Upungufu wa damu, tatizo Bagamoyo

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Dk Kandi Lusingu (kushoto) akizungumza na madiwani kuhusu tatizo la upungufu wa damu kwa wakazi wa wilaya hiyo.

Muktasari:

Wagonjwa wamekuwa wakigundulika na changamoto ya upungufu wa damu wanapofikishwa hospitalini kwa matibabu

Bagamoyo. Takribani wagonjwa sita kati ya 10 wanaofika kutibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani wanakutwa na changamoto ya upungufu wa damu kutokana na kutokula vyakula sahihi.

Akizungumza leo Jumanne Machi 5, 2024 wakati wa ziara ya siku moja ya timu ya madiwani na watalaamu wa Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara waliotembelea katika Halmashauri hiyo,  Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Dk Kandi Lusingu amesema licha ya utafiti kuendelea kufanyika, ulaji umekuwa ukichangia  kwa kuwa, wengi hawali mboga za majani.

Amesema wagonjwa wamekuwa na changamoto ya upungufu wa damu wanapofikishwa hospitalini kwa matibabu.

 “Unajua tatizo kubwa katika wilaya yetu ni upungufu wa damu ambao upo kwa kiwango kikubwa kwa sababu watu wanapanda mboga za majani, lakini hawali,” amesema Dk Lusingu.

“Mara nyingi wanakula ndimu na samaki, imetulazimu sasa kupita kila kijiji na kuandaa siku ya lishe na kuwafundisha lishe bora kwenye uji na mboga angalau tunaona mabadiliko madogo sasa.

 “Unaweza kupokea wagonjwa sita miongoni mwa 10 wakawa hawana damu ya kutosha bila kujali umri ndio maana tunafanya utafiti wa kina ili kuweza kujua licha ya chakula nini tatizo linasababisha changamoto ya ukosefu wa damu,” amesema Dk Lusungu.

Somoye Kayombo, diwani wa viti maalumu Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara amesema kuwa tatizo la upungufu wa damu ni kubwa na linapaswa kuwekewa mikakati ili kudhibiti.

 “Upungufu wa damu unaumiza hasa kwa wajawazito ambao ni vema kujua chanzo na dalili ili wataalamu waweze kutoa ushauri wenye tija kwa wananchi na waweze kuepuka madhara yanayoweza kupata wanapokuwa na upungufu wa damu,” amesema Kayombo.