Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ushuru tiketi mtandao pasua kichwa

Mkurugenzi Mtendaji wa Latra, Habibu Saluo akiwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng'azi wakiwa kwenye moja ya operasheni katika mabasi kukagua matumizi ya tiketi za abiria kuwabaini wanakwepa kutumia tiketi Mtandao.

Muktasari:

  • Latra yatoa ufafanuzi alichosema mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby.

Dar es Salaam. Wamiliki wa mabasi ya abiria ya masafa marefu wamelalamikia ushuru wa asilimia 0.5 unaotozwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kupitia tiketi mtandao, wakieleza kuwa unaongeza ugumu katika uendeshaji biashara.

Latra kupitia Sheria namba 35 ya Udhibiti na Kanuni za Usafirishaji wa Mabasi ya abiria ya mwaka 2020, imeweka kipengele kinachowataka watoa huduma kulipa walau asilimia moja ya mapato ghafi kwa ajili ya ushuru.

Kwa kutambua asilimia moja ni kubwa na ili kuvutia sekta binafsi kuwekeza, mwaka 2021 Serikali ilitengeneza kanuni za sheria hiyo na kupunguza ushuru hadi asilimia 0.5, unaotakiwa kutozwa kwa kila tiketi inayokatwa na abiria.

Baadhi ya wasafirishaji na vyama vinavyohusika na sekta hiyo, wanapinga ushuru huo kukatwa moja kwa moja kwenye tiketi wakitaka kiasi hicho cha fedha kiingizwe kwenye leseni ya biashara ili kuwapa nafuu ya uendeshaji, wakieleza wamekuwa wakilipia ushuru wa maegesho na kwenye stendi, hivyo kuongeza gharama za uendeshaji.

Mei 6, 2024 akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby alilalamikia ushuru wa Sh3,000 unaotozwa kwa kila tiketi mtandao, akisema unawagharimu wamiliki wa mabasi.

 “Sasa unakuta kwenye basi abiria mmoja anakatwa Sh3,000 inakatwa juu kwa juu kwenye tiketi mtandao, sasa mmekuwa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) badala ya kudhibiti watu, hii haiwezekani lazima mjitafakari na hasa mkurugenzi mpya usije ukaleta mzozo wa watu wenye mabasi kugoma,” alisema.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Latra, Habibu Suluo, akizungumza na Mwananchi amesema kiwango cha ushuru kilichotajwa na Shabiby si halisi, bali kinachotozwa kwa kila tiketi ni asilimia 0.5 kwa mujibu wa kifungu cha 35 cha Sheria ya Latra.

Suluo ametoa mfano akisema ushuru wa asilimia 0.5 kwa mabasi yanayoenda Dodoma kutoka Dar es Salaam kwa nauli ya Sh20,000 katika kiwango hicho Latra inachukua Sh100 kwa kila tiketi.

“Mfano mwingine kama abiria anakatiwa tiketi kwa Sh40,000 katika kiwango hicho kwa kuzingatia sheria hiyo, tunachukua Sh200 kwa kila tiketi ya abiria; kwa abiria anayekwenda Kigoma na kulipa nauli Sh100,000 ambayo ni safari ndefu, Latra tunachukua Sh500,” amesema Suluo.

Amesema asilimia 15 kati ya fedha zinazokusanywa katika ushuru hupelekwa serikalini na kinachobakia hutumika katika uendeshaji wa taasisi hiyo, ikiwemo kuwalipa mishahara watendaji wake.


Kauli ya Taboa

Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo amesema wamiliki wa mabasi hawapo tayari kulipa ushuru huo, hivyo wapo kwenye vikao kupata ufumbuzi wa jambo hilo.

“Sisi Taboa tuko kwenye mjadala na Latra wa hiyo asilimia 0.5 ili kupata muafaka. Wameona abiria wengi hawakati tiketi mtandao wanaenda kukata ofisini na vituoni, ndiyo maana tumeingia kwenye vikao vinavyoendelea kupata ufumbuzi,” amesema.

Amesema wanashauri ushuru wa asilimia 0.5 utozwe kupitia leseni za biashara.

Gharama ya leseni ya mabasi ya masafa marefu kwa mwaka, kwa daraja la kawaida (Ordinary) ni Sh120,000, daraja la kati la kwanza (Lower semi Luxury) ni Sh120,000 na daraja la kati la pili (Upper semi Luxury) ni Sh170,000, wakati daraja la starehe (Luxury) ni Sh170,000.

