VIDEO: Simulizi aliyejichoma sindano 38 tumboni akisaka mtoto kwa miaka 13

Fahamu mchozo (ute ute) wakati wa ujauzito

Dar es Salaam. Miaka 13 haikuwa kikwazo kwa Josephine kupambana kupata ujauzito, akitumia zaidi ya Sh20 milioni.

Kwa sasa Josephine (si jina halisi) ana watoto pacha wa kiume wenye umri wa miaka mitano.
Anasema ni baraka kwake kwa kuwa mateso aliyopitia yamegeuka faraja anapowatazama watoto hao wakiwa wenye afya njema.

“Ukipata mtoto kwa umri huu nilionao unamshukuru Mungu,” anasema Josephine, mkazi wa jijini Arusha mwenye miaka 49.

Anasema mume wake alikuwa msaada katika safari yake ya majonzi na simanzi; iliyomalizika kwa tabasamu baada ya kupata ujauzito kwa njia ya upandikizaji mimba kwa wanawake walioshindwa kupata kwa njia ya kawaida (IVF).
 

Mtazamo wa jamii

Anasema pamoja na mume wake walitafuta mtoto kwa zaidi ya miaka 10; akifanya IVF mara nne na kutumia zaidi ya Sh60 milioni, huku Sh40 milioni zikiwa ni msaada kutoka hospitali.
Anabainisha baadhi ya watu, wakiwamo ndugu wa mumewe walisema kwa umri wake mkubwa ni ngumu kupata ujauzito.

“Ukiwa na shida ya kupata ujauzito jamii inakunyooshea kidole moja kwa moja; utasemwa maneno mabaya na kuitwa kila aina ya majina, usipokuwa na imani utayumba na kupoteza matumaini. Nakumbuka mwanzoni maneno yaliniumiza sana.

“Nilionana na watu wengi, walinishauri mengi, nilikunywa dawa mbalimbali. Wengine walinishauri niwe napumzika, nakula vizuri lakini mimi na mume wangu tulijua nini tunataka,’’ anasema, akieleza jinsi alivyohudhuria maombi katika makanisa kadhaa kuomba msaada wa Mungu.

Josephine anaeleza miaka minne ndani ya ndoa bila kupata ujauzito hawakuwahi kwenda hospitali, wala kunywa dawa ya aina yoyote.

“Nakumbuka kwa miaka hiyo dawa pekee ya kienyeji niliyowahi kunywa ilikuwa ya Kimasai kwa sababu baadhi ya ndugu walihisi nina chango kutokana na maumivu ya tumbo niliyokuwa napata kila ninapoingia katika hedhi, lakini sikuona mabadiliko yoyote,” anasema.
Anaeleza hata hospitalini vipimo vilionyesha hana tatizo linalosababisha ashindwe kupata ujauzito.

“Nilipoambiwa sina tatizo nilikuwa nawaza labda mambo ya Kiafrika (uchawi), labda kuna shida mahali ya kiroho, sikusema kama nimerogwa. Nikawa namwambia mume wangu au ulikuwa unataka kumuoa msichana mwingine akatufanyia kitu,” anaeleza.

Safari ya kupandikiza mimba

Anasema mwanga ulianza kuonekana baada ya kukutana na ndugu yake aliyempa habari za Hospitali ya Avinta Care iliyopo jijini Arusha, eneo la Uzunguni inayotoa matibabu ya IVF.
“Niliamua kwenda kujaribu kupata ujauzito kwa kupandikiza kwa kuwa nilikuwa na kiu ya mtoto. Nikiwa njiani mawazo (kupata ujauzito) yaliteka fikra zangu, hamu yangu ikiwa ni kuonana na daktari nijue nini ataniambia kuhusu hali yangu,’’ anasema.

