Uzalendo wa JKCI waokoa Sh47 bilioni

Muktasari:

Wagonjwa hao ni 1,055 waliofanyiwa upasuaji wa moyo wangetumia Sh46.4 bilioni, waliofanyiwa upasuaji wa kuwekewa betri maalumu ya kuwasaidia kupumua (Pacemaker) 16, wangetumia Sh976.8 milioni.

Dar es Salaam. Awali ilikuwa kama ndoto, lakini hivi sasa imedhihirika inawezekana baada ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kuokoa Sh47.3 bilioni ambazo Serikali ingezitumia kuwatibu wagonjwa wa moyo nje ya nchi baada ya kuwafanyia upasuaji watu 1,071 tangu kuanzishwa kwake Januari 9, mwaka jana.

Wagonjwa hao ni 1,055 waliofanyiwa upasuaji wa moyo wangetumia Sh46.4 bilioni, waliofanyiwa upasuaji wa kuwekewa betri maalumu ya kuwasaidia kupumua (Pacemaker) 16, wangetumia Sh976.8 milioni.

Hayo yalisemwa jana wakati JKCI ikitoa elimu kwa wagonjwa wa kliniki ya moyo kuhusu afya ya moyo, ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yenye kaulimbiu; ‘Yape nguvu maisha yako’. 

Mkuu wa Kitengo cha Utafiti cha JKCI ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Pedro Pallangyo alisema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo Januari mwaka jana hadi Agosti, mwaka huu watu 67,079 wametibiwa kama wagonjwa wa nje.