Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Upelelezi kesi ya Kambi Zuberi na wenzake wakamilika

Mshtakiwa Kambi Zuberi( kulia) akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi yake na mwenzake kuahirishwa.

Muktasari:

  • Hii ni mara ya pili, washtakiwa hao kufikishwa katika Mahakama ya Kisutu, kwa mara ya kwanza Novemba 21, 2022, ambapo walisomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka manane yakiwemo ya kusafirisha heroini.

Dar es Salaam. Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Toangoma Kigamboni, Kambi Zuberi Seif (40) na wenzake watano, umekamilika.

Wakili wa Serikali, Titus Aron ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Alhamisi Julai 2, 2026, wakati shauri hilo lilipotajwa.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu, kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroni zenye uzito wa kilo 34.89 pamoja na kutakatisha fedha.

Mbali na Zuberi, washtakiwa wengine ni aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya Simba, Muharami Sultani (40), maarufu Shilton; Maulid Mzungu(54), maarufu Mbonde na mkazi wa Kisemvule ambaye ni dalali wa viwanja na muuza nazi.

Pia yupo, Said Matwiko(41) mkazi Magole; John Andrew(40), maarufu Chipanda na mkazi wa Kitunda ambaye kazi yake ilikuwa ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy pamoja na mshtakiwa wa sita ni Sarah Joseph, ambaye ni mke wa Matwiko.

Wakili Titus ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Benda Nyaki.

"Upelelezi wa washtakiwa hawa umekamilika, tunasubiri kusajili nyaraka muhimu Mahakama Kuu ili kesi hii iendelee na hatua nyingine," amedai Titus.

"Kutokana na taarifa hii, tunaomba mahakama yako itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama nyaraka hizo zimeshasajiliwa katika mfumo.”

Hata hivyo, leo mshtakiwa Kambi pekee yake ndio amepelekwa mahakamani huku washtakiwa wengine wakisikiliza kesi yao kwa njia ya video wakiwa mahabusu katika Gereza la Segerea.

Hakimu Nyaki alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hadi Julai 8, 2026 kwa kutajwa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya mwaka 2016 na Novemba 4, 2022 maeneo tofauti ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, ambapo waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini hydrochloride.

Shtaka la pili ni kusafirisha heroini, tukio wanalodaiwa kulitenda Oktoba 27, 2022 katika eneo la Kivule Wilaya ya Ilala washtakiwa kwa pamoja walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 27.10.

Pia Novemba 4, 2023 eneo la Kamegele Wilaya ya Mkuranga, washtakiwa wote walikutwa wakimiliki dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa Kilo 7.79.

Hata hivyo, shtaka la nne, tano, sita, saba na nane ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili mshtakiwa Kambi pekee yake.

Kambi anadaiwa kati ya Aprili 15, 2021 na Aprili 25, 2021 wilayani Ilala, alijipatia magari matano aina ya Tata yenye jina la Safia Group of Companies LTD huku akijua mali hizo zilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.