Anasema daktari bingwa aliyeonana naye katika hospitali hiyo ni Nicholaus Mazunguni, aliyemuagiza yeye na mumewe wafanye vipimo kadhaa.
“Tulipofika hospitali hatukuanza IVF moja kwa moja, tulianza vipimo na tiba za kunisaidia kupata ujauzito kwa njia ya kawaida kwa mwaka mmoja, ikashindikana kupata ujauzito kwa njia hiyo.

“Alipoona imeshindikana, daktari alitushauri kufanya IVF kwa sababu umri ulikuwa umekwenda, hivyo njia pekee iliyobaki ilikuwa ni kupandikiza,’’ anasema.
Anaeleza iliwachukua miezi minane kutafakari na kufanya uamuzi, kipindi ambacho pia waliomba Mungu awafanikishe kwa kuwa IVF gharama yake ni kubwa.
 

Gharama za upandikizaji

“Safari ya IVF kwa mara ya kwanza ilikuwa ngumu kwa sababu ilikuwa Sh12 milioni, bado gharama za dawa na vipimo; hivyo nilitafuta Sh20 milioni ili nifanye matibabu haya,” anasema Josephine, ambaye kitaaluma ni mwalimu.

“Kulingana na kazi yangu sikuweza kupata kiasi chote cha fedha, nililazimika kuchukua mkopo wa Sh20 milioni. Nilianza matibabu, nilichomwa sindano zaidi ya 38 tumboni. Nilikuwa nakwenda hospitali kila siku kwa kipindi cha wiki mbili, ratiba yangu ya kazi ilibadilika, kuna nyakati nilidanganya kazini ili niweze kutibiwa,” anaeleza.

Miaka 13 misukosuko ya kusaka mtoto


Katika matibabu hayo, mwanamke hupewa homoni ya FSH inayotolewa kwa njia ya sindano kwa siku tisa hadi 12 mfululizo ambayo huchochea uzalishaji mkubwa wa mayai.
 

Mara ya kwanza

Anasema baada ya kumaliza sindano, alivunwa mayai na kupandikizwa kiini tete. Alitakiwa kulala bila kufanya kazi kwa siku 14 akisubiri kupima ili kujua kama mimba imetungwa au la.
“Kipindi cha siku 14 baada ya kupandikizwa sikufanya chochote zaidi ya kula na kulala, niliendelea kuchomwa sindano kwa siku 14, kwa kweli ni matibabu yanayohitaji uvumilivu,” anasema.

Anaeleza baada ya muda huo alikwenda hospitali kupima ujauzito lakini mimba haikutunga, jambo lililomuumiza na kumkatisha tamaa. Anaeleza daktari alimtia moyo na kumtaka asimwambie mume wake.

“Daktari alisema yeye ndiye atakayempa majibu mume wangu. Ugumu wa majibu ulinifanya niwaze mengi, kwanza kurudisha mkopo tuliokopa huku hakuna tulichofanikiwa, wakati mwingine unawaza umepoteza hela ila tuliomba Mungu atutie nguvu,” anaeleza.
Baada ya kuzungumza na daktari anasema mume wake hakukata tamaa. “Yeye ndiye aliyenipa moyo, aliniambia hata kama nisipopata ujauzito hawezi kunikimbia. Alinipa ujasiri na kunitia nguvu.

Daktari alisema tutarudia (kupandikiza), nilikaa takriban miezi minne bila kurudi hospitali, kumbuka bado nafanya rejesho (kulipa deni) na gharama ya matibabu ni kubwa hivyo ilinifanya nisite kurudia kupandikiza.’’
 

Safari ya pili

Anasema baada ya ushauri wa daktari, walielezwa hospitali italipia gharama za matibabu ya awamu ya pili ambazo ni Sh15 milioni na wao watalipia vipimo, dawa na sindano.
“Tulikubali kufanya matibabu ya awamu ya pili, hatukuwa na kipato kingine zaidi ya mishahara yetu ambayo yote tuliishia kulipia matibabu na kufanya rejesho,’’ anasema.

