VIDEO: Serikali yawavutia kasi vigogo CWT waliokwepa u-DC

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Japheth Maganga akizungumza kwenye mkutano wa chama hicho, kushoto kwake ni Rais wa Chama hicho Leah Ulaya. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Sakata la vigogo wa Chama cha Walimu Nchini (CWT), limeingia katika sura mpya, baada ya Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Jenista Mhagama kueleza kinachofuata baada ya watu hao kushindwa kuapa jana.

Dodoma. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amesema wanasubiri taarifa kutoka kwa wizara zinazohusika ili waangalie taratibu na sheria zinasema nini juu ya viongozi wa Chama cha Walimu Nchini (CWT) kutotokea kula kiapo cha ukuu wa wilaya katika mikoa husika.

Viongozi walioshindwa kuapa ni Rais wa CWT, Leah Ulaya ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita na Katibu Mkuu wa chama hicho, Japheth Maganga aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Kagera

Akizungumza leo Jumanne Januari 31, 2023, Mhagama amesema yeye ameona kwenye vyombo vya habari kuwa wateule hao hawako tayari kula viapo kwa nafasi walizoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Rais amepewa madaraka ya kukasimu majukumu yake ya utendaji wakazi ndani ya Serikali kwa watu mbalimbali kwa kutumia sifa na vigezo walivyonavyo.

VIDEO: Serikali yawavutia kasi vigogo CWT waliokwepa u-DC

Amesema kuwateua viongozi hao inakuwa ni heshima kubwa ambayo anakuwa ameitoa inayoendana na madaraka hayo ya kikatiba.

Amesema wanachosubiri ni taarifa rasmi kutoka wizara zinazohusika wao yaani Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu.

“Kwa sababu wale ni viongozi wa chama cha wafanyakazi ambao wanasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu lakini wale ni watumishi ambao wanafanya kazi chini ya Ofisiya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa hiyo tutapata hizo taarifa,” amesema.

Mhagama amesema wakipata taarifa basi ndani ya Serikali wataona ni jambo gani ambalo linaweza kufanyika mahususi kutokana na hilo jambo ambalo limejitokeza kwao Utumishi wa Umma.

“Tunasubiri tu, tuletewe hizo taarifa rasmi kwa sababu tunajua kuwa wale ni watumishi wa umma ambao waliazimwa kwenda kufanya kazi maeneo mengine kwa hiyo na sisi tunazo taratibu zetu.

“Kwa hiyo taarifa tutakazoletewa kwenye wizara zinazohusika na sisi tutaangalia taratibu zetu zikoje, miundo yetu ya kiutumishi inasema nini? Taratibu za kisheria zinasema nini kupata taarifa rasmi kutoka kutoka wizara wanazowajibika,” amesema.

Amesema baada ya hapo kama kutakuwa jambo lolote ambalo litatokana na wao basi watawataarifu Watanzania.