Upandikizaji ini kufanyika nchini 2025

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba MNH, ambaye pia ni daktari bingwa wa mfumo wa chakula na ini, Dk John Rwegasha
Muktasari:
- Huduma hiyo inatajwa kuwa mwendelezo wa azma ya Serikali kuhakikisha huduma za ubingwa bobezi zinapatikana nchini.
Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), imepanga kuanzisha huduma ya kupandikiza ini kuanzia 2025.
Huduma hiyo inatajwa kuwa mwendelezo wa azma ya Serikali kuhakikisha huduma za ubingwa bobezi zinapatikana nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi, amebainisha hayo wakati akifungua mafunzo ya awali ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya ini, kuelekea kwenye kongamano la wataalamu wa magonjwa ya ini Barani Afrika (Colda), linalotarajiwa kufanyika September 7-9 Jijini Dar es Salaam.
Amesema mafunzo mbalimbali ya wataalamu yanaendelea kutolewa kupitia kituo cha kutoa mafunzo, uchunguzi na matibabu ya kibobezi ya magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika kilichopo MNH.
Amesema kuwa kongamano la wataalamu wa magonjwa ya ini barani Afrika, ni moja ya maandalizi katika kusaidia huduma za upandikizaji ini kuanza kufanyika nchini.
"Kongamano litatoa fursa ya wataalamu kujifunza, kujadili na kupanga mwendelezo wa mafunzo ya mara kwa mara ya ndani na nje ya nchi ambayo yatawajengea uwezo wataalamu kuanzisha huduma ya upandikizaji ini nchini.
“Hii safari ni ndefu na nzito lakini tunaamini kwa msaada wa Serikali na wadau mbalimbali, tutafanikiwa kwani hadi sasa kituo kina uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa waliofanyiwa huduma hiyo nje ya nchi, pale wanaporejea nyumbani tofauti na awali ambapo walilazimika kurudi nje ya nchi," amesema.
Amebainisha kwamba jambo hilo linaenda sambamba na uboreshaji wa maabara za kiuchunguzi wa patholojia, uchunguzi wa damu, uchunguzi wa radiolojia na tiba radiolojia na uboreshaji wa vyumba vya wagonjwa mahututi.
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba MNH, ambaye pia ni daktari bingwa wa mfumo wa chakula na ini, Dk John Rwegasha, amesema katika kongamano hilo, wataalamu watajifunza namna mbalimbali za kutibu magonjwa ya kuondoa mawe kwenye mfumo wa nyongo na ini bila kuhitaji upasuaji mkubwa.
Kwa upande wake, Dk Wongani Mzumara, ambaye ni mshiriki kutoka Malawi, amesema kongamano hilo ni fursa ya wataalamu wa Kiafrika kujifunza mbinu mpya za kutibu magonjwa ya mfumo wa chakula na ini na kwamba ameona fursa ya ushirikiano kati ya MNH na Malawi katika eneo hilo.
Kongamano hilo linahudhuriwa na wataalamu kutoka nchi za, Malawi, Gambia, Afrika ya Kusini, Nigeria na Tanzania.