Unyanyasaji wa kijinsia wakoleza mjadala miswada ya sheria za uchaguzi

Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango leo Jumanne, Januari 30, 2024, wakati akichangia maoni yake kwenye miswada mitatu ya sheria za uchaguzi bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Hoja kuhusu unyanyasaji wa kijinsia kuwa sehemu ya makosa ya uchaguzi ni moja ya mambo yaliyoibuliwa bungeni leo Januari 30, 2024 katika mjadala wa wabunge kuhusu miswada ya sheria za uchaguzi.

Dar es Salaam. Umuhimu wa kuwepo ulinzi wa kisheria dhidi ya unyanyasaji wa wanawake katika uchaguzi ni miongoni mwa hoja zilizoibuliwa na wabunge wakati wakijadili miswada mitatu ya sheria za uchaguzi.

Hoja hizo zilijikita katika kuonyesha haja ya makosa ya unyanyasaji wa kijinsia kuingizwa kwenye makosa ya uchaguzi.

Wabunge hao wametoa hoja hizo bungeni jijini Dodoma leo Januari 30, 2024 walipokuwa wakijadili kuhusu miswada ya sheria za uchaguzi.

Aliyeanza kujenga hoja hiyo ni mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango-Malecela akisema kumejengeka tabia ya wanawake kunyanyaswa katika majukwaa ya kampeni za uchaguzi.

Mbunge huyo amesema yeye ni miongoni mwa waathirika wa matukio hayo kwa kuwa ameshiriki muda mrefu kuwania ubunge wa jimbo.

“Mimi ni mwathirika, mimi ni mbunge wa jimbo mwanamke, nimeanza kugombea jimbo tangu 2005, nakutana na haya mambo ambayo watu wanayachukua kama madogo hapana. Manyanyaso ni makubwa sana wakati tunagombea,” amesema.

Amesisitiza umuhimu wa jambo hilo kuwekewa mkazo katika sheria hizo ili lisifanyike.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Khadija Taya ‘Keysha’ naye amegusia hoja hiyo akisisitiza umuhimu wa jinsia zote kupewa fursa sawa.

Ameeleza unyanyasaji umekuwepo si kwa wanawake pekee, hata wanaume akitolea mfano, “Kuna wabunge wanaume wanaitwa mashoga.”

Katika hoja yake, nje ya muktadha huo, Khadija ameeleza umuhimu wa sheria hizo za uchaguzi kuweka utaratibu wa kupatikana kwa viongozi wa viti maalumu, kwa kuwa baadhi ya vyama havina utaratibu mzuri.

“Tume ya Uchaguzi ndiyo inapaswa kusimamia mchakato huu kwa kuwa imeelekezwa na Katiba ya Tanzania,” amesema.

Hoja nyingine zilizoibuliwa katika mjadala huo ni pongezi kutokana na mabadiliko yaliyofanyika, yakitajwa kuakisi R4 za Rais Samia Suluhu Hassan.

Pongezi hizo zilitolewa na mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda aliyesema upo umuhimu wa Bunge kupitisha sheria hizo, kwa kuwa zinahusisha mambo muhimu.