Vijana, Wafanyakazi wa Nyumbani wafundwa kutengeneza viungo

Mkaguzi kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mkoa wa Mwanza, Nelson Mugema akitoa mafunzo kwa vijana na wafanyakazi wa nyumbani 45 kutoka kata ya Mahina na Buhongwa jijini Mwanza katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mkolani. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

Vijana na wafanyakazi wa nyumbani 45 kutoka kata mbili ya Mahina na Buhongwa jijini Mwanza wamefundwa vitendo namna ya kuzalisha bidhaa kwa kuzingatia ubora na sheria ya mlipa kodi ili kuchangia pato la taifa.

Mwanza. Vijana na wafanyakazi wa nyumbani 45 kutoka kata mbili ya Mahina na Buhongwa jijini Mwanza wamefundwa vitendo namna ya kuzalisha bidhaa kwa kuzingatia ubora na sheria ya mlipa kodi ili kuchangia pato la taifa.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Shirika la WoteSawa na kufadhiliwa na Foundation for civil society (FCS) yamefanyika siku tano tangu Julai 17 hadi 21, 2023 lengo likiwa ni kuhamasisha haki za kiuchumi na kijamii kwa wafanyakazi wa nyumbani na vijana.

Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo yanayofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Mkolani, Ofisa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Giliard Abel amesema vijana wengi hukwepa kulipa kodi, kufungua biashara na wakati mwingine kupigwa faini kwa sababu ya kukosa elimu ya mlipa kodi.

“Ukosefu wa elimu ya mlipa kodi kwa vijana inawafanya wengi kukwepa kulipa kodi na mwishowe kujikuta wakipigwa faini ambazo hazikuwa na ulazima,”amesema Abel

Mkaguzi kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mkoa wa Mwanza, Nelson Mugema amesema vijana wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu uzalishaji hali inayopelekea kuzalisha bidhaa zisizo bora kwa ajili ya matumizi.

 “Ni wakumbushe wajasiriamali na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali kuthibitisha ubora wa bidhaa zao, Shirika la Viwango Tanzania lipo wazi kwa ajili ya kuwapa huduma mbalimbali,” amesema Mugema

Mratibu Msaidizi wa Mradi wa kuhamasisha haki za kiuchumi na kijamii kwa wafanyakazi wa nyumbani kutoka Shirika la WoteSawa, Ester Petro amesema wameandaa mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo wa kuzalisha bidhaa vijana ambazo zitakuwa na ubora huku wakizingatia sheria na taratibu za mlipa kodi.

“Tumekuja na mafunzo haya ambayo washiriki wamefundishwa kwa vitendo lengo kubwa ni kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kupata uelewa wa kutengeneza bidhaa ili wakirudi mtaani waweze kutengeneza bidhaa kamili wakizingatia ubora wa TBS na watakapokuwa wanafanyabiashara walipe kodi,”amesema Ester

Mohamed Venant, mmoja ya washiriki katika mafunzo hayo kutoka kata ya Buhongwa amesema ukosefu wa elimu ya mlipa kodi imekuwa ikipelekea kupigwa faini na mamlaka husika huku muda mwingine wakilazimika kukimbia ili kuwakwepa.

“Elimu ya mlipa kodi ilikuwa changamoto kubwa sana kwetu mfano kuna muda tulikuwa tukisumbuliwa kuwa tulipie tini ya biashara lakini kupitia mafunzo haya nimetambua kumbe inatolewa bure,”amesema Venant

Binti wa kazi za Nyumbani kutoka kata ya Buhongwa, Theonestina Garazi ametoa wito kwa Serikali na mashirika mengine kuendelea kutoa mafunzo ya uzalishaji bidhaa na mlipa kodi ili kuwakwamua kiuchumi na kuongeza pato la taifa.

“Nipende kulishukuru sana Shirika la WoteSawa kwa kuandaa mafunzo haya naamini yanaenda kuwