Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vielelezo 480 kuwasilishwa kesi ya fundi mashine za EFD, wenzake

Muktasari:

  • Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi wanakabiliwa na mashtaka 574 likiwemo la kuisababishia TRA hasara ya zaidi ya Sh971 milioni.

Dar es Salaam. Jumla ya vielelezo 480 vinatarajiwa kuwasilishwa mahakamani na upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi, inayowakabili washtakiwa wanne, wakiwemo mtu na mpenzi wake na fundi wa mashine za risiti za kielektroniki (EFD).

Pia Jamhuri katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mfawidhi Is-haq Kuppa inatarajia kuwaita jumla ya mashahidi 40 kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

Katika kesi hiyo iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni iliyoko Kinondoni, washtakiwa hao wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 574 yakiwemo ya kughushi, kutakatisha fedha haramu, kukwepa kodi na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya zaidi ya Sh971.7 milioni.

Washtakiwa hao ni Frank Kagale, Awadhi Mhavile (anayetambulishwa kama fundi wa EFD), Ally Msesya maarufu kama Ally Yanga na Salma Ndauka, anayetambulishwa kuwa ni mpenzi wa mshtakiwa wa kwanza, Frank.

Idadi hiyo ya vielelezo na idadi ya mashahidi imetajwa na waendesha mashtaka Septemba 12, 2024, jioni wakati wa usikilizwaji wa awali, ambapo washtakiwa walisomewa maelezo ya awali ya kesi.

Walisomewa maelezo hayo na Wakili wa Serikali Tumpale Lawrence, akisaidiwa na mawakili wa Serikali, Emmanuel Medalakini na Auni Chilamula.

Katika maelezo hayo imedaiwa kuwa Machi, 2023, TRA ilipokea taarifa kutoka kwa msiri wake kuwa kuna risiti za kielektroniki zilizotolewa kutoka kwenye mashine zilizopotea au kuibwa kutoka kwa wamiliki halali na zinasambazwa isivyo halali.

Kwa mujibu wa Wakili Tumpale, kutokana na taarifa hiyo uchunguzi ulianza kwa kushirikiana na maofisa wa Jeshi la Polisi na Julai 7, 2023 mtu aitwae Meshack Athanas, dereva wa bodaboda alikutwa na risiti za kielektroniki saba, zenye thamani ya kodi ya Sh128.5 milioni.

Kati ya risiti hizo, nne zilikuwa zimetolewa kutoka kwenye mashine ya kieletroniki, mali ya Africa Harmony and Trade Ltd yenye namba 03TZ843040152, aliyesajiliwa kwa namba ya mlipakodi 159265420.

Risiti mbili zilitolewa kutoka kwenye mashine ya kieletroniki mali ya Tabisco Entreprises Ltd, yenye namba 03TZ442007272 na namba ya mlipa kodi ni 100219557 na risiti moja iliyotolewa kutoka kwenye mashine ya kieletroniki mali ya Eco Consumer Products ltd yenye namba 03TZ442021550.

Alipohojiwa baada ya kukamatwa, Meshack alieleza kuwa alipewa risiti hizo na Ally Omary Msesya (mshtakiwa wa tatu).

Siku hiyohiyo, Meshack aliwaongoza wapelelezi katika ukamataji wa Msesya na Julai 8, 2023 aliwaongoza wapelelezi kumkamata mshtakiwa wa pili, Awadhi.

Baada ya kukamatwa mshtakiwa Awadhi alikutwa na risiti 11 za kieletroniki za uongo zenye thamani ya Sh133 milioni.

Risiti hizo zilikuwa zimetolewa kutoka kwenye mashine ya kieletroniki yenye namba 03TZ843040152, mali ya Africa Harmony Industry and Trade Ltd na nyingine za 13 kampuni ya Incotext, zikisadikika kuwa za wizi au zimepatikana kinyume cha sheria na mashine hizo zilihodhiwa.

"Katika kumhoji Mhavile (Awadh) alimtaja Kagale (Frank) kuwa ndiye mwenye mashine iliyotumika kutoa risiti bandia alizokutwa nazo," amedai Tumpale.

