Nchi inahitaji zaidi uwekezaji mkubwa, tuvute wawekezaji

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akikata utepe pamoja na viongozi wengine wakati wa uzinduzi wa Kiwanda cha Vioo cha Sapphire Floating Glass kilichopo Mkuranga mkoani Pwani. Picha na Ikulu

Hivi karibuni Tanzania ilishuhudia uzinduzi wa uwekezaji mkubwa wa kiwanda cha kuzalisha vioo vya ujenzi, ikiwa ni cha nne kujengwa barani Afrika na cha kwanza katika ukanda wa Afrika mashariki na kati.

Jumla ya uwekezaji wake unatajwa kuwa Dola za Marekani 311 milioni (Sh779 bilioni), ni mkubwa wenye maana katika uchumi wa nchi yoyote, ikiwamo Tanzania ambayo ipo katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Ajira zitakazozalishwa zinatajwa kuwa zaidi ya 1,600, huku zisizo za moja kwa moja zikitajwa kuwa zitafikia 6,000, uzalishaji wake wa sasa ukiwa tani 700 kwa siku.

Kwa mujibu wa wawekezaji wa kiwanda hicho, ujenzi ukikamilika kitazalisha zaidi tani 500.

Asilimia 75 ya vioo vitakavyozalishwa na kiwanda hicho vitauzwa nje ya nchi, huku asilimia 25 vikiuzwa katika soko la ndani.

Kiwanda hicho kinatumia malighafi za ndani kwa asilimia 80 na asilimia 20 zinatoka nje ya nchi.

Katika uzinduzi wa kiwanda hicho, Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kuwa atafanyia kazi mapendekezo yaliyopo ili hiyo asilimia 25 nayo itoke nchini katika eneo la Engaruka.

Kwa kuongeza usambazaji wa bidhaa hiyo nchini na kutumia malighafi za ndani katika uzalishaji, kunaleta matokeo chanya ya kiuchumi, kwa kuwa mnyororo wake wa thamani ni mkubwa na watu wanaonufaika ni wengi.

Akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda hicho, Balozi wa China nchini, Chen Minjian alitoa wito kwa wawekezaji kutoka nchini mwake kuendelea kuwekeza Tanzania kwa masilahi ya ushirikiano wa nchi hizo mbili.

Mwakilishi huyo wa China nchini aliongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni miradi mingi ya uwekezaji kutoka China imekuja na kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta ya uchumi.

Takwimu za mwaka 2022 zinaonyesha kuwa thamani ya biashara baina ya mataifa hayo mawili ilikuwa Dola za Marekani 8.31 bilioni.

Pia ikiongezeka kwa asilimia 100 ndani ya miaka 10 na mpaka sasa China ndiyo mbia mkubwa wa kibiashara kwa Tanzania.

Minjian alisema viwanda kama hivyo ambavyo uwekezaji wake ni mkubwa ni matokeo ya mradi ulioanzishwa na Rais Xi Jinping wa Ukanda Mmoja Njia Moja (BRI), na vina mchango mkubwa katika kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda na kutengeneza fursa nyingi kwa wazawa, zikiwemo za ajira.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Wangkang Investment Group, Frank Yang, kiwanda chake ni kikubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kikiwa na ukubwa wa eneo la ekari 169.

Yang alisema kuwa uwepo wa kiwanda hicho Tanzania haitaagiza tena vioo vya ujenzi nje ya nchi na badala yake itakuwa muuzaji mkubwa kwa nchi zinazoizunguka.

“Uzinduzi wa kiwanda hiki ni hatua kubwa, tunataka Tanzania iache kuagiza vioo na tutaendelea kuangalia uwezekano wa kupanua uwekezaji wetu hapa nchini na kuwa mabalozi wema wa uwekezaji Tanzania," alisema Yang, huku akieleza kwa nini Tanzania ni sehemu sahihi kwa uwekezaji.

Uwekezaji kama huo unaiweka nchi yetu katika ramani ya uzalishaji barani Afrika, ikizingatiwa fursa kubwa iliyopo sasa ya Soko huru la Afrika (AfCFTA). Tanzania itakuwa katika nafasi nzuri ya kuwa muuzaji wa vioo badala ya kuwa mwagizaji.

Akizungumzia uwekezaji huo, Waziri wa Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema mbali na faida za kimtaji na ajira, Serikali itapata mapato mapya ya kodi ya Sh42.79 bilioni kwa mwaka, lakini pia kiwanda hicho kitatusaidia kuokoa Dola milioni 54 ambazo zilikuwa zinatumiwa kuagiza vioo nje ya nchi.

Kwa muda mrefu viongozi wamekuwa wakipigia chapuo na kuvutia uwekezaji kutoka nje kama kigezo muhimu cha kukuza uchumi wa nchi.

Nasisitiza uwekezaji kama huu wa Sapphire ndio unaohitajika kwa nchi yetu kwa kuwa unaleta manufaa tofauti muhimu.

Kwanza kwa ukubwa wake matokeo yake yanakuwa makubwa kuanzia kuongeza ukwasi katika mzunguko wa fedha, kupunguza mzigo wa kuagiza bidhaa nje ya nchi na hata ajira kwa Watanzania.

Kila mtu kwa nafasi yake ni muhimu kushiriki katika uvutiaji wa wawekezaji nchini, hususan uwekezaji mkubwa kama huu ambao unaleta manufaa makubwa.

 Hata Serikali katika mikakati yake ya kuvutia uwekezaji ifikirie ule ambao unaleta athari chanya katika nyanja tofauti.

Kwa mtazamo wangu, mbali na uwekezaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa muhimu zinazohitajika sokoni kama vioo, eneo lingine ambalo linaweza kuwa na athari chanya endapo uwekezaji ukifanyika kwa ukubwa ni kilimo na uongezaji wa thamani wa bidhaa zake.

Ephrahim Bahemu ni mwandishi wa gazeti hili (0756939401)