VIDEO: Mfahamu rubani mwanamke anayeileta ndege mpya ya mizigo

Muktasari:

  • Kapteni Neema mwenye uzoefu wa miaka 14 ya kuwa rubani akirusha ndege aina mbalimbali tangu mwaka 2009, punde tu baada ya kuhitimu masomo yake nchini Afrika Kusini ndiye amepewa  jukumu hilo la kihistoria kwa Tanzania.

Dar es Salaam. Ndege mpya ya mizigo ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya ‘BOEING 767-300F AIR TANZANIA CARGO’ imetua kwenye ardhi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam na kupokelewa na Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wa juu wa Serikali.

Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba tani 54 za mizigo imeletwa na rubani mwanamke, Kapteni Neema Swai aliyepewa jukumu la kuirusha kutoka Seattle nchini Marekani kuja Tanzania.

Kapteni Neema mwenye uzoefu wa miaka 14 ya kuwa rubani akirusha ndege aina mbalimbali tangu mwaka 2009, punde tu baada ya kuhitimu masomo yake nchini Afrika Kusini ndiye amepewa  jukumu hilo la kihistoria kwa Tanzania.

LIVE: Mapokezi ndege mpya ya mizigo inayorushwa na rubani mwanadada

Taarifa ya tukio hilo lililovuta hisia za watu wengi imechapishwa katika ukurasa wa Instagram wa ATCL huku ikipokea maoni mengi ya kusifia na kupongeza uamuzi huo kutoka kwa watu mbalimbali.

“Rubani mwanadada Neema Swai ndiye amepewa dhamana ya kuirusha BOEING 767-300F AIR TANZANIA CARGO toka Marekani hadi Tanzania tayari yuko angani uelekeo JK Nyerere International Airport muda wa kuwasili kuanzia saa nane mchana,” imesema taarifa hiyo.

Katika ukurasa wa ATCL, @sangumarie amepongeza uwepo wa marubani wanawake Tanzania huku akionyesha kuwa ni mafanikio.

“Nani aliona miaka 61 baadaye Watanzania watakuwa na marubani wanawake? Nyerere amka uone ndoto uliyoiota...wanawake ninyi ni tai na si kuku,” ametoa maoni.

Akizungumzia ujio wa ndege hiyo jana Juni 3, 2023 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema itarahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kwenda nje ya nchi.

Waziri Mbarawa amesema Serikali iliamua kununua ndege hiyo kwa kuzingatia unafuu wake wa matumizi ya mafuta na kuongeza itakuwa na uwezo wa kusafiri kwa saa kumi bila kutua.

"Ujio wa ndege hii utaleta unafuu kwa wafanyabiashara, hasa wa mbogamboga, maua, nyama, samaki na madini na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje na Serikali pamoja na wafanyabiashara, hususani wa dawa," amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa ATC, Sarah Reuben amesema baada ya kuwasili nchini, ndege hiyo itaanza kutoa huduma Julai 2023 baada ya kukamilisha taratibu za usajili.