Viwango hivyo kwa mujibu wa Latra, vinajumuisha gharama ya maombi ya leseni Sh10, 000 na ya ratiba Sh10, 000.

Kwa mujibu wa Mwalongo kiwango cha asilimia 0.5 kwa gari linaloenda Mwanza kutoka Dar es Salaam ni Sh7, 000 kwa siku, ambayo kwa mwezi ni Sh210, 000.

“Itaumiza, unakuta mtu kwenye kampuni ana magari 15 na wengine 30 ukipiga hesabu kwa mwaka ni hela nyingi, wapo ambao  wanakata tiketi kupitia mtandao na mabasi mengine hawatumii, ndiyo maana hawajaanza kuhisi maumivu,” amesema.

Kwa mujibu wa Mwalongo, tangu mwaka jana wameshafanya vikao vinne lakini hawajapata ufumbuzi.

Hata hivyo, Suluo amesema hakuna vikao vinavyofanyika kujadili suala hilo, isipokuwa kinachofanyika ni Latra kutoa elimu kwa wasafirishaji kuhusu umuhimu wa kulipa ushuru huo kwa mujibu wa sheria.

“Hakuna mazungumzo ni kuendelea kutoa elimu ili tukianza kuchukua hatua na kuwatoza faini wajue tulishawaelimisha,” amesema Suluo.

Kwa mujibu wa Suluo faini ni Sh250, 000.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Machi, 2024 katika kituo cha mabasi cha Magufuli ulibaini baadhi ya mabasi hayatumii tiketi za kielekroniki.

Baadhi ya wenye mabasi hususani ya daraja la kawaida la lile la kati, hawatoi tiketi za kielekroniki kwa maelezo kwamba mashine imeharibika, au wakimtaka abiria apande basi na baada ya kuwa ameingia ndani, hapewi tiketi hiyo.

Wapo wengine wanaotoa tiketi za kawaida kwa maelezo kuwa zitabadilishwa na baada ya abiria kuingia ndani ya basi hilo halifanyiki, huku wengine wakitakiwa kuingia kwenye basi pasipo kuelekezwa namba ya kiti cha kukaa.

Katibu wa Taboa, Priscus John amesema hawapo tayari kulipa ushuru huo moja kwa moja kupitia tiketi kwa kuwa wamiliki wengi hawana bajeti toshelevu ya kumaliza safari hadi mwisho.

“Shida Latra wanataka kuchukua ushuru kwa kila abiria lakini gharama zetu za uendeshaji ni ngumu kila stendi tunayoingia tunalipa ushuru, na nyingi hawatoi risiti,” amesema.

Amesema wanalipa ushuru katika wilaya zenye huduma na stendi zote wanazopita barabarani.

“Kwa siku gharama ya uendeshaji wa basi moja kutoka Dar es Salaam hadi Musoma ni Sh150,000, kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma Sh120,000, na kutoka Dar es Salaam hadi Songea Sh110,000 hizo nilizotaja ni matumizi ya kawaida na ushuru kwenye standi,” amesema.

Mmiliki wa mabasi yanayofanya safari kati ya Dar es Salaam na Mtwara ambaye hakutaka jina lake kuwekwa wazi amesema biashara hiyo ni ngumu kiuendeshaji, hivyo ni muhimu Latra ikubali kuweka kiwango hicho cha ushuru kwenye leseni ya biashara.

“Kulazimisha kutoza kwa kila tiketi kiuendeshaji itazidi kutuumiza, kila siku gharama zinazidi kupanda,” amesema.


Walichosema Uwamata

Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Mabasi (Uwamata), Majura Kafumu amesema kila wanaposhusha abiria lazima walipe ushuru.

“Mfano stendi ya Magufuli gari likilala ndani kuna gharama ya maegesho na ushuru wa Manispaa jumla inakuwa kama Sh9,000, unapoingia Pwani jumla ni Sh6,000, Kibaha Sh2,000 na wanalazimisha kuingia Mlandizi Sh2,000 na ukifika Chalinze wanakulazimisha kuingia stendi Sh2,000,” amesema.

Kafumu amesema mkoani Morogoro wanatozwa Sh5,000 zilizogawanyika maeneo mawili kuanzia stendi ya Msamvu Sh3,000 na ukifika Mikumi Sh2,000.

“Ukiwa unaenda Dodoma ukifika Gairo Sh2,000 sawa na Kibaigwa, Bahi na Manyoni, ni lazima uingie hata kama huna abiria,” amesema.