Prime
Utaratibu huu hapa bima ya afya kwa wote ikianza leo
Muktasari:
- Serikali imetangaza gharama, makundi yatakayogharamiwa na hatua za usajili, huku ufuatiliaji wa huduma ukifanywa kwa kutumia alama za vidole na utambuzi wa sura ili kudhibiti udanganyifu.
Dar es Salaam. Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unaanza rasmi leo, Januari 26, 2026, ukiwa na lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya bila kikwazo cha fedha.
Mpango huo unafanywa chini ya Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance Act, 2023) iliyopitishwa na Bunge, Novemba mosi, 2023 na ikatiwa saini na Rais Samia Suluhu Hassan, Novemba 19, 2023, kabla ya kutangazwa na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali, Toleo Namba 48 la Desemba mosi, 2023.
Hivyo, hatua zote kuu za kupitishwa na Bunge, kutiwa saini na Rais, na kuchapishwa katika gazeti la Serikali, zinafanya kuwa sheria kamili itakayomlazimisha kila raia wa Tanzania kuwa na bima ya afya.
Kwa mujibu wa tamko la Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, mpango huo unaanza na wananchi wasio na uwezo, wakiwamo wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu, ambao gharama zao zitabebwa na Serikali kwa ufuatiliaji utakaofanywa kwa kutumia alama za vidole na utambuzi wa sura ili kudhibiti mianya ya udanganyifu.
Katika utekelezaji wake, Waziri Mchengerwa amekasimisha jukumu hilo wiki iliyopita kwa wakuu wa mikoa yote nchini kubeba dhamana ya moja kwa moja katika mikoa yao.
Katika kikao cha kazi alichokaa nao wakiwa wameambatana na makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wilaya na wakurugenzi wa halmashauri, Mchengerwa alisema awamu ya kwanza ya utekelezaji itaambatana na kuanza kutumika kwa kitita cha huduma muhimu.
Alisema kitita hicho kitatolewa na Skimu za Bima ya Afya, wakilenga makundi yaliyo hatarini, ikilenga wapate huduma za afya bila kikwazo cha fedha.
"Bei ya kitita hicho ni Sh150,000 kwa kaya isiyozidi watu sita, kikiwa kinazingatia utaratibu wa rufaa katika vituo vya afya vilivyoingia mkataba na Skimu za Bima ya Afya," alisema Mchengerwa na kuongeza:
"Huu si mradi wa wizara moja, bali ni ahadi ya Taifa kwa wananchi wake. Mafanikio ya mpango huo yatapimwa si kwa hotuba wala maagizo, bali kwa idadi ya wananchi wanaolindwa dhidi ya gharama za matibabu na wanaopata huduma kwa heshima."
Mbali na kifurushi hicho cha msingi, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), utakaosimamia mpango huo, umeandaa vifurushi vingine kulingana na uwezo wa mwanachama.
Kifurushi cha Tarangire kwa kaya ya watu sita ni Sh796,560; Ngorongoro Sh1,684,800; Mikumi Sh2,621,760; Serengeti Sh3,880,800, huku kifurushi cha juu zaidi cha Tanzanite kikigharimu Sh11,162,640 kwa kaya ya watu sita.
Jinsi itakavyofanya kazi
NHIF wanaeleza kwa kina namna Bima ya Afya kwa Wote itakavyotekelezwa, namna ya kujisajili na gharama za vifurushi mbalimbali kwa kaya ya watu sita.
Kifurushi hicho chenye huduma 277, kinaeleza kuwa kiongozi wa kaya atalipia kwa mkupuo au kupitia kampuni ya simu, kuanzia na Sh14,000 na kisha mtumiaji atakatwa kidogo kidogo mpaka atakapokamilisha Sh150,000 ya kifurushi cha kaya.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Desemba 22, mwaka jana, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka alisema wameanza utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Alisema mifumo yao imesimama na imeshafanyiwa majaribio, wananchi wanaweza kujisajili wenyewe, waajiri kusajili wafanyakazi, na michango kulipwa kwa njia ya mtandao.
