumia muda mwingi kufafanua hali hiyo na kulihusisha ongezeko hilo na mambo kadhaa, yakiwamo mafanikio makubwa iliyopata mahakama katika kusogeza huduma kwa wananchi.

“Huko nyuma kulikuwa na mashauri machache lakini kadiri tunavyosogeza huduma karibu na wananchi ndivyo na mashauri yanaonekana kuongezeka. Pia kuna mwamko wa watu kufungua mashauri kwa sababu uelewa wa wananchi kuhusu haki zao umeongezeka kupitia elimu tunayotoa kupitia vyombo vya habari, kwa hiyo watu wanapata mwamko kuhusu haki zao,” anasema.

Kwa upande mwingine, Bashanga amelihusisha ongezeko hilo na kuimarishwa kwa madawati ya jinsia katika mahakama na vituo vya polisi ambako watu wengi wamekuwa wakiyatumia kutafuta haki zao.

Bashanga anaamini kuna haja ya kufanya utafiti wa kina ili kujiridhisha na ongezeko hilo na sababu zinazochangia.

“Hilo ongezeko ni hypothetical (sio la uhakika) but you can test (lakini unaweza kulipima) kwa kufanya real research (utafiti halisi). Kwa hiyo ili kupata majibu sahihi lazima kulinganisha takwimu zetu na jamii inasemaje,” anasema Bashanga.

Katibu huyo anasema kuna uwezekano kuwa mashauri mengine ya ubakaji na ulawiti hayajafika mahakamani ama waliofungwa hawajakata rufaa na kuongeza kuwa zipo kesi nyingi zinaishia kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP).

“Ukikusanya takwimu zote hizo ndipo unaweza ku-draw conclusion (kuhitimisha) kwamba mashauri yameongezeka na unakuwa na majibu kwa nini yameongezeka,” anasema.

Mahakama pia inaamini kuwa ongezeko la kesi hizo limechangiwa na kuboreshwa kwa miundombinu ya utoaji haki na kuongezeka kwa imani ya wananchi kwa mahakama.


Makosa ya mahakimu

Akizungumzia makosa ya kiufundi yanayofanywa na mahakimu na waendesha mashtaka, ofisa huyo alisema mahakama inalitambua hilo na hivi sasa inafanya jitihada za makusudi ili kupunguza ama kuondoa kabisa makosa yanayojirudia mara kwa mara na watoaji haki hao.

Anasema mahakama imeanzisha utaratibu wa kutoa mafunzo ya mara kwa mara ya elimu endelevu ya sheria kwa mahakimu na majaji.

“Tunaandaa semina kwa njia ya mtandao kuhusu mambo mengi, ukiwamo utaratibu wa kupokea ushahidi wa mtoto baada ya kuibuka changamoto ya wengi kuto-comply (kutofuata) sheria inavyotaka,” anasema.

Uchunguzi wa Mwananchi umeonyesha kuna watu waliofungwa kwa makosa ya ubakaji au ulawiti lakini waliachiwa (hasa na Mahakama ya Rufaa) kutokana na makosa ya kiufundi yanayofanywa na mahakimu, waendesha mashtaka na wapelelezi.

“Lolote linaloibuliwa na Mahakama ya Rufani tunalichukulia kwa umakini na tunahakikisha linazingatiwa na wahusika wote, kwa hiyo kuna jitihada kubwa sana zinafanywa kuhakikisha watu hawakosei. Ndio maana Court of Appeal (Mahakama ya Rufani) iko strict (inasimama imara) na makosa kama haya, nao wakiyafunika ujue itazidi kuwa shida zaidi,” anasema.