Polisi wapewa msaada wa vitanda Moshi

Muktasari:

  • Mkuu wa Shule ya Polisi Tanzania (CCP), Ramadhani Mungi amesema Exim imechangia kuhakikisha maisha ya watu na mali zao zinalindwa

Dar es Salaam. Benki ya Exim imetoa seti ya vitanda kwa Shule ya Jeshi la Polisi Tanzania (CCP) iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro ili kusaidia kuboresha mazingira ya mafunzo.

Exim inaamini msaada huo utasaidia kuboresha mazingira ya mafunzo kwa maofisa wa polisi yatakayochangia kuboresha Jeshi la Polisi katika majukumu yake ya kuwahakikishia ulinzi na usalama Watanzania wote na mali zao.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko, Stanley Kafu amesema, “kupitia mkakati wetu wa kurudisha kwa jamii unayojulikana kama Exim Cares na kama ishara ya mashirikiano yetu ya muda mrefu, tunayo furaha kuchangia vitanda 40 kwa Shule ya Jeshi la Polisi Tanzania ya hapa Moshi.

 “Ushirikiano wetu na Jeshi la Polisi haujaanza leo, mwaka jana Exim tuliingia makubaliano na Jeshi la Polisi Tanzania yenye lengo la kuwezesha utoaji wa mikopo ya masharti nafuu kwa askari polisi kupitia programu yetu maalumu ijulikanayo kama ‘Wafanyakazi Loan.

Akifafanua zaidi Kafu amesema kupitia ‘Wafanyakazi Loan’, askari wanaweza kukopa kuanzia Sh1 milioni hadi Sh160 milioni na marejesho kati ya miezi 6 hadi miezi 96 kutegemeana na ahadi ya mkopaji inayoweza kutumika kutekeleza ndoto za mkopaji ikiwa ni pamoja kupata mkopo wa nyumba, kununua magari na kulipia ada ya masomo ili kujiendeleza kielimu.

Exim imedhamiria kuendelea kushirikiana na Serikali na vyombo vyake vya usalama kuhakikisha ustawi unakuwepo katika sekta mbalimbali ikiwamo usalama, afya, uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania wote bila ubaguzi wa namna yoyote.

Kuhusu msaada huo Mkuu wa Shule ya Polisi Tanzania (CCP), Ramadhani Mungi amesema, “Exim imechangia kuhakikisha maisha ya watu na mali zao zinalindwa, kwa hiyo tunashukuru sana kwa vitanda hivi, vitasaidia sana kuboresha shule yetu.”