VIDEO: Lissu awasha moto tena, Ndugai amjibu

Muktasari:

  • Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ameandika waraka wa mwaka 2019 kudai demokrasia kwa mwaka 2019, akitaja matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu huku pia akihoji sababu ya Bunge kutogharamia matibabu yake.

Dar es Salaam. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ametoa waraka mrefu ukielezea masuala mbalimbali ikiwamo kushambuliwa kwake na Bunge kutogharamia matibabu yake.

Hata hivyo, Spika wa Bunge Job Ndugai amemjibu mnadhimu huyo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni akimtaka arejee Tanzania waweke mambo mezani kisha Watanzania wapime nani asiye na shukrani.

Waraka huo wenye maneno 3,974, ambao Lissu amesema utaendelea wiki ijayo una kichwa cha habari ‘Mwaka mpya 2019: Mwaka wa kurudisha demokrasia, haki za binadamu na utu wetu Tanzania.’

Alishukia Bunge

Lissu ambaye yupo Ubelgiji anakopata matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, mchana wa Septemba 7, 2017 alipokuwa akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge jijini Dodoma alihoji inawezekanaje hadi sasa Spika hajafanya mawasiliano ya aina yoyote na yeye juu ya hali ya afya ya ke licha ya kwamba hajaonekana bungeni kwa mwaka mmoja na miezi minne lakini ameendelea kumlipa mshahara wa kila mwezi.

Ameilaumu Serikali na Bunge kwa kutogharamia matibabu yake huku akimtaja Spika Ndugai kutotekeleza ahadi yake ya kumtembelea.

“Kabla sijahamishiwa nchini Ubelgiji (Januari 6 mwaka jana) kutoka Kenya, Spika Ndugai aliahidi hadharani, kwenye mahojiano na Azam TV, kwamba atafika kunitembelea, mahali popote nitakapokuwa nimelazwa hospitalini.Hadi ninapoandika maneno haya, bado Spika Ndugai hajatimiza ahadi yake hiyo. Hakuna mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge, au ofisa yeyote wa Bunge, aliyefika hospitalini kuniona na kunijulia hali.”

Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu madai hayo, Spika Ndugai alisema wameshayatolea ufafanuzi malalamiko hayo mara kadhaa.

Alisema alipanga kwenda kumtembelea Nairobi lakini, “tarehe zangu nilizokuwa nimezipanga, akawa amehamishiwa kwenda Ubeligiji, kwa hiyo safari yote ikawa imevurugika.”

Kuhusu Bunge kugharamia matibabu yake, alisema ni kwa sababu hakufuata utaratibu unaotakiwa kwa mbunge kutibiwa nje.

“Mbunge hatibiwi katika nchi anayotaka mwenyewe kama yeye anavyofanya, unatibiwa nje pale inapobidi, pale unapokuwa na recommendations (ushauri) ya madaktari bingwa watatu wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema.

Alisema kuna wabunge wanaotibiwa nchi za mbali kama Ujerumani, Uingereza na Marekani kwa gharama zao.

“Sasa nashangaa analalamika kitu gani wakati ukishachagua jambo si unaenda na chaguo lako?” alihoji.

Aliongeza kuwa Bunge linaendelea kumlipa mshahara kwa sababu hajafukuzwa kazi.

“Tumempenda sana huko aliko na ndiyo maana anauliza kwa nini tunaendelea kumlipa, angesema ahsante kwa upande huo, angalau mmenijali,” alisema.

Mbali na Bunge, Lissu amemtaja pia Rais John Magufuli akihoji sababu za kutomjulia hali ya afya yake. Hata hivyo, baada ya tukio hilo, Rais Magufuli alimtuma Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kwenda Nairobi alikokuwa amelazwa kumjulia hali na kumpa salamu za pole.

Jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa alisema Rais hawezi kujibizana na kila mtu.

Kuhusu Polisi

Lissu pia amehoji sababu ya shambulio hilo kutokea katika makazi ya viongozi wa umma, eneo lenye ulinzi mkali, katikati ya kipindi cha Bunge.

Pia, amehoji sababu ya Jeshi la Polisi kutomkamata mshukiwa yeyote wa tukio hilo huku pia akidai kuwapo kwa watu wanaofahamika waliosambaza maneno kwenye mitandao ya jamii wakitaka auawe.

“Katika shambulio hili, hakuna anayeshukiwa na Jeshi letu la Polisi hadi sasa. Hakuna aliyehojiwa na wapelelezi mahiri wa jeshi letu la Polisi. Hakuna aliyekamatwa na, kwa hiyo, hakuna aliyeshtakiwa” alidai Lissu.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Ahmed Msangi alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa hayuko ofisini.

“Leo niko shambani huku, unaonaje ukinitafuta Jumatatu nikiwa ofisini?” alisema Msangi.

Hata hivyo, Oktoba 2017, akizungumza na vikosi vya jeshi hilo Mbeya, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro alitangaza kufunga mjadala kuhusu kupigwa risasi kwa Lissu huku akiwaonya wanasiasa kuacha kuuendeleza na waliachie jeshi lifanye kazi yake.

Pia alikataa kuijibu familia ya mbunge huyo kuwa jeshi hilo halina dhamira ya dhati ya kufanya uchunguzi.

Lissu pia alizungumzia suala la watu kadhaa waliotekwa na kupotea akiwamo Ben Saanane aliyekuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyepotea tangu Novemba 2016 na mwandishi wa Mwananchi, Azory Gwanda aliyetoweka Novemba 2017, ambao hawajulikani walipo mpaka sasa.

Amegusia pia masuala ya haki za binadamu yakiwamo matukio ya utekaji, mashambulio ya kudhuru miili na watu waliouawa kwa kupigwa risasi.