Wakili huyo ameendelea kueleza kuwa kutokana na maelezo ya Awadhi juhudi za kumtafuta Kagale zilianza na Julai 19, 2023 wapelelezi walipokea taarifa kutoka kwa msiri kuwa ana rafiki wa kike aitwae Salma Ndauka ambaye ni mshtakiwa namba nne.

Siku hiyohiyo Julai 19, 2023, Salma alikamatwa na katika upekuzi alikutwa na mashine 10 za EFD aina ya Incotex, kati yake mashine nane ndizo zilitambulika namba zake na mashine mbili hazikutambulika kwani zilifutika na zote zilihodhiwa.

Vilevile alipohojiwa alimtaja pia Kagale kuwa ndiye mwenye mashine hizo.

"Januari 16, 2024 Kagale alikamatwa na katika mahojiano alikiri kuwa mashine za alizokutwa nazo Ndauka ni za kwake na alikiri kuzitumia kutoa risiti mbalimbali za uwongo," alieleza Wakili Tumpale.

Wakili Tumpale aliendelea kueleza kuwa uchunguzi ulibaini kuwa mashine yenye namba 03TZ443024331 mali ya Kampuni ya Oceanic Cachet Limited kati ya Aprili, 2023 na Julai, 2023 ilitumika kutoa risiti za uongo zenye thamani ya zaidi ya Sh1.9 bilioni.

"Kutokana na kiasi hicho kiasi cha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) zaidi ya Sh294.7 milioni hakikuwasilishwa TRA", alisema Wakili Tumpale.

Alidai kuwa mashine yenye namba 03TZ442007272 mali ya Tabisco Enterprises Ltd kati ya Aprili, 2023 na Juni, 2023 ilitumika kutoa risiti za uongo au za uwongo zenye thamani ya zaidi ya Sh2.37 bilioni.

Amesema kutokana na kiasi hicho cha fedha za mauzo, Kodi ya VAT kiasi cha Sh373.5 milioni haikuwasilishwa TRA. 

Pia ameeleza kuwa mashine namba 03TZ843040152 mali ya Africa Harmony lndusry and Trade Ltd katika kati ya Mei, 2023 na Juni, 2023 ilitumika kutoa risiti za uongo zenye jumla ya zaidi ya Sh1.9 bilioni za mauzo na zaidi ya Sh303.7 milioni kama VAT hakikuwasilishwa TRA.

Kutokana na matukio hayo, Wakili Tumpale amedai kuwa washtakiwa, waliisababishia TRA hasara ya zaidi ya Sh971.9 milioni.

Pia amedai kuwa risiti hizo ziliupotosha mfumo na Kamishna Mkuu wa TRA kwa kuonyesha kuwa Kampuni ya Oceanic Cachet Ltd ilifanya mauzo ya zaidi ya Sh1.9 bilioni, Tabisco Enterprises Ltd mauzo ya zaidi ya Sh2.3 bilioni na Africa Harmony lndusry and Trade Ltd mauzo ya zaidi ya Sh1.9 bilioni.

Wakili Tumpale amedai wakati wa uchunguzi ilibainika zaidi kuwa watuhumiwa wote wanne walikuwa wakiongoza na kuratibu genge la uhalifu wa makosa mbalimbali.

Ameyataja makosa hayo kuwa ni kutoa risiti zisizo sahihi, kutumia mashine za kieletroniki kwa namna ya kuupotosha mfumo au Kamishna Mkuu wa TRA, kukwepa kodi kinyume na sheria, kuisababishia hasara TRA na kutakatisha fedha.

Baada ya kusomewa maelezo hayo ya awali, washtakiwa wote walitakiwa kueleza mambo wanayokubaliana nayo na wasiyokubaliana nayo.

Washtakiwa wengine walikubali utambuliaho wake binafsi na mahali anakoishi lakini akakana mashtaka yote, lakini Awadhi alikana dini iliyoandikwa kwamba ni Mkristu akidai yeye ni Mwislamu na kwamba si fundi wa EFD bali yeye ni msambazaji wa mashine hizo.

Hakimu Kuppa alipanga kesi hiyo kuanza kusikilizwa ushahidi Septemba 24, 2024 na aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe hiyo huku akiamuri washtakiwa kuendelea kushikiliwa mahabusu, kutokana na kikabiliwa na mashtaka yasiyo na dhamana.