Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UoI yamtunuku Samia

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa ameshika Tuzo ya Mlima Kilimanjaro ambayo Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) kimemtunuku Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) kimemtunuku tuzo ya Mlima Kilimanjaro, Rais Samia Suluhu Hassan kikitambua mchango wake mkubwa katika uongozi, utalii na elimu.

Iringa. Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) kimemtunuku ‘Tuzo ya Mlima Kilimanjaro,’ Rais Samia Suluhu Hassan, kikitambua mchango wake katika elimu, uongozi na utalii.

UoI ilianzisha tuzo hiyo ikiwa ni sehemu ya kutambua watu na taasisi zenye mchango chanya katika kukuza maendeleo ya Taifa, huku wengine waliowahi kuipata ni pamoja na hayati Benjamin Mkapa.

Wengine ni Mkuu wa Majeshi mstaafu ambaye pia ni Mkuu wa UoI, Venance Mabeo, Spika mstaafu, Anna Makinda na Mjumbe wa Halmashauri Kuu (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Richard Kasesela.

Akikabidhi tuzo hiyo ambayo imepokelewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Novemba 30, 2023,  Makamu Mkuu wa UoI, Profesa Ndelilo Urio amesema Rais Samia alipokea nchi katika kipindi kigumu, na wapo ambao hawakuamini kama angeweza.

"Ametengeneza historia ya pekee kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Tanzania, wote wanatambua alipokuwa anachukua madaraka kulikuwa na hali ngumu na wengi hawakutegemea angeweza, amekuwa kiongozi wa mfano na ameifanyia Tanzania mambo mengi,” amesema Profesa Urio katika mahafali ya 26 ya chuo hicho.

Amesema pia wamempatia tuzo hiyo kwa uamuzi wake wa kuongeza wanufaika wa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Tanzania (Heslb).

“Miaka mitano tulikuwa na wanafunzi 376 tu wanao nufaika na mikopo ya elimu ya juu lakini mpaka sasa tunao wanafunzi 2834, hakuna upendeleo kwa vyuo vya Serikali na vyuo vikuu binafsi," amesema.

Kuhusu utalii, Profesa Urio amesema idadi ya wanafunzi wanaosoma fani hiyo  imeongezeka tangu alipoonyesha juhudi zake kupitia filamu ya ‘Royal Tour.’

"Lakini tumeambiwa idadi ya watalii na mapato kwenye sekta ya utalii yameongezeka hivyo hakuna ubishi kwamba ‘Royal Tour’ imehamasisha utalii," amesema Profesa Urio.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshukuru kwa tuzo hiyo na kuwaomba Watanzania waendelee kuutangaza Mlima Kilimanjaro kuwa upo Tanzania.

"Asante kwa tuzo hii ya Mlima Kilimanjaro kwa Rais Samia, nitaifikisha kwa heshima na niwapongeze kwa kuibuni," amesema na kuongeza;

"Kuna wanao sema Mlima Kilimanjaro upo kwao, unaweza kuuona popote lakini ili upande Mlima Kilimanjaro lazima uje Tanzania,”amesema.