VIDEO: Mabomu ya machozi yarindima Dar

Mabomu ya machozi yarindima Dar

Muktasari:

  • Polisi mkoani Dar es Salaam wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyabiashara wa soko la Karume (Mchikichini) ambao wameandamana na kufunga barabara iliyopo karibu na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla wakishinikiza kuruhusiwa kuendelea na biashara katika soko hilo lililoungua usiku wa kuamkia jana Jumapili.

Dar es Salaam. Polisi mkoani Dar es Salaam wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyabiashara wa soko la Karume (Mchikichini) ambao wameandamana na kufunga barabara iliyopo karibu na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla wakishinikiza kuruhusiwa kuendelea na biashara katika soko hilo lililoungua usiku wa kuamkia jana Jumapili.

Wafanyabiashara hao maarufu machinga wamefunga barabara kwa kutumia mawe na magogo katika makutano ya barabara ya Uhuru na Kawawa Ilala Boma muda mfupi baada ya kuandamana mpaka kwenye geti la  Ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa huku wakidai kuwa wanataka RC Makalla atoe tamko la kuwaruhusu waendelee kufanya shughuli zao kwenye soko hilo.

Wafanyabiashara wa soko la Karume lililoungua wakiwa wameandamana kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Picha na Tatu Mohamed

Kabla ya kufunga barabara, wafanyabiashara hao ambao baadhi yao walikuwa wamebeba mabango waliandamana huku wakiwa wanaimba "Tunataka Soko letu" wakiwa wamezingira geti la ofisi hiyo, ikiwa ni siku moja imepita tangu soko hilo kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng'wilabuzu Ludigija aliwaomba wafanyabishara hao kuwa wavumilivu na kufuata utaratibu uliotangazwa na Serikali kwamba waiachie kamati ifanye kazi kwa siku saba na kutoa ripoti badala ya kuandamana kutaka kushindana na Serikali.

""Mnatakiwa kujiongeza pamoja na kwamba mnadai haki lakini lazima mfuate utaratibu, jana Waziri aliagiza kamati ifanye uchunguzi hivyo tuiachie Kamati ifanye kazi na walete ripoti," amesema Ludigija.," aliwasihi Ludigija

Jana Jumapili baada ya soko hilo kuungua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla aliwataka wafanyabiasha wa soko hilo kuwa watulivu huku akiahidi kuundwa kamati ambayo itachunguza chanzo cha moto huo kwa siku 14 akipiga marufuku shughuli zozote kuendelea wakati wa uchunguzi huo.

Muda mfupi baada ya RC Makalla kutoa tamko hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa aliagiza kamati hiyo kufanya uchunguzi kwa siku saba badala ya 14.