Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ngome za vijana zaainisha kasoro ya miswada ya sheria za uchaguzi

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT Wazalendo, Abdul Nondo (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, kulia ni Katibu wa Vijana CUF,Iddi Mkanza na Katibu wa Vijana NCCR Mageuzi, Elisante Ngoma (kushoto).Picha na Sunday George

Muktasari:

  •  Viongozi wa mabaraza na ngome za vijana za vyama vya ACT- Wazalendo, NCCR- Mageuzi na CUF wameichambua na miswada mitatu ya mitatu ya sheria za uchaguzi na vyama vya siasa na kutoa mapendekezo kadhaa ili kuleta usawa katika chaguzi zijazo.

Dar es Salaam. Muungano wa viongozi wa mabaraza na ngome za vijana ya vyama vya ACT- Wazalendo, Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR- Mageuzi, wameanishia hoja 10 zenye kasoro katika miswada ya Sheria za Uchaguzi na vyama vya Siasa iliyowasilishwa bungeni, Novemba 10, 2023 wakisema zinatakiwa kufanyiwa maboresho.

Miongoni mwa kasoro hizo ni wakurugenzi wa majiji na manispaa kuendelea kusimama chaguzi, upatikanaji wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa tume, muundo wa tume ya uchaguzi na sifa za wajumbe, dhamana ya fedha inayowekwa na mgombea kwa msimamizi wa uchaguzi na zuio la mtu asiyeridhika na uamuzi wa tume kutokwenda mahakamani.


Kasoro nyingine ni miswada kutojumuisha hoja za vijana, chaguzi za serikali ya mitaa, vijiji na vitongoji, kifungu kinachozuia wafungwa kupiga kura, fedha za shughuli za Tume kutoka bajeti ya Serikali, Tume kulipisha wananchi kwa kadi ya kupiga kura zilizopotea au kuharibika na Msajili wa Vyama vya Siasa kupewa madaraka makubwa.

Miswada iliyopelekwa bungeni ni wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023.

Viongozi hao wa mabaraza na ngome za vijana kutoka vyama hivyo vitatu wanaungana  baadhi ya wadau wa siasa waliotoa maoni ya mwaka 2023 wakisema miswada hiyo haijakata kiu ya Watanzania kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na mazingira sawa ya uchaguzi.

Wakitoa tamko la pamoja leo, Jumanne Januari 2,2023 makao makuu ya ACT-Wazalendo jijini Dar es Salaam, viongozi hao wa mabaraza na ngome za vijana wamesema wanaipinga miswada hiyo kwa sababu ina upungufu na haijabeba hoja za ustawi wa vijana na vifungu vingi vinakinzana na Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.

Katibu wa Vijana wa CUF, Idd Mkanza amewaambia wanahabari wanapinga wakurugenzi kusimamia  chaguzi kwa sababu baadhi yao ni makada wa CCM na hakutakuwa na usawa kwa wagombea wa vyama vya upinzani kama ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 uliolalamikiwa na vyama mbalimbali.

"Tunapendekeza vifungu 6 (1) na 6 (2) katika muswada wa sheria ya uchaguzi vinavyoruhusu kutumia wakurugenzi wa halmashauri na watumishi wa umma vifutwe ili kutoa fursa kwa Tume ya Taifa Uchaguzi kuajiri watendaji wake kwa sifa zitakazoainishwa.

"Watu waombe kwa sifa, wafanyiwe usaili wa wazi badala ya Tume kutumia wakurugenzi wa halmashauri au manispaa," amesema Mkanza ambaye ni mwenyekiti wa Jukwaa la Vyama vya Siasa chini ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Kuhusu upatikanaji wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mkanza amesema kwa mujibu wa kifungu cha 5(1) cha muswada wa Sheria mpya ya Tume ya uchaguzi viongozi hao bado wanateuliwa na Rais moja kwa moja bila kupitia mchakato wa kuomba na kufanyiwa usaili na kamati ya usaili.

Mkanza anapendekeza viongozi hao wanapaswa kupita kwenye mchakato wa kuomba kufanyiwa usaili na kamati ya usaili kama wajumbe wengine wa Tume.

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT- Wazalendo, Abdul Nondo amesema kifungu cha 10 (1) C cha muswada wa sheria ya uchaguzi kinazuia mtu aliyetiwa hatiani kwa kifungo kinachozidi miezi sita au maisha kupiga kura. Hata hivyo, Nondo amesema kifungu hicho kipo kinyume na ibara ya 5 (1) na 21 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977

"Kifungu hiki kinachozuia wafungwa kupiga kura kinapaswa kufutwa kwa sababu kinakinzana na ibara ya 5 (1) ya Katiba ya Tanzania, pia kinzana na hukumh ya mahakama kuu katika kesi no 3 ya mwaka 2022 iliyofunguliwa na mwanaharakati Tito Magoti.

"Lakini ulimwengu umebadilika sasa nchi nyingi duniani zikiwemo za Denmark, Finland, Ufaransa, Zimbabwe na Japan zinaruhusu wafungwa kupiga kura bila kikwazo," amesema Nondo.

Katibu wa Vijana wa NCCR- Mageuzi, Elisante Ngoma amesema endapo miswada hiyo mitatu itapitishwa kama ilivyo watashirikiana na wadau mbalimbali kwenda mahamani kupinga sheria zote zitakazopitishwa katika vifungu vyote vinavyokinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.