Uzuri na kadhia za Hospitali ya Mloganzila

Muktasari:

Hospitali ya rufaa Mloganzila ni tawi la Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na ina kila aina ya vielelezo kuwa miongoni mwa taasisi za kisasa za afya Afrika Mashariki.

Dar es Salaam. Ukitaja hospitali zinazoongoza kwa muonekano mzuri kwa sasa nchini Tanzania ni pamoja na Mloganzila.

Hospitali hiyo ya rufaa ni tawi la Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na ina kila aina ya vielelezo kuwa miongoni mwa taasisi za kisasa za afya Afrika Mashariki.

Ukifika eneo ilipojengwa, nje ya uzio wake unakutana na ‘round about’ iliyopambwa na bustani yenye maua na majani yenye rangi ya kijani kibichi licha ya kuwepo na hali ya jua kali linalowaka kwa sasa jijini Dar es Salaam.

Uzio wake wa rangi ya kijani unaendana na majani ya ukoka yaliyopambwa kwa ustadi kuzunguka hospitali hiyo kabla ya kufika kwenye lango kuu la kuingilia lililotengenezwa kwa uimara na mvuto wa aina yake.

Ndani ya viunga vya hospitali kuna eneo kubwa la kuegesha magari na vibanda maalumu vilivyotengenezwa kwa ajili ya watu kupumzikia wakisubiri muda wa kuona wagonjwa.

Ukiacha muonekano wa nje, hospitali hiyo inasifika kwa kuwa na vifaatiba vya kisasa, miundombinu ya kutosha kwa ajili ya matibabu na huduma za uhakika zinazotolewa na madaktari waliobobea.

Hata hivyo waswahili husema ‘kizuri hakikosi kasoro’, ndivyo ilivyo kwa hospitali hiyo ambayo sasa kumeanza kujitokeza dosari ndogondogo zinazozua malalamiko kwa wananchi wanaofika hospitalini hapo kuwaona jamaa zao waliolazwa.

Hospitali hiyo imeweka utaratibu wa kila anayekwenda wodini kumuona mgonjwa lazima apatiwe kadi maalumu anayopaswa kuionyesha katika lango kuu la kuingilia jengo la hospitali.

Utaratibu huo ndio kiini cha malalamiko kwa sababu umekuwa ukiwasababishia watu kusota kwenye foleni tena wakiwa juani wakisubiri kupatiwa kadi hizo.

Mwananchi lilifika hospitalini hapa juzi Novemba 29 saa 9:45 alasiri na kukuta watu wengi wakiwa wamefika ili kuwahi foleni hiyo.

Kama ilivyo kwenye maeneo yaliyo na shida ya maji ya bomba, ndoo na mabeseni mabovu hutumika kupanga foleni ili maji yatakapoanza kutoka, mhusika akinge kwa haraka.

Ndivyo ilivyo kwa Mloganzila kwani Mwananchi lilishuhudia misururu ya vikapu, viatu na chupa za chai zinazosimama badala ya watu wanaosubiri muda ufike ili wapatiwe kadi za kuingia wodini.

Na ilipofika saa 9:55 alasiri, watu wote waliokuwa pembeni walionekana kunyanyuka na kusimama kwenye mstari bila kujali jua kali lililokuwa likiwaka muda huo.

Wenye vipochi wanavitumia kujikinga jua na wengine wakifanya hivyo kwa mitandio na mikono, lakini hakuna aliyeonekana kukata tamaa na kusogea kivulini.

Saa 10:00 jioni, askari wa Suma JKT aliwasili eneo hilo akiwa na kadi mkononi alizoanza kuzigawa kwa kufuata foleni na safari ya kwenda wodini ikaaanza.

Cha kushangaza, baada ya muda mfupi hakuwa na kadi nyingine tena mkononi na Mwananchi lilihesabu kadi alizogawa na kubaini kuwa hazikuzidi 25.

Hivyo askari alilazimika kuhesabu watu 20 na kuwapa namba kwa mdomo kisha alisitisha na kwenda jengo la utawala kuchukua kadi nyingine.

Wakati askari anapofuata kadi nyingine watu wanaendelea kusimama juani wakisubiri muda wao ufike wakawaone wagonjwa wao.

Mama mmoja alisikika akilalamika, “Yaani nikifika hapa ndiyo hamu ya kuja huku inaisha, jua kali unaanza kuchoka kabla hujamuona mgonjwa.”

Watu waliendelea kuwa watiifu wakimsubiri askari hadi aliporejea na kuendelea na kazi yake ya kugawa kadi na zilipoisha aliondoka na kuzifuata tena wodini.

Ni takribani dakika 18 hadi 20 askari huyo anatumia kuwamaliza watu wote walioko kwenye foleni na kuanza kuwahudumia wanaokuja kwa kuchelewa.

Mwandishi wa Mwananchi anakuwa miongoni mwa wanaochukua kadi hizo na kwenda wanakoelekea wengine, huko nako kuna foleni nyingine. Foleni hiyo ni ya kumpa kadi askari mwingine ambaye kazi yake ni kupokea zinazotolewa na askari wa nje ili awaruhusu kuelekea wodini.

Askari huyo anapokea kadi bila kumhoji mtu anakwenda wapi na kufanya nini, hapo ndipo linapokuja swali kadi hizo zina maana gani?

Swali hilo linaulizwa pia na baadhi ya watu waliozungumza na Mwananchi huku wakionyesha kulalamikia utaratibu huo.

“Hospitali nzuri lakini utaratibu mbovu kabisa, mtu unaweza kusimama kwenye foleni dakika 15 unasubiri kupata kadi ya kwenda kumuona ndugu yako anayeumwa, na eneo lenyewe la kusimama hakuna kivuli,” alisema Ali Sultan mkazi wa Mburahati.

Naye Neema Mkinga mkazi wa Kimara Temboni, ni miongoni mwa waliokumbwa na kadhia hiyo.

Alisema dosari hiyo ndogo inapaswa kufanyiwa marekebisho mapema kabla haijawa sugu.

“Hii hospitali ni mpya inawezekana bado hawajajua ni utaratibu gani unaweza kufanyika kuepusha usumbufu huu, mambo mengine yote yanakwenda vizuri,” alisema Mkinga.

Mwananchi lilimtafuta Kaimu Naibu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Julieth Magendi aliyekiri kuwepo na idadi kubwa ya watu wanaokwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kuona wagonjwa.

“Foleni inaonekana kwa sababu watu ni wengi, kama unavyofahamu utamaduni wa kiafrika unaweza kukuta mgonjwa mmoja ametembelewa na watu zaidi ya watano kwa pamoja.

“Ila tunaichukua hiyo kama changamoto tutaangalia utaratibu wa kufanya na ndani ya wiki moja tutakuwa tumepata ufumbuzi,” alisema Dk Magendi.