Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ushuru wa maegesho sasa wageuka shubiri

Moshi. Mfumo wa ukusanyaji ushuru wa maegesho (parking fee) ambao halmashauri zimeurithi kutoka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), umegeuka shubiri kwa wamiliki wa magari katika mji wa Moshi.

Kinachoonekana, malalamiko ya wamiliki wa magari katika miji mikubwa yaliyofanya chanzo hicho kurejeshwa halmashauri Julai, 2022 ndio hayo hayo yanatikisa mji wa Moshi huku wamiliki wakitaja changamoto tano kubwa.

Changamoto hizo ni mfumo kutotuma meseji kwa mmiliki kuwa ametozwa ushuru wa shilingi ngapi, kwa kuegesha gari wapi na kwa muda gani na watoza ushuru kutoweka karatasi yoyote kwa mmiliki kumjulisha anadaiwa ushuru.

Mbali na changamoto hizo, wamiliki wanalalamikia kuandikiwa ushuru katika maeneo ambayo hawajawahi kufika tena nje ya Mkoa wa Kilimanjaro na watoza ushuru kuwekewa lengo kumechangia wafanye udanganyifu.

Ukiacha changamoto hiyo, wamiliki wa magari wanalalamika kutozwa ushuru hata wakiwa wamesimama kwenye eneo la kuvuka watembea kwa miguu (Zebra Crossing) ambapo watoza ushuru hupiga picha na kuliandikia gari ushuru.


Akiboa: Mfumo ufumuliwe

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi mikoa ya Kilimanjaro na Arusha (Akiboa), Hussein Mrindoko, alisema mfumo huo unapaswa kufumuliwa kwa kuwa hauna tofauti na ufisadi kwa baadhi ya tozo kuwa na mashaka.

“Jana nimeambiwa nadaiwa Sh25,000 ya ushuru wa maegesho. Sasa nawauliza nili park (kuegesha) wapi hadi ifikie Sh25,000 kumbe ni malimbikizo. Mie sina taarifa kama nadaiwa,” alisema.

Katibu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Kilimanjaro, Awadhi Lema alisema tatizo hilo la mfumo wa maegesho ni kubwa kwa kuwa unaweza kukuta gari hukutoka nayo siku hiyo, lakini ukikagua unakuta unadaiwa.

“Hili tatizo ni kubwa na linakera hasa kwa wamiliki wa magari wakati mwingine gari limepaki nyumbani ukilikagua unakuta linadaiwa wakati gari halijatoka. Nafikri wanatakiwa wabadilishe mfumo wa utozaji ushuru.

“Inapaswa iwe kwamba huwezi kumuandikia mtu mpaka umuone mwenye gari ndiyo umuandikie, lakini mtindo wa kuandika na kubandika kwenye kioo na wakati mwingine wala hukuti karatasi yoyote,”alisisitiza Katibu huyo.


Wamiliki magari wapaza sauti

Baraka Matemba, mkazi wa Moshi na dereva wa muda mrefu, alisema jana kuwa kuna siku aliandikiwa ushuru kuwa ameegesha gari soko la Juu wakati hajawahi kupita eneo hilo wiki nzima na kutaka mfumo huo ushuru ufumuliwe.

“Kuna mmoja akamulika gari yangu nikiwa kwenye zebra nimesimama, pale nje Kindoroko Hoteli nikashuka nikamuuliza kwani hapa nime park (kuegesha). Akasema samahani. Sasa si ni bahati nilimuona?

“Baadhi wanaingiza kwenye mfumo bila kuweka karatasi kwenye kioo kama tulivyokuwa tumezoea. Tunaomba dereva ajulishwe gari yake inapoandikiwa madai au apewe karatasi,”alieleza.

Kwa upande wake, Hilda Lyimo alidai aliwahi kukuta anadaiwa ushuru na aliposoma vizuri akagundua inanyesha kuna siku aliegesha gari Dar es Salaam wakati yuko Bristol Cottage mjini Moshi na hajawahi kwenda huko na gari.

“Changamoto na kero kubwa ni pale unakuta umeegesha sehemu kuchukua kitu kwa sekunde kadhaa unakuta tayari ameandika. Kero nyingine ni kukatiwa ushuru saa 11 jioni au saa 12 nje kabisa ya muda ule wa kazi. Huwa sielewi,”alisema.

Mtangazaji wa Radio Banana FM, Esther Machangu alisema mfumo wa sasa ni kero kubwa na kutaka utaratibu wa zamani urejeshwe ambapo mkatishaji ushuru alikuwa anakwenda kwenye gari na kukutaka ushuru na kulipa fedha taslimu.

“Wakati mwingine wanapiga picha magari yanayotembea. Huu mfumo uondolewe umetuletea madeni yasiyo na maana,” alisema.

Robert Minja, alisema changamoto kubwa ni malengo waliyowekewa watoza ushuru na kwa kuwa mfumo hurekodi kumbukumbu za nyuma, baadhi ya watoza ushuru wanapoona siku inaisha hawajafikia lengo.

“Cha kufanya Serikali iangalie namna bora ya ukusanyaji wa ushuru wa maegesho kwa kuangalia kiwango cha tozo, muda wa kikomo na mmiliki aweke karatasi ya madai na sio kufanya kwa siri kama wanavyofanya,” alisema Minja.

Kwa mujibu wa Minja, mfumo wa mmiliki wa gari kupata ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kujulishwa gari yake imekatiwa ushuru ni kwa wale waliojisajili kwenye mfumo na akisema hao ni wachache na wengi hawajui utaratibu huo.

Hussein Mfinanga, alisema anaupenda mfumo huo kwa sababu unaepusha kelele na majibizano na watoza ushuri na unampa muda mzuri kulipa kwa utulivu ila changamoto ni kutozwa ushuru katika maeneo ambayo hakuegesha siku hiyo.


Manispaa Moshi wakiri tatizo

Mwanasheria wa Manispaa ya Moshi, Sifaeli Kulanga alisema kumekuwepo na changamoto na wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka kwa wananchi yanayohusiana na maegesho na kwamba wameendelea kuzishughulikia.

"Chanzo cha maegesho kilikuwa kinasimamiwa na Tarura, lakini kuanzia Julai 2022 kilikabidhiwa Manispaa. Tunaendelea kukisimamia pamoja na changamoto zake nyingi ambazo zinajitokeza ikiwemo changamoto ya teknolojia,”alisema Kulanga.

“Zamani ilikuwa mtu anaegesha gari lake anawekewa stika, lakini kwa sasa mtu anaegesha anapigwa picha mtu ana scan number (kuchukua namba) ya gari. Tumekuwa tukipokea changamoto mbalimbali juu ya suala hilo,” alieleza na kuongeza:

“Ziko changamoto za watu kulalamika magari yao kuonyesha yameegeshwa Tanga, Dodoma lakini yuko Moshi, huu ni muingiliano wa mashine hizi na tumeendelea kuripoti changamoto hizi kwa wakala baada ya kuyapata kutoka kwa mteja na yanafikishwa makao makuu kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

"Changamoto tunazipokea nyingi na mara ya mwisho tumeipokea ni kwamba kuna mtu Ushirika yeye gari yake imeegeshwa nyumbani, lakini mkeka unakuja ameegesha mjini, wakati mwingine Arusha huku gari iko nyumbani, changamoto hiyo tumeichukua na kuiripoti ambapo imefanyiwa kazi."