VIDEO: Mvua ilivyoleta maafa mikoa mitatu

Baadhi ya wakazi jijini Mwanza wakiwa wameshindwa kuendelea na shuguli zao baada ya kuzingirwa na maji yaliyosambaa daraja la Mkuyuni jijini Mwanza. Picha na Saada Amir

Muktasari:

  • Mmoja afariki dunia Morogoro, miundombinu ya nyumba ikibomoka Mbeya.

Moro/Mikoani. Mvua za masika zinazoendelea kunyesha nchini zimeleta madhara katika mikoa ya Morogoro, Mbeya na Mwanza, zikisababisha kifo cha mtu mmoja na kuharibu nyumba na miundombinu ya barabara.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Februari 22, 2024 ilitoa tahadhari ikieleza vipindi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, hivyo kusababisha uharibifu wa miundombinu, mazingira, upotevu wa mali na maisha.

Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk Ladislaus Chang'a, alipotoa taarifa ya uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua za masika katika kipindi cha Machi hadi Mei, 2024, alisema kutakuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani kwa msimu wa masika 2024, katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Daraja la Mkuyuni la leta kizaazaa Mwanza, wakazi wakaa saa nne kwenye foleni

Mmoja afariki dunia

Kufuatia madhara hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Dunstan Kyobya amethibitisha kifo cha mtu mmoja aliyesombwa na maji baada ya mvua kubwa kunyesha wilayani humo.

Mvua pia imesababisha maeneo mengi ya Mji wa Ifakara kukumbwa na mafuriko, Kyobya alisema akizungumza na Mwananchi, na kuwa zaidi ya nyumba 100 zimezingirwa na maji.

"Machi 25, 2024 Kilombero tulipata mafuriko makubwa ambayo yalisababisha kata tano za Lumemo, Viwanja Sitini, Mbasa, Mrabani na Katihinduka kujaa maji," amesema.

Kyobya amesema: "Historia imeonyesha tangu mwaka 1998 katika wilaya yetu mvua kubwa kama hii haikuwahi kunyesha, hivyo iliponyesha mito ilijaa na kuzidiwa, hali iliyosababisha kutema maji yaliyosababisha Mto Lumemo kujaa na maji kuingia kwenye makazi ya watu."

Amesema jiografia ya Wilaya ya Kilombero iko kama bakuli kwa kuwa maji mengi yanatoka milimani na kupelekwa bondeni yaliko makazi ya watu, hivyo kuna haja ya wananchi kuchukua tahadhari.

"Kiuhalisia jiografia ya wilaya yetu si rafiki, hivyo huu ni wakati wa kuchukua tahadhari kwa wananchi wote wa Wilaya ya Kilombero na Halmashauri ya Ifakara. Naomba niwatake wananchi ambao wana shughuli za kilimo mabondeni watoke, wanaosafiri wachukue tahadhari, maana barabara zinaweza kukatika," amesema.

Miongoni mwa mito inasababisha mafuriko ya mara kwa mara katika baadhi ya maeneo jijini Mbeya ikiwepo Kata ya Mbalizi road, Mabatini na kwingineko. Picha na Hawa Mathias

Kutokana na maji kuzingira kata za Halmashauri ya Mji wa Ifakara, amewaagiza wakuu wa shule kufunga masomo kwa muda kwa kuwa hakuna mazingira rafiki kwa watoto kwenda shule.

"Tuna kata sita mpaka sasa ambazo bado zimezingirwa na maji, nawaagiza wakuu wa shule kupitia ofisa elimu kata, kufunga shule kwanza, huku tukingojea maji yapungue ili watoto waweze kwenda shule bila bughudha kama ilivyo sasa, maana tukiruhusu waende yatatokea maafa zaidi ambayo hatutaki yatokee," amesema.

Pia amewataka bodaboda kuendesha vyombo vyao kwa uangalifu na kuwa makini na madimbwi.

Eva Joseph, mkazi wa Kata ya Viwanja Sitini amesema mafuriko yamewasababishia changamoto na ugumu wa maisha.

"Mafuriko yalipotokea tulidhani ni hali ya kawaida, lakini kadiri muda ulivyosogea maji yalizidi kujaa, mwisho tukajikuta nyumba zimezingirwa na yakawa yanazidi kujaa. Mimi na familia yangu tukashauriana kuondoka kwenda sehemu ya mwinuko, hatukudhurika mpaka mvua ikakatika," amesema.

“Changamoto kubwa kwetu ni baada ya mafuriko, watoto hawawezi kwenda shule, tulio wengi tunashindwa kupika kwa kuwa chakula kimeloa, hivyo tunaiomba Serikali itupatie msaada wa chakula wakati tunangojea maji yapungue ili turudi majumbani," amesema.

Sakina Prosper, mkazi wa Ifakara aliiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa miundombinu ya uhakika ili waondokane na adha ya mafuriko iliyosababisha mifugo kusombwa na mazao kuharibiwa shambani.


Kaya 120 zaanza kurejea

Kwa upande wa Kilosa, Mkuu wa Wilaya, Shaka Hamdu Shaka amesema mvua zimepungua wilayani humo na kaya 120 zilizokuwa zimehifadhiwa kutokana na mafuriko yaliyotokea wiki mbili zilizopita, zimeanza kurejea kwenye makazi yao.