Anasema alianza utaratibu upya kwa kuchomwa sindano, kutolewa mayai na mbegu za mumewe kwa ajili ya kupandikiza. Licha ya jitihada hizo, anaeleza hakupata ujauzito.
“Hii ya mara ya pili nilijiuliza nina tatizo gani, mbona sishiki mimba, maswali haya yalikuwa yanazunguka kichwani mwangu, mbali na kupokea ushauri kutoka kwa daktari na wasaidizi wake, bado nilikuwa na wasiwasi juu ya uwezo wangu wa kushika mimba,’’ anasema.
 

Awamu ya tatu

Anasema hata mara ya tatu walipopandikiza hakupata ujauzito. “Majibu hayakuwa mazuri, hapa sasa nilikuwa namuonea huruma daktari, mara hii ya tatu hospitali ilitulipia Sh15 milioni na sisi kulipia dawa, pamoja na vipimo.

“Nilihitaji kupumzisha mwili, hususan sindano, maana zilikuwa nyingi. Awamu ya kwanza nilichoma zaidi ya 38 tumboni; sindano moja kila siku kwa siku 14. Awamu ya pili na ya tatu idadi hiyo hiyo na dawa; akili yangu na mwili wangu ulichoka, nilihitaji kupumzika,” anasema.
 

Upandikizaji mara ya nne

Mwaka 2018 baada ya kupona majeraha ya moyo anasema alirudi kwenye matibabu. Safari ikianza Januari hadi Mei alipopandikizwa mbegu (IUI -Intrauterine insemination).
Huu ni upandikizaji wa mbegu za mwanamume kwenye kizazi baada ya mbegu kuandaliwa kitaalamu. Hufanyika kwa kutumia kifaa maalumu kupitia mlango wa kizazi; kawaida haina maumivu na huchukua dakika chache kuziingiza.

Anasema baada ya siku 14 alikwenda kupima na alikuwa na ujauzito. “Nilifurahi sana, ndoto zikawa zimetimia, yaani maisha yangu yakabadilika kwa mwezi mmoja wa ujauzito,’’ anasema.
 

Mimba kuharibika

Josephine anasema kuna siku akiwa kwenye sherehe ya harusi ya rafiki yake alinyanyuka kwenda kuchukua chakula na kuhisi maumivu makali ya tumbo, wakati akipiga hatua akagundua anatokwa damu.

“Nilishtuka, nilikwenda hospitali nikaelezwa mimba imeharibika. Niliumia, nikamwachia Mungu, uchungu huu hausimuliki, furaha yangu ilikatika. Lakini ilikuwa tofauti kwa daktari kwa sababu alicheka badala ya kusikitika.

“Akaniambia kilichonipata ni wazi kuwa nina uwezo wa kushika mimba, hivyo alinitaka pamoja na mume wangu kuanza tena matibabu; kupandikiza kwa mara ya nne kwa IVF. Hapo ilikuwa ni mwezi mmoja baada ya mimba kutoka,’’ anasema.
 

Tabasamu larejea

Anasema walifanya IVF ya nne akianza matibabu upya ya kuchoma sindano za kuvuna mayai kwa siku 10, kupandikiza na kuchoma sindano kwa siku 14 baada ya kupandikiza na kusubiri majibu.

Josephine anasema baada ya siku 14 alipima na kuelezwa ni mjamzito. Aliendelea kuchoma sindano kwa miezi mitatu, huku kila sindano akilipia kati ya Sh10,000 hadi Sh15,000.
Anaeleza baada ya miezi mitatu alianza kutumia dawa ya ‘cyclogest pessary’ akilipia Sh90,000 kwa dozi ya siku 20. Alitumia dawa hizo ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
Josephine anasema baada ya miezi tisa alijifungua watoto pacha wa kiume kwa njia ya upasuaji, ambao sasa wana miaka mitano.
 