Kwa mujibu wa Dk Isaka, msingi wa mpango huo ni kifurushi cha huduma muhimu chenye gharama ya Sh150,000 kwa mwaka kwa kaya isiyozidi watu sita, ambacho kitawezesha mwanachama kupata matibabu ya magonjwa muhimu katika ngazi ya msingi, kwa kuzingatia utaratibu wa rufaa.
“Kaya zisizo na uwezo zitatambuliwa kupitia Tasaf na kugharamiwa na Serikali, kwa wananchi wa kaya hizi, wataanza kunufaika mara moja pindi utekelezaji unapoanza,” alisema Dk Isaka.
Ngazi ya pili ni ile ya kuchangia kwa mujibu wa sheria kwa sekta rasmi, yaani sekta ya umma na binafsi, ambapo asilimia tatu inakatwa kwa mwajiriwa na asilimia tatu anachangia mwajiri, na kufanya kuwa asilimia sita.
Ngazi ya tatu ni ya hiari, ambapo NHIF, ambao wana vifurushi, watashirikiana na Jubilee, Strategy, Assembly na wengine kama NSSF wenye vifurushi wanavyovitoa kwa sekta isiyo rasmi.
Baadhi ya wataalamu wakizungumza na Mwananchi jana Jumapili Januari 25, 2026, wanasema kuanza kwa bima hiyo ya afya kwa wote ni mabadiliko makubwa katika mfumo wa afya nchini, lakini utekelezaji wake utahitaji maandalizi ya kutosha.
“Kimsingi huu ni mpango mzuri skwa usawa wa kijamii. Changamoto itakuja kwenye uwezo wa vituo vya afya kuhudumia idadi kubwa ya wagonjwa bila kuchelewa au kupungua kwa ubora wa huduma,” anasema Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania, Dk Mugisha Nkoronko.
Dk Nkoronko anasema madaktari wanatamani wananchi wote washiriki kuchangia kwenye mfuko, kwa sababu bila kufanya hivyo hakutakuwa na matokeo.
“Ni muhimu kufanya utafiti na wachumi wa afya watuambie wastani mtu mmoja anahitaji shilingi ngapi kwa huduma za afya kwa mwaka, tuhakikishe kila mmoja anailipa kwa njia fulani ili iingie kwenye mfuko moja kwa moja, ikiwezekana,” anasema.
Hata hivyo, wataalamu wa uchumi wa afya wanasema mfumo huo unaweza kupunguza umaskini unaosababishwa na gharama za matibabu endapo utasimamiwa vizuri.
“Kaya nyingi zimekuwa zikiingia kwenye madeni kwa sababu ya matibabu. Bima ya afya kwa wote inaweza kubadilisha hali hiyo, lakini uwazi wa michango na ulipaji wa watoa huduma ni jambo la msingi,” anasema Mchumi, Catherine Mwinuka.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi wanaelezea matumaini makubwa, huku wengine wakitaka ufafanuzi zaidi kuhusu namna mpango huo utakavyofanya kazi.
Mkazi wa Temeke, mkoani Dar es Salaam, Asha Mohammed, anasema: “Kama kweli gharama itakuwa nafuu na huduma zitapatikana bila usumbufu, hii itatusaidia sana, hasa sisi wenye watoto.”
Juma Selemani, mfanyabiashara mdogo kutoka Mwanza, anasema anaunga mkono mpango huo lakini ana hofu kuhusu utekelezaji wake.
“Tumeshawahi kusikia mipango mizuri, lakini changamoto imekuwa kwenye utekelezaji. Tunaomba ianze kwa uwazi na ubora wa huduma,” anasema.
Serikali imesema imejipanga kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi, kwa kushirikiana kati ya NHIF na watoa huduma binafsi. Elimu kwa umma itaendelea kutolewa ili wananchi waelewe haki na wajibu wao chini ya mfumo mpya wa bya afya.