Uzalishaji umeme binafsi kuongeza uzalishaji viwandani
Muktasari:
- Kampuni za uzalishaji na usindikaji bidhaa za vyakula, vinywaji, saruji, vifungashio, nguo, dawa na uchimbaji madini, zinaweza kuzalisha umeme na kuokoa kati ya asilimia 15 hadi 25 ya gharama za nishati kwa kutumia gesi asilia.
Dar es Salaam. Baadhi ya wazalishaji wa bidhaa za viwandani nchini wameaanza kujizalishia umeme binafsi kwa lengo la kupata umeme wa uhakika utakaowahakikishia uzalishaji wa uhakika.
Hatua hiyo inakuja wakati Tanzania ikipitia mgawo wa umeme kutokana na ongezeko la watumiaji wakati uzalishaji ni mdogo na uchakavu wa mitambo na miundombinu ya Shrika la Umeme (Tanesco).
Tanzania inavyo vyanzo tofauti vya kuzalisha umeme ikiwamo gesi asilia yenye mita za ujazo trilioni ndani na nje ya bahari ya Hindi, ikizalisha umeme wa rasilimali hiyo katika vituo vya Songo Songo, Mnazi Bay, and Kiliwani.
Katika kuhakikisha kuwa wazalishaji wanapata umeme wa uhakika, kampuni ya kimataifa Clarke Energy imeanza kushirikiana na baadhi ya viwanda kwa kutoa majenereta yanayotumia gesi asilia kuzalisha umeme.
Hadi sasa kampuni hiyo imeshasimika mitambo inayozalisha Zaidi ya megawati 45 kwa wazalishaji nchi.
Akizungumza hivi karibuni katika mkutano wa wadau wa nishati jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi mtendaji wa Afrika, Yiannis Tsantilas amesema kwa sasa wazalishaji viwandani wanaweza kujihakikishia umeme wa kutosha kutokana na teknolojia mpya ya uzalishaji.
“Teknolojia hii inaleta umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya uzalishaji na usindikaji na kwa wazalishaji wa umeme binafsi na kuuza (IPP) wanaouza kwa viwanda vingine.
“Wateja wetu ni pamoja na viwanda vya vyuma, vioo, wazalishaji wa unga, tumbaku, mafuta na gesi,” amesema.
Ameongeza kuwa mitambo inayozalisha umeme huo inafungwa na kufanyiwa ukarabati na wataalamu nchini, huku kukiwa na karakana yenye vifaa.
“Kampuni yetu ina utajiri wa uzoefu wa kutosha wa kutoa nishati endelevu nay a uhakika kwa viwanda na kupitia mkutano huu tunalenga kutafuta ushirikiano na wadau wengine.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkuu wa Clarke Energy, Emile Hamman amefafanua kuwa, pamoja na uhakika, faida za kujizalishia umeme kwa kutumia gesi asilia kunasaidia kupunguza gharama kulingana na nishati nyingine.
“Kampuni nyingi za uzalishaji na usindikaji bidhaa za vyakula, vinywaji, saruji, vifungashio, nguo, dawa na uchimbaji madini, zinaweza kuzalisha kuokoa kati ya asilimia 15 hadi 25 ya gharama za nishati kwa kutumia gesi kuzalisha umeme.
“Uokoaji huo wa nishati unaweza kuongezeka kama mahitaji ya mteja yatakuwa na uhifadhi wa joto, yaani kutumia joto linalopotea kutoka kwenye moshi kutengeneza mvuke, maji ya moto au kupoozea,” alisema.
Alisema, mara mtambo wa gesi ukishasimikwa, unaungwa na mtandao wa mabomba ya gesi au vifaa vingine vinavyosafirisha gesi kama ilivyogandamizwa (CNG) au gesi ya kimiminika (LNG) kwenda kwa mteja na mgavi wa gesi.
“Timu yetu itakabidhi mtambo wa kuzalisha umeme na mtandaow a gesi kwa mteja na mpango wa kuhudumia mtambo huo.
Hadi kufikia mwaka 2021, Tanzania ilikuwa ikizalisha megawati 1,605.86 za umeme ambazo kati yake asilimia 48 ni kwa gesi asilia, maji asilimia 31, petrol asilimia 18 na nishati za viumbe asilimia moja. Tanzania pia imekuwa ikiingiza umeme kutoka Uganda, Zambia na Kenya.