Kauli ya daktari

Dk Mazunguni anasema wapo wanawake waliofanya IVF zaidi ya mara moja bila mafanikio na wengine mara moja na kupata ujauzito. Anabainisha hali hiyo inatokana na mwili wa mwanamke, namna unavyopokea dawa na tatizo la mwanamke husika.

Mtaalamu huyo anasema kwa mujibu wa takwimu la Shirika la Afya Duniani (WHO), mafanikio ya IVF kupata ujauzito au mtoto ni kuanzia asilimia 15 hadi 45 na hutegemea umri na tatizo alilonalo mwanamke. Anasema gharama yake ni kuanzia Sh7 milioni hadi Sh15 milioni.
Dk Mazunguni anasema alimhudumia mwanamke huyo kwa miaka mitatu akifanya IUI moja na IVF mara nne.

“Kati ya wanawake 10 wanaofanya kwa mara ya kwanza wanaweza kupata wawili hadi watatu, hawa ni wanawake wenye matatizo tofauti yanayosababisha washindwe kupata ujauzito kwa njia ya kawaida. Nawasisitiza wanawake wanaokuja kufanya matibabu kufuata masharti na kutokukata tamaa.

“Unaporudia matibabu kwa mara ya pili, kila kitu kinaanza upya, kuanzia sindano za kupevusha mayai, hivyo gharama inategemea na tatizo la mwanamke. Tunawashauri wagonjwa huduma ya upandikizaji inavyofanyika ili awe tayari kupokea majibu yoyote bila kukata tamaa,” anasema.

Gharama halisi za mizunguko minne ya IVF anasema ni Sh60 milioni, hivyo mwanamke huyo alilipia mzunguko wa kwanza na hospitali kumsaidia mizunguko mingine minne.
Anasema kinachosababisha gharama kuwa kubwa ni dawa zinazotumika kuwaandaa kinamama, vifaa, dawa wakati wa kuvuna mayai na upandikizaji wa kiini tete.
Dk Mazunguni anakumbuka namna walivyomfanyia matibabu ya upandikizaji mama huyo kwa mara nne.

“Niliwaambia siyo kila wakati matibabu haya utapata ujauzito, kuna wakati mama anaweza kufanya zaidi ya mara moja ndiyo akafanikiwa, hivyo niliwaandaa kwa majibu yote mawili na baada ya kuwa sawa ndipo wakaingia kwenye matibabu,’’ anasema Dk Mazunguni.
Anabainisha kuwa mwanamke huyo kupata ujauzito na kujifungua ilikuwa habari njema kwa kituo hicho.
 

Sababu kutoshika mimba

“Umri unapokuwa mdogo kati ya miaka 18 hadi 35 tunakuwa na uhakika mwanamke anapotumia dawa za kumsadia kutengeneza mayai atatengeneza yenye hali nzuri ikilinganishwa na mwenye umri wa miaka 36 na kuendelea.

“Hivyo, yule mwenye umri mdogo ana uwezo mkubwa wa kufanikiwa. Sababu ni nyingi za kufanikiwa au kufeli, hatuangalii sababu moja,’’ anasema.
Anasema tangu wameanza matibabu hayo mwaka 2018, wamewapandikiza wanawake 1,400 na watoto 600 wamezaliwa.

“Changamoto ni mtazamo wa jamii kwamba unapofanya IVF lazima ufanikiwe, wengine wanachukua mkopo benki kufanya matibabu, hivyo wasipofanikiwa inawaumiza,’’ anasema.
Anasema kwa wiki moja huwahudumia zaidi ya wagonjwa 180, ingawa siyo wote wanaofika katika kituo hicho hupatiwa huduma ya upandikizaji.

Dk Mazunguni anasema ni asilimia nne tu kati ya wanaowaona hufanyiwa huduma ya upandikizaji.

“Wengine wakishafanya vipimo hugundulika wanahitaji huduma ya dawa na baada ya muda hupata ujauzito,’’ anasema.