Vigogo CWT wajifungia Tanga, Serikali yabariki

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omari Mgumba.

Muktasari:

  • Mwananchi imeshuhudia wakati viongozi hao wakuu wa CWT wakiwa ukumbini, nje kuna askari pamoja na waandishi wa habari ambao wamewasili baada ya kupata taarifa kwamba uongozi utakuwa na kikao na wanahabari.

Tanga. Wakati bado kukiwa na sintofahamu ya viongozi wa Chama cha Walimu Taifa (CWT) kutokwenda kuapishwa nafasi za ukuu wa wilaya walizoteuliwa, viongozi hao wameendelea kushiriki Kikao cha kamati ya utendaji katika hoteli ya Regal Naivera Jijini hapa, huku nje kukiwa na ulinzi wa askari wa jeshi la polisi wenye silaha.

Viongozi walioshindwa kuapa ni pamoja na Rais wa CWT, Leah Ulaya ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita na Katibu Mkuu wa chama hicho, Japheth Maganga aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Kagera.

Wakati wenzao wakihapishwa jana Januari 30, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela wenyewe hawakuripoti maeneo waliyopangiwa bali walijifungia jijini Tanga kuongoza mkutano wa viongozi wakuu wa CWT.

Leo Januari 31, Mwananchi limeshuhudia viongozi hao pamoja na wenzao wakiendelea na vikao vyao, huku waandishi wa habari pia wakibaki nje kuwasubiri.

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omari Mgumba amesema Serikali imetoa baraka kuendelea na kikao hicho kinachoongozwa na wakuu wa wilaya wateule na kwamba sheria haiwafungi kuwa wakuu wa wilaya huku wakiwa viongozi wakuu wa vyama hivyo.

Mgumba aliyeambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo pamoja na Wilaya ya Tanga, amesema amekwenda kuwahakikishia kuwa wapo salama na hakuna atakayewabughudhi.

"Yanayosambaa kwenye mitandao kwamba Rais alikamatwa, Katibu Mkuukahojiwa yapuuzeni, Serikali ipo pamoja na nyinyi na hakuna atayewabughudhi." amesema Mgumba.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mmoja wa maofisa wa CWT, zinaeleza kuwa kikao hicho cha kamati ya utendaji kitaendelea hadi ajenda zilizopangwa zitakapokamilika.