Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Upendo kichocheo mahusiano mazuri kati ya ‘hausigeli’, watoto

Roseline Atieno.

Muktasari:

  • Mwanasaikolojia amesema hakuna anayezaliwa akiwa na chuki, bali hufundishwa au kuona kupitia wengine.

Dar es Salaam. Upendo na kujali wengine vinatajwa kuwa na mchango wa kuwapo mahusiano mazuri kati ya mtumishi wa kazi za ndani na mwajiri wake.

Inaelezwa kwa kuwa wasaidizi wa kazi nyumbani ndiyo hukaa muda mrefu na watoto wakati wazazi wao wanapokuwa katika shughuli zingine, wanapaswa kuwa na mapenzi na watoto wanaowalea.

Maoni hayo yametolewa kutokana na video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha  Roseline Atieno maarufu 'Rosie' raia wa Kenya, ambaye amekuwa akifanya kazi ya kulea watoto nchini Lebanon kwenye familia   inayotajwa kuwa ya watu maarufu nchini humo.

Katika video hiyo, Rosie alipokuwa akiagwa uwanja wa ndege nchini Lebanon watoto hawakutaka aondoke, hivyo waliangua vilio.

Ramadhani Massenga, ambaye ni mwanasaikolojia alisema kilio cha watoto kwa Rosie kinadhihirisha kuwa chuki watu wanafundishwa.

Amesema hakuna mtu anayezaliwa akiwa mwenye chuki na mtu, bali kwa kufundishwa au kuona kupitia wanaomzunguka.

"Wazazi wanatakiwa kuwalea watoto kwa upendo mkubwa, ambao utaenda kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye kwa kuishi vizuri na familia au jamii nyingine," amesema Massenga.

Amesema kuna baadhi ya wazazi wamekwenda shule na wana kila kitu, lakini wameshindwa kulea watoto wao ambao wanakosa nidhamu.

Massenga amesema watu wanatakiwa kuwa makini wanapochagua au kuletewa wasichana wa kuwasaidia kazi za nyumbani, kwani kwa kiasi kikubwa  husaidia makuzi ya watoto.


Esta Sabato, kutoka Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii, Mkoa wa Katavi anasema jamii inatakiwa kubadilika katika malezi ya watoto kwa kuishi vizuri na wasaidizi wa kazi.

“Waajiri wana nafasi ya kutengeneza mazingira mazuri ya kuishi watoto kutokana na matendo wanayoonyesha kwa mfanyakazi, kama yatakuwa ya amani na upendo,” amesema.

Amesema kwa kukaa vizuri na mtumishi wa ndani, watoto hawataona tofauti kati yao, wazazi au hata mgeni wanayeishi naye.

Khadija Rajab, Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Temeke, amesema matukio ya watumishi wa ndani kuua na kujeruhi watoto wa waajiri wao, yanatokana na vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa na familia husika.

“Kesi zinakuja mwajiri hajamlipa msichana mshahara wake mwaka mzima au miezi kadhaa, kwa hali ya kawaida huu ni ukatili halafu mtu huyo unamuachia mtoto akulele, kuna moyo wa uovu unaingia kwake,” amesema.

Amesema mwajiri anapoona hawezi kumtendea jambo zuri msaidizi wake ni vyema kumuondoa ili kuepusha madhara kwa watoto anaomwachia.

Naye, Naitham Kareem, mkazi wa Makumbusho jijini Dar es Salaam amesema, “Kuna baadhi ya watu wanaishi na msichana kama mnyama, hawezi kuchanganyika na waajiri wake kwa kila kitu hadi kwenye kula wanamtenga, hii naweza kusema ni roho mbaya watu wameumbiwa. Wanachosahau msaidizi hana pa kutolea dukuduku lake hivyo asipofikiria kwa makini humalizia hasira zake kwa watoto,”amesema.