VIDEO: Mbwa afichua yalipo mabaki mwili wa mwalimu

Muktasari:

  • Mwalimu huyo aliyekuwa akifundisha katika shule binafsi ya awali iliyopo eneo la Shabaha, alipotea Julai 20, 2023 bila mafanikio ya kupatikana kabla ya mabaki ya mwili wake yalipookotwa jana Agosti 22, katika mashamba ya TPC.

Moshi. Mabaki ya mwili wa mwalimu Lightness Peter (29) mkazi wa Bomambuzi, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro yamekutwa katika mashamba ya Miwa ya TPC.

Mwalimu Lightness aliyekuwa akifundisha katika moja ya shule binafsi ya awali iliyopo katika eneo la Shabaha wilayani hapo alipotea Julai 20, mwaka huu bila mafanikio hya kupatikana kwake kabla ya mabaki ya mwili wake kuokotwa jana Agosti 22, katika mashamba hayo. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania, Simon Maigwa amethibitisha jana Agosti 24,2023 kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, uchunguzi unaendelea ili kuweza kubaini chanzo cha kifo hicho.

Kamanda Maigwa amesema taarifa za awali zinaonyesha siku ya tukio mwalimu Lightness alitoka nyumbani asubuhi kwenda kazini kama kawaida lakini hakurudi.

"Jana mwili wake umekutwa umeshaliwa, yamekutwa mabaki, tayari tumefungua jalada la uchunguzi ili kubaini kifo chake kimetokana na nini, je ni kifo cha kawaida au kimetokana na uhalifu mwingine,”amesema Kamanda Maigwa.

"Ilionekana mifupa na baadhi ya nguo alizokuwa amevaa, taarifa tulizopata siku ya tukio aliondoka nyumbani asubuhi kwenda kazini kama kawaida lakini hakurudi, hivyo tunaendelea na uchunguzi na tutatoa taarifa kamili uchunguzi utakapokamilika.”

Mabaki ya mwili wa mwalimu yakutwa shamba la miwa

Akizungumzia tukio hilo, Sadick Stephan aliyekuwa bosi wa marehemu Lightness amesema siku ya tukio marehemu hakufika kazini na hawakupewa sababu za kutofika, hadi alipopigiwa simu na mmoja wa marafiki zake akimuulizia kwa kuwa hakuwa amerudi nyumbani.

"Siku ya tukio nilipigiwa simu usiku na rafiki wa marehemu, akiniuliza kama marehemu ametoka kazini kwani hakuwa amefika nyumbani, nilimtaka anipe muda niulize maana sikuwepo kazini, lakini nilipopiga simu kwa mke wangu, alinijulisha kuwa siku hiyo hakufika kazini na hakuwa na taarifa nae.”

John Joseph mkazi wa eneo hilo amesema mabaki ya mwili huo yalikuwa ndani ya mashamba hayo yalisogezwa pembeni ya njia kabla ya wafanyakazi wa mashamba hayo kuyaona na kutoa taarifa.

"Jana saa sita mchana walinzi wa mashamba waliona kundi kubwa la mbwa wakiwa wamejikusanya jambo lililowafanya kufuatilia nini kipo katika eneo hilo, ndipo walikuta mabaki ya mwili huo, na kuwashirikisha majirani waliotambua nguo za lightness na vitu kadhaa kwenye pochi yake,”amesema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Relini kata ya Bomambuzi Elizabeth Mputa ameomba uongozi wa kampuni ya TPC kuongeza doria na ulinzi katika mashamba hayo ya miwa ili kuweza kupunguza vitendo vya kihalifu kwa kuwa yako karibu na makazi ya watu.

Diwani wa Bomambuzi, Juma Raibu ameomba Jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kuweza kubaini chanzo cha tukio hilo.

"Niombe jeshi la polisi kufanya upelelezi wa kina ili kubaini chanzo cha kifo cha binti huyu, lakini pia wananchi wenye taarifa za tukio hili kutoa taarifa polisi kwa waliohusika na hili,”amesema Raibu.