VIDEO: Mbunge ahofia ng'ombe kuvishwa shanga kiunoni

Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby wakati akichangia taarifa za Kamati za Bunge za Uwekezaji mitaji (PIC), Hesabu za serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za umma ((PAC) bungeni leo Jumanne Februari 7,2023. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Mbunge wa Gairo Ahmed Shabiby amesema inakoelekea Serikali itazivisha ng'ombe shanga za kiunoni.

Dodoma. Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby amesema inakoelekea Serikali itazivisha ng'ombe shanga za kiunoni.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Februari 7,2023 wakati mbunge huyo akichangia taarifa za Kamati za Bunge za Uwekezaji mitaji (PIC), Hesabu za serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za Umma ((PAC).

Shabiby amesema kuna upigaji mkubwa unaofanywa na watu aliosema wanafahamika na ndiyo wanapunguza kasi ya Rais katika Utendaji kazi wake ambao ni mzuri.

Amesema upigaji katika nchi hii bado ni mkubwa na unafanywa kwa wazi na wajanja kwa kushirikiana na baadhi ya mamlaka.

https://www.youtube.com/embed/9x7hCGZP8BY

Kuhusu mifugo amesema kuna wakati nchi haieleweki inahitaji kitu gani wala inaelekea wapi hasa  kwa wafugaji ambao wanaendelea kuishi na sintofahamu.

Kwa mujibu wa Shabiby, suala la kuwavisha hereni ng'ombe halina tija badala yake ni upigaji wa kuwaonea wafugaji.

"Mlianza kupiga chapa ikashindikana, mkaja na suala la kengele nalo likashindikana sasa mnakuja na hereni baadaye mtakuja na kuvisha ng'ombe shanga viunoni kisha mtawavisha vikuku miguuni," amesema Shabiby.

Mbunge huyo ameomba mpango wa kuvisha mifugo hereni usitishwe mara moja kwa sababu hauna tija isipokuwa ni uonevu kwa wafugaji.