Vijana 200 wanufaika na mafunzo ya ufundi, ujasiriamali

Arusha. Jumla ya vijana 200 kutoka mikoa minne Tanzania wamenufaika na mafunzo ya ufundi na ujasiriamali baada ya kufadhiliwa na Shirika la maendeleo la Ujerumani (GIZ) kupitia programu ya kukuza ujuzi na ajira kwa maendeleo ya vijana (E4D).

Hayo yamesemwa jijini Arusha na Meneja miradi wa  kuwezesha ajira za vijana kwenye sekta ya sola kutoka shirika  la GIZ programu ya EFD, Faustine Msangira wakati akizungumza  katika kikao cha majadiliano na  wawakilishi wa makampuni ya sola kutoka Tanzania, taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

Aidha kikao hicho kililenga kujadili namna sekta ya nishati jadidifu ya sola itakavyoweza kutoa ajira kwa vijana na kuondokana na changamoto hiyo ili vijana waweze kujiajiri na hata kuajiri wengine kupitia sekta hiyo.

Msangira amesema shirika hilo limefikia hatua ya kutoa ufadhili kwa vijana hao kulingana na uhitaji wa kampuni za sola kuhusu vijana wenye utalaamu wa kutosha kuhusu masuala ya nishati mbadala ambapo vijana hao ni kutoka mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Manyara na Geita .

Amesema mafunzo hayo yanatolewa kwa vijana hao kupitia mradi unaotekelezwa  na shirika hilo wa kukuza ujuzi na ajira kwa maendeleo ya vijana Tanzania mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kwa kushirikiana na serikali ya Ujerumani (GIZ) chini ya mradi wa Sola unaotekelezwa kwa kushirikiana na TAREA.

"Mafunzo haya yanasaidia sana vijana wetu kuweza kujiajiri pindi wanapohitimu kwani huwa tunawapatia  na vitendea kazi kwa ajili ya kujiajiri na tumechukua  vijana 200 wa mfano tu ila awamu ya pili tutaongeza vijana wengine kwani maombi yaliyotumwa  yalikuwa mengi sana na mradi huu ulianza mwaka 2022 na unaishia mwishoni mwa mwaka 2023," amesema

Aidha amefafanua kuwa mwitikio wa wanawake katika mafunzo hayo ya ufundi ni mkubwa kwani wanawake ni asilimia 40 huku wanaume ni asilimia 60 jambo ambalo linaleta hamasa kubwa ya wanawake kujitokeza katika masuala ya ufundi kwa ujumla.

Amesema wadau hao wameweza kukutana na kuangalia namna ya kuwasaidia vijana kupitia sekta hiyo ya nishati ya sola na kuweza kuweka  mikakati mbalimbali katika kipindi hiki ambacho mradi unafikia  mwisho ili waweze kuwasaidia vijana hao hata kama hakuna hela za wafadhili. 

Naye Mkuu wa kitengo cha huduma kwa wateja kutoka kampuni ya sola ya Mysol, Emmanuel Meisilal amesema kampuni hiyo inahusika na ukuzaji na usambazaji wa sola Tanzania ambapo ilianzishwa mwaka 2011 na hadi sasa hivi imeweza kupata soko mikoa yote ya Tanzania.

Meisilal amesema katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana  wameweza kutoa ajira kwa vijana 400 kwenye ufundi huku zaidi ya vijana 500  wakiajiriwa na imewasaidia kwa kiasi kikubwa sana kuondokana  na changamoto ya ajira .

Ofisa biashara Mkuu wizara ya Viwanda na Biashara, Wilfred Kahwa amesema mjadala huo ni muhimu sana kwani wameweza kujadili namna ya kuweza kuondokana na changamoto ya ajira kwa vijana kupitia sekta hiyo ya nishati jadidifu ya sola.

Kahwa amesema sekta ya umeme jadidifu ni moja ya eneo ambalo ni kivutio kwa sasa na ina fursa nyingi kwa vijana kuweza kujiajiri  hivyo ni vizuri makampuni hayo yakatumia fursa hiyo kuweza kuajiri vijana wengi iwezekanavyo ili waweze kuondokana na changamoto  ya ajira ambayo imekuwa ni janga  la kitaifa. 

Kwa upande wake Mwalimu wa umeme kutoka chuo cha Veta Shinyanga, Aziza Abdallah amesema kutolewa kwa mafunzo hayo kwa vijana hao kumewasaidia sana kuweza kujiajiri na hata wengine kupata ajira katika makampuni mbalimbali ya sola.