Upandikizaji mimba wafichua udhaifu wa wanaume

Dar es Salaam. Idadi ya wanaume wanaokabiliwa na matatizo ya kushindwa kutungisha mimba inaongezeka nchini, huku ikitajwa kuwa wagumu kukubali vipimo, wakihofia aina ya upimaji na wenye mapokeo hasi ya majibu yao ikilinganishwa na wanawake.

Upandikizaji mimba ulivyoibua udhaifu mpya kwa wanaume

Kwa mujibu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), robo tatu ya matatizo ya ugumba kati ya wanawake zaidi ya 1,200 wanaofika kila mwaka kuhitaji usaidizi wa upandikizaji mimba yanawahusu wanaume.

Wengi mbegu zao huwa hafifu, zisizo na mwendo na nguvu ya kuhimili kulifikia yai kwa ajili ya utungishaji mimba, hali inayochangiwa na ulaji usiofaa, aina ya kazi wanazofanya, magonjwa ya zinaa katika via vya uzazi na mabadiliko ya homoni.

Hayo yamebainika wakati Muhimbili ikiwa katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuanza upandikizaji mimba kupitia maabara Novemba mwaka huu, baada ya mchakato muhimu kukamilika.

Akizungumza juzi katika mahojiano maalumu kuhusu hali ya magonjwa ya mfumo wa uzazi, Mkuu wa kitengo cha magonjwa ya kike na uzazi, Dk Matilda Ngarina alisema wanaume wengi wanaamini mwanamke ana jukumu la kubeba ujauzito, wakisahau wana wajibu wa kuwapatia mbegu bora.

“Wanaume kwa sasa wana matatizo mengi na magumu kuliko wanawake na kwa kuwa jamii inaamini mwanamke ndiye anayezaa, wanaokuja hospitali ni wanawake na tunaendelea kuwasihi wawalete wanaume, hasa pale unapompima na unamkuta hana shida yoyote.

“Kuna wengine anakwambia hawezi kuja kwa daktari, kwa hiyo unaamua kuanza naye,” alisema Dk Ngarima.

Alisema wanaume wakifika hospitali mara nyingi hukosa ushirikiano, ijapokuwa wachache wanakubali maelekezo na wanasikiliza na kwamba wapo ambao hawafiki kabisa na wanaokwenda wana haraka ya kuondoka.

“Wengi kipimo cha kutoa mbegu hawakipendi, wanaona kama kinawaaibisha, kwamba atoe mbegu akiwa hayupo na mwanamke wanaona ni kigumu na kinawashushia hadhi yao, lakini sisi tupo katika matibabu kwa kuwa kutoa mbegu ni tendo la siku moja, maana inabidi zitolewe kwa kujichua,” alisema.

Dk Ngarina alisema majibu yanapotoka wanawake wapo tayari kuyapokea, lakini ni changamoto kubwa kwa wanaume, wengi wanayakataa na wengine wanapata msongo wa mawazo.

“Hawapo tayari, ukimwambia ana shida huenda ikamfanya asiweze kupata mtoto ni habari mbaya sana kwao, wengi wanaipokea vibaya, wanapata huzuni, msongo wa mawazo, wanafanya maamuzi magumu,” alisema.

Alisisitiza kuwa sayansi ipo na namna ya kusaidia ipo, ni kiasi cha kutulia na huwa wanawashauri nini cha kufanya kwa kuwa hata kama mwanaume ana mbegu moja inaweza kuchukuliwa akapandikizwa mke.

Sababu za ugumba

Kwa mujibu wa Dk Ngarina, changamoto kubwa inayowakumba wanaume ni ulaji usiofaa, hali inayosababisha mbegu zinakosa ubora.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni changamoto ya homoni. “Kuna wanaume wanaota matiti, wengine hawana nguvu za kiume sababu homoni nazo zinasababisha sasa mbegu zinatengenezwa, uume usimame, amwage mbegu ni homoni.

“Kingine ni maambukizi katika via vya uzazi, mara nyingi huharibu mbegu zinakotengenezwa. Kingine ni mishipa ya damu inayosambaa kwenye korodani kuvimba, damu haiendi inavyotakiwa na hii mara nyingi kuna aina ya kazi mwanamume akifanya, mfano gari unaendesha kutoka hapa mpaka Zambia umekaa au anayeendesha daladala kutwa nzima.

“Au kazi yoyote ya kukaa muda mrefu mzunguko wa damu unakuwa siyo kama inavyotakiwa, mishipa ile ya damu inavimba, kwa hiyo haiwezi kutengeneza mbegu kama inavyotakiwa,” alifafanua.

Alisema ijapokuwa wapo wanaozaliwa na tatizo la kijenetiki, huku akihimiza watafiti kulifanyia kazi eneo hilo ili kubaini kiini hasa cha ongezeko la hili tatizo je, ni mabadiliko ya hali ya hewa?

Mambo ya kuzingatia

Lishe bora ndiyo msingi wa mwanamume kuwa na mbegu bora pamoja na mwanamke kuimarisha mfumo wake wa uzazi kwa mujibu wa Dk Ngarina.

“Ili kutokushindwa kupata watoto huko baadaye, tunashauri watu wale chakula bora, hasa kutoka utotoni ambacho kina vitu vyote sita, mboga za majani, wanga, mizizi, protini, siku hizi tunaona wanaume wanakula chipsi yai na soda kuanzia asubuhi mpaka jioni, lazima mwili wako utapata shida, vyakula hivi ni muhimu ili kuboresha ovari na korodani,” alisema.

Alitaja matunda, mboga za majani na maji kuwa huondoa sumu mwilini na ni muhimu asubuhi, mchana na jioni, kwani husafisha sumu mwilini.

Aliwataka watu kuacha kula chakula kilichokobolewa sana na juisi zilizochujwa, kwani takataka zinazoondolewa zina umuhimu mkubwa katika kupambana na afya ya uzazi.

Dk Ngarina alisisitiza watu kuacha ngono zembe. “Ni njia ya rahisi na ya kwanza kusababisha maambukizi kwenye via vya uzazi na mirija kote kwa wanaume na wanawake, hivyo tunashauri waache.”

Alikemea matumizi ya P2 kwa wasichana na wanawake na kuwataka pia wahakikishe wanatumia vema njia za uzazi wa mpango kwa kufuata ushauri ili kutovuruga mfumo wa homoni na kusababisha ugumba baadaye.