Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Mbuzi aliyechunwa, kuvishwa sanda azua taharuki Tabora

Askari Polisi akiwa anashusha kitu kilichodhaniwa kuwa ni mtoto ambacho baada ya kufunguliwa kikagundulika kuwa ni mbuzi iliyochunwa kisha kufungwa kwenye Sanda baadae kutundikwa juu ya Muembe mtaa wa Bomba mzinga kaya ya Isevya manispaa ya Tabora. Picha na Johnson James

Muktasari:

  • Mbuzi huyo amekutwa katundikwa juu ya mti wa muembe na awali waliyemuona walidhani ni ni mtoto mchanga katupwa.

Tabora. Katika hali isiyo ya kawaida, wakazi wa Mtaa wa Bombamzinga, Kata ya Isevya, Manispaa ya Tabora, wamejikuta katika taharuki baada ya kugundua mbuzi aliyekuwa amechunwa ngozi, kuvishwa sanda na kisha kutundikwa juu ya mti wa muembe.

Tukio hilo limezua taharuki na hofu kwa wakazi wa mtaa huo huku wengi wakidhani kifurushi hicho kilikuwa ni mtoto mchanga waliyedhania amekufa na kutundikwa juu ya mti huo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Desemba 12, 2024, Mwenyekiti wa mtaa huo, Ramadhan Kamandwa amesema taarifa za tukio hilo alizipata baada ya kupigiwa simu.

“Nikaacha shughuli nyingine na kuja hapa mara moja,” amesema mwenyekiti huyo.

Amesema awali alipofika hata yeye alidhani ni mtoto mchanga aliyekuwa ametundikwa juu ya muembe, hivyo akapiga simu polisi kuomba msaada wa kufika eneo hilo haraka.

"Nilipata taarifa za tukio na kufika haraka. Tulidhani ni mtoto mchanga ameuawa na kufungwa kwenye sanda, lakini baada ya kuchunguza, tulikuta ni mzoga wa mbuzi ambaye amechunwa ngozi, kavishwa sanda na katundikwa juu ya mti huu wa muembe. Tukio hili limewashtua sana wakazi wa mtaa huu," amesema Kamandwa.

Kwa mujibu wa Kamandwa, uchunguzi wa awali umebaini kuwa tukio hilo linaweza kuwa limechochewa na imani za kishirikina.

Mbuzi aliyechunwa, kuvishwa sanda azua taharuki Tabora

Amesema kama mtaa, watahakikisha wanafanya uchuguzi wa kumbaini aliyefanya kitendo hicho na kumkabidhi kwa vyombo vya dola ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Shuhuda wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina la Dezile Fungameza, amesema alipofika eneo la tukio baada ya kusikia taarifa hizo, alikuta kifurushi kilichofungwa mithili ya mtoto mchanga.

"Tulidhani ni mtoto aliyefariki na kufungwa kwenye sanda. Polisi walipofika na kufungua kifurushi hicho tukagundua kuwa alikuwa ni mbuzi aliyekuwa amechunwa na kuvalishwa sanda,” amesema Fungameza.

Tukio hilo ambalo limetokea usiku wa kuamkia Desemba 12, 2024, limezua taharuki kwa  wakazi hao wa Bombamzinga, huku wengi wakilitafsiri kama ishara ya kuongezeka kwa imani za kishirikina katika eneo lao.

Hivi karibuni, Askofu wa Dayosisi ya Magharibi Kati Tabora, Dk. Isaac Laizer, alitoa wito wa kipekee kwa taifa kuombea Mkoa wa Tabora. Alisema mkoa huo umekithiri kwa matukio yanayohusishwa na imani za kishirikina, jambo ambalo, kwa maoni yake, ni la kipekee na la kushangaza.

"Mkoa wa Tabora unapaswa kuombewa kwa dhati. Mambo ya ushirikina hapa ni ya kiwango cha juu sana. Kuna haja ya mkoa huu kuwa sawa na mikoa mingine nchini," alisema Dk Laizer.