RC Shigela akosa majibu kutoonekana DC mteule Mbogwe

Wakuu wa wilaya wapya mkoani Geita, Grace Kingalame (Nyang’hwale), Deusdedith Katwale (Chato) na Cornel Magembe (Geita) wakila kiapo cha maadili katika hafla ya kuapishwa kwao iliyofanyika mkoani humo jana. Picha na Rehema Matowo

Muktasari:

  • Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela amewaapisha wakuu wa wilaya watatu kati ya wanne walioteuliwa kuongoza wilaya za mkoa huo, huku akisema hana taarifa za kutofika kwenye uapisho mkuu mteule wa wilaya ya Mbogwe, Leah Ulaya ambaye pia ni Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Taifa.

Geita. Wakati wakuu wa wilaya za Chato, Nyanghwale na Geita wakiapishwa leo Januari 30, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela, Mkuu wa Wilaya mteule wa Mbogwe, Leah Ulaya hajaonekana kwenye uapisho huo.

Akizungumzia kutooneakana kwa mkuu huyo mteule, Shigela amesema uapisho huo ulipangwa kwa wateule wote, lakini Ulaya hajafika na hajatoa sababu za kutofika na kwamba endapo ataripoti ataapishwa kwa siku nyingine itakayopangwa.

“Sina taarifa yoyote hajafika na sijui yuko wapi wala ni nani kwa maana ameteuliwa na Rais, mimi nimeambiwa watu wako ndio hao waliofika nimewaapisha.

“Yeye kama atakuja nitapewa taarifa basi ataapishwa kwa wakati huo,” amesema Shigela.

Wakuu wa wilaya wateule walioapishwa ni pamoja na Grace Kingalame wa Nyanghwale, Deusdedith Katwale wa Chato na Cornel Magembe wa Geita.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha mkuu wa mkoa amesema miongoni mwa walioapishwa wawili wanatoka mkoa huo na kwamba Rais ameona wanafaa ndio maana kawaleta na kuwatahadharisha wannachi kutowaharibu kwa siasa zao.

“Wapeni ushirikiano wamepangwa nyumbani kuna ndugu na wazazi msigeuze dhamana mkawapa kazi ngumu waacheni wafanye kazi kwa mamlaka yao,” amesema Shigela

Katika ukumbi huo walikuwepo viongozi wa CWT Mkoa wa Geita pamoja na Sengerema ambao walifika kushughudia na kuwapongeza viongozi wenzao walioteuliwa na kupewa dhamana ya kuongoza Wilaya.

Mmoja wa kiongozi wa CWT wilaya akizungumza kwa masharti ya kutokutaka kutajwa majina amesema hajui sababu ya kiongozi wao kutofika kwenye uapisho.

“Sisi tumekuja kuwapongeza walimu wenzetu walioaminiwa na Rais na kuteuliwa, hapa yupo Magembe, mwingine hatujamuona.

“Tunamshukuru Rais kwa kutuamini sisi walimu na kutoa nafasi hizo naimani watazitumikia kwa uaminifu ili kuipa sifa taaluma na chama chetu,” amesema.

Akizungumza mara baada ya kuapishwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe aliyewahi kuwa akiongoza Wilaya ya Ukerewe, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua na kusema kabla ya kuanza kazi atafika kanisani kusali kwanza.

“Nilikuwa DC Ukerewe kocha akaona sitoshi akaniweka benchi kwa muda sasa kocha ameona nimeusoma mchezo vizuri na kuniteuwa kuwa mkuu wa wilaya ya Geita niliposikia jinalangu januari 25 sikuamini nikitoka hapa naenda kanisani kumshukuru Mungu kwanza,” amesema Maghembe.

Kwa upande Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame amesema nafasi aliyoaminiwa ataitumia kwa uaminifu kwa ajili ya maendeleo ya watu wa Nyanghwale na taifa kwa ujumla na kuomba ushirikiano wa wananchi katika kutekeleza adhma yake hiyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chato, Deusdedith Katwale amesema kazi hiyo sio rahisi na kuomba wananchi wamuombee ili aweze kutekeleza majukumu yake.