Utitiri wa mageti ya ushuru hifadhini wakera wadau wa utalii

Muktasari:

  • Uwepo wa mageti mengi ya ushuru ndani ya maeneo ya hifadhi imetajwa kuwa kero kubwa kwenye biashara ya utalii nchini, huku Serikali ikitakiwa kutengeneza dirisha moja pekee la kukusanya mapato ili kuondoa kero hiyo.

Arusha. Uwepo wa mageti mengi ya ushuru ndani ya maeneo ya hifadhi imetajwa kuwa kero kubwa kwenye biashara ya utalii nchini.

Kutokana na kero hiyo, wadau wa utalii wameishauri Serikali kutengeneza dirisha moja pekee la kukusanya mapato.

Hayo yamesemwa Oktoba 5 na wadau wa utalii Kanda ya Kaskazini kwenye mkutano wa ukusanyaji maoni juu ya changamoto wanakabiliana nazo, ulioandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa lengo la kuboresha sera na sheria za sekta hiyo ili kuongeza mapato na ajira.

Akizungumza kwenye mkutano huo, katibu wa Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania (TCT), Richard Rugimbana amesema Serikali ikiboresha sekta ya utalii itarudisha sekta hii katika nafasi nzuri ya kuchangia mapato nchini.

"Mtalii anapokuja nchini anataka astarehe na kufurahia maisha kwa muda na wakati wake, sasa tunaingia kule unajikuta kila kituo unasimama kuanza kudaiwa ushuru unaojirudia.

"Tafadhali sana Serikali, sisi hatuna nia ya kukwepa msikusanye fedha bali mtuokolee muda, kwa kutengeneza dirisha moja la kulipa kodi, tozo na mapato yoote pamoja ili mtu ukiingia hifadhini uwe huru," amesema Rugimbana.

Kwa upande wake Kamishna wa Sera kutoka Mizara ya Fedha na Mipango, Elijah Mwandumbya amesema kuwa wamekutana na wadau walioko kwenye mnyororo wa sekta hiyo ili kuja na sera, kanuni na taratibu zitakazotibu changamoto ili kuongeza watalii mapato na ajira.

"Changamoto kubwa iliyotajwa mbali na ubovu wa miundombinu ya barabara hifadhini, ni mageti yaliyoanzishwa na Serikali za Mitaa chini ya halmashauri zetu ili kupata mapato kwenye sekta ya utalii.

“Hivyo tutakaa pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi) tujadili kwa pamoja namna ya kuondoa vituo hivyo."

Amesema kuwa suluhisho la kuwa na dirisha moja ambalo wadau wa sekta ya utalii watakuwa wanalipa kodi, tozo na mapato yote hapo ni jambo linalotekezeka.

Awali akifungua mkutano huo kwa njia ya mtandao, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru alisema kuwa wameitisha mkutano huo baada ya nchi kuathiriwa na ugonjwa wa Uviko -19, na kuvuruga mwenendo mzima wa utalii na uchumi wa nchi.

"Lengo la mkutano huu ni kutekeleza maagizo ya viongozi wetu hasa Rais Samia Suluhu Hassan ya kutengeneza mazingira wezeshi ya sekta binafsi ziweze kukua tena na kuchangia maendeleo ya uchumi,"

"Awali kabla ya Uviko-19 sekta ya utalii ilikuwa inachangia zaidi ya dola 2 bilioni kwenye kwenye uchumi, lakini kwa sasa kiwango hicho kimepotea hivyo nawaomba tushirikiane kurudisha hili kwani bado vivutio tunavyo na sisi tutawatengenezea mazingira wezeshi kupitia sera za kibajeti na nyie fanyeni kazi yenu tufikie lengo," amesema Mafuru.