Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vifungashio hivi vinavyohatarisha afya yako

Muktasari:

  • Matumizi ya karatasi zenye maandishi kufungashia bidhaa yanahatarisha afya na yanaweza kusababisha kuvuja kwa taarifa binafsi. Wataalamu wanashauri kutumia vifungashio salama vya chakula na kuimarisha elimu kwa wananchi na taasisi kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi.



Dar es Salaam. Licha ya kuwa mbadala wa gharama nafuu kwa wafanyabiashara, matumizi ya karatasi zenye maandishi kufungashia bidhaa yameelezwa kuwa hatari kutokana na kemikali zinazoweza kudhuru afya na pia kusababisha kuvuja kwa taarifa binafsi.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, wino unaotumika katika uchapishaji wa karatasi hizo mara nyingi huwa na kemikali zisizostahili kugusana na chakula na ni hatari kwa afya ya binadamu.

Akizungumza na Mwananchi, daktari bingwa kutoka Idara ya Mafunzo na Utafiti wa Magonjwa ya Ndani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Ernest Winchislaus, amesema matumizi ya karatasi hizo yameendelea kutokana na urahisi wa upatikanaji wake na gharama nafuu.

Amesema karatasi zilizochapishwa kwa wino huwa na kemikali ambazo hazijatengenezwa kwa matumizi ya kugusana moja kwa moja na chakula na zinaweza kuwa na madhara endapo zitaendelea kutumika kufungashia chakula.

"Changamoto kubwa hujitokeza zaidi pale chakula kinapokuwa cha moto au chenye mafuta, kwa sababu baadhi ya kemikali zilizopo kwenye wino zinaweza kuhamia kutoka kwenye kifungashio kwenda kwenye chakula na hatimaye kuingia mwilini," amesema Winchislaus.

Daktari huyo amesema karatasi au magazeti yaliyotumika pia yanaweza kuwa chanzo cha uchafu na vijidudu kutokana na kushikwa na watu wengi au kuhifadhiwa katika mazingira yasiyo na usafi wa kutosha.

Ameshauri wafanyabiashara na wananchi kutumia vifungashio vilivyotengenezwa mahsusi kwa ajili ya chakula, kama karatasi maalumu za kufungashia chakula (food-grade), maboksi yaliyoidhinishwa kwa matumizi ya chakula, vyombo vya glasi, chuma cha pua au plastiki zenye ubora unaokubalika.

"Si kila karatasi inafaa kutumika kufungashia chakula. Ni muhimu jamii ikaelewa kuwa kuchagua kifungashio sahihi ni sehemu ya kulinda afya ya mlaji," amesema.


Ubora wa vifungashio

Mtengenezaji wa vifungashio vya karatasi jijini Dar es Salaam, Alod Shambalai, amesema wamejikuta wakitumia karatasi zisizo na taarifa za watu kwa sababu magazeti ni mepesi, yanachakaa haraka na hayafai kwa baadhi ya vyakula vyenye mafuta au majimaji.

Amesema kwa vyakula vya mafuta, maandishi yaliyopo kwenye magazeti yanaweza kuhamia kwenye chakula, jambo linalowafanya wafanyabiashara na wateja kutopendelea kutumia vifungashio hivyo.

"Hizi karatasi za magazeti ni laini sana. Zikifungashia chakula chenye mafuta, hufyonza mafuta na wakati mwingine maandishi yanaweza kuonekana kwenye chakula. Pia, kwa vyakula vyenye majimaji, zinachanika haraka," amesema.


Uhifadhi wa taarifa

Kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Na. 11 ya mwaka 2022, kila taasisi inayochakata taarifa binafsi inapaswa kuwa na Ofisa wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi (DPO) anayesimamia uzingatiaji wa sheria katika ukusanyaji, matumizi, uhifadhi na uharibifu wa taarifa, akiwa amepatiwa mafunzo.


Elimu inahitajika

Mtaalamu wa masuala ya ulinzi wa taarifa binafsi, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, amesema changamoto kubwa iliyopo ni uelewa mdogo wa wananchi na baadhi ya taasisi kuhusu Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

"Watu wengi bado hawaelewi kuwa taarifa binafsi zinapaswa kulindwa wakati wote, hata baada ya nyaraka husika kumaliza kutumika," amesema.

Amesema mara nyingi nyaraka zenye taarifa za wateja, wagonjwa au watumishi huchapishwa na kutumika ofisini, lakini baadaye hutupwa bila kuharibiwa kwa utaratibu salama.

"Vielelezo vilivyoonekana vinaonyesha baadhi ya karatasi zinazotumika kufungashia bidhaa bado zina taarifa zinazoweza kumtambua mtu. Hivyo, lazima kuwepo na elimu kwa taasisi zinazokusanya taarifa za wananchi, ikiwemo hoteli, kampuni na taasisi nyingine," amesema.

Edmund Komba, msimamizi wa nyumba ya kulala wageni, amesema vitabu wanavyotumia kuandikisha wageni kutokana na idadi ya wateja hudumu kwa mwaka mmoja.

"Kuna namna huwa tunakosea kutupa hivi vitabu, hususan kwa kuwapa wazoa taka au wafanyakazi wa usafi baada ya kumalizika kwa matumizi yake, maana kila mwaka tunafunga na kuanza kutumia vipya," amesema Komba.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa vifaa vya ofisini, Jackline Henry, amesema elimu kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi imemfanya kubadili namna ya kuteketeza karatasi zilizoharibika.

"Nilikuwa na makaratasi mengi, hata yale yaliyokuwa na taarifa kama vyeti vilivyochapishwa vibaya, lakini sasa ninayachana na kuyachoma mwenyewe ili kuhakikisha yanateketea," amesema.

Amesema amehudhuria hafla kadhaa na elimu waliyopewa na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imemsaidia kutambua kuwa hata karatasi moja inaweza kubeba taarifa muhimu za mtu.