VIDEO: Mgeja amfuata Lowassa CCM, aigusa Chadema

Aliyekuwa Kada wa Chadema, Hamis Mgeja akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam  leo kuhusu uamuzi wake wa kujiunga rasmi na CCM. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamisi Mgeja ambaye alitimukia Chadema mwaka 2015, leo ametangaza kurudi CCM

 


Dar es Salaam. Siku chache baada ya mwanasiasa maarufu nchini na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuondoka Chadema na kurudi CCM, aliyekuwa kada wa chama hicho cha upinzani, Khamis Mgeja leo naye ametangaza rasmi kurudi chama hicho tawala.

Mgeja amedai wakati akiwa katika mapumziko ya kisiasa alijitathimini na kuona sababu zilizomfanya ahamie Chadema wakati wa uchaguzi mwaka 2015  sasa hazipo.

"Nimeamua kurudi nyumbani, sijafuata mkumbo wala kushawishiwa na mtu bali utendakazi wa Serikali yangu ya awamu ya tano umenifanya nirudi."

"Leo tarehe sita kwa utashi wangu naamua kurudi CCM na sitawaunga mkono tena Chadema," amesema.

Amesema sababu nyingine inayomfanya atoke Chadema ni kwa sababu chama hicho kimejaa ubinafsi na kisichosikiliza ushauri wa watu wengine.

"Nikiwa Chadema nimewashauri sana waachane na siasa za kiwanaharakati lakini hawakunisikiliza. Sasa ninaomba niwaambie kwa sababu hawakusikiliza ushauri wangu  wanakwenda kuwa na anguko kubwa la kisiasa uchaguzi wa 2020,” amesema.

Mgeja aliondoka CCM na kutimukia Chadema mwaka 2015 baada ya Lowassa kujiunga na chama hicho Julai 28, 2015 na kupewa fursa ya kugombea urais.

Katika kampeni za uchaguzi huo uliofanyika mwaka 2015 ambao Lowassa aligombea, Mgeja alikuwa miongoni mwa makada wa Chadema waliozunguka nchi nzima kumnadi.