"Mji wa Kilosa umekaa mithili ya bakuli na kwa kuwa tayari mvua nyingi zilishanyesha, ardhi bado ina ubichi, hivyo ikinyesha kidogo tu tayari yanatokea mafuriko, ila kwa sasa hali si mbaya, japo yapo mashamba ya mabondeni bado yametuamisha maji, lakini hayana madhara kwa mpunga," amesema.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Dk Aziz Keto amesema hospitali ya wilaya hiyo siku mbili zilizopita ilizingirwa na maji baada ya Mto Furua unaokatiza katikati ya mji wa Malinyi kujaa maji na kuyamwaga kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo kwenye hospitali hiyo.

"Hali hii imekuwa ikitokea mara kwa mara na inatokana na eneo kubwa la wilaya hii kuwa bonde. Hata hivyo, baada ya jua kuwaka kwa siku mbili maji yaliyojaa eneo la hospitali yameanza kupungua," amesema.

Dk Keto alisema athari za mafuriko ni wagonjwa na wauguzi kushindwa kutoka jengo moja kwenda jingine kupata huduma kama vile vipimo.

Mbunge wa Malinyi, Antipas Mgungusi amesema hospitali hiyo imejengwa eneo lenye bonde na haiwezekani tena kuhamishwa kwa kuwa sehemu kubwa ya wilaya hiyo iko bondeni na kumekuwa na mafuriko ya mara kwa mara.

Hospitali hiyo iliyoanza kutoa huduma ya mama na mtoto na ya wagonjwa wa nje, mpaka sasa imegharimu zaidi ya Sh2.2 bilioni.

Vifaatiba kama vile X-ray na Utra-sound vimeshafika, asilimia 70 ya huduma za matibabu zinatolewa hospitalini hapo.

Mgungusi amesema amewasiliana na Ofisi ya Makamu wa Rais -Mazingira kuomba fedha ili kuboresha miundombinu ya hospitali, ikiwa ni pamoja na kujenga mifereji na kuweka kisima kwa ajili ya kuvuna maji yanayoingia eneo hilo.

Pia vinatakiwa kujengwa vivuko kuunganisha majengo na kushirikiana na taasisi na mamlaka nyingine za Serikali kuhakikisha miundombinu ya maji inajengwa.


Hali ilivyo Mbeya

Wananchi wa Kata ya Sinde, jijini Mbeya wameiomba Serikali kuboreshwa mifereji kutokana na kaya 16 kuathiriwa baada ya makazi yao kuzingirwa na maji.

Mvua iliyonyesha usiku wa Machi 22, 2024 ilisababisha mifereji inayounganisha kata za Isanga na Sinde kujaa na kuingia kwenye nyumba za wananchi.

Queen Mbando amesema kwa miaka mingi wanaishi maisha ya mateso, akiiomba Serikali kuboresha mitaro ya maji kutoka Kata ya Isyesye na Uwanja wa Ndege wa zamani ili kuwanusuru na mafuriko ya mara kwa mara kutokana na mkondo mkubwa wa maji kupita kwenye makazi yao.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Sinde, Anyandwile Mwasanu amesema mafuriko yameleta athari kwenye makazi ya watu 16, yakiharibu vyakula na nyumba.


Mto Mkuyuni wafurika

Wakazi jijini Mwanza wamelazimika kutumia zaidi ya saa nne kwenye foleni baada ya maji kujaa hadi kupita juu ya daraja la Mto Mkuyuni kutokana na mvua iliyoanza kunyesha asubuhi jana.

Mvua iliyokatika saa tatu asubuhi kisha kuanza tena saa tano hadi sita mchana, ilisababisha daraja hilo kujaa maji yaliyosambaa barabarani na kwenye maeneo ya biashara, likiwemo soko la Mkuyuni.

Daraja lipo katikati ya barabara ya Kenyatta inayounganisha kata za Mkuyuni, Butimba, Nyegezi, Mkolani na Buhongwa na Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza.

"Hali ni mbaya, watu wanavushwa, wanaanguka kwenye mitaro, nashauri Serikali waangalie namna ya kufanya kwa sababu vifo vinaweza kutokea, Serikali ituangalie kwa jicho la tatu," amesema Amos Paschal, mkazi wa Mkuyuni.

Mfanyabiashara wa karanga eneo la Mkuyuni, Maria Emmanuel amesema wafanyabiashara wanapata changamoto kufanya biashara eneo hilo.

Amesema tangu saa tano asubuhi maji yalijaa yakitokea darajani hadi saa saba mchana alipozungumza na Mwananchi Digital, hivyo wameshindwa kufanya biashara.

"Serikali iweke daraja kubwa zaidi ili kuhimili wingi wa maji. Nahisi changamoto hapa ni daraja kwa sababu maji yakijaa darajani na mitaroni watu wanashindwa kupita," ameeleza.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, Pascal Ambrose amesema Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa njia nne katika barabara ya kutoka katikati ya Jiji la Mwanza hadi Stendi ya Mabasi ya Nyegezi, hivyo ujenzi utaenda sambamba na kuboresha daraja hilo.

"Katika mwaka wa fedha ujao tunaanza kujenga barabara mpya ya njia nne, kwa hiyo tutaboresha daraja hilo na changamoto itaisha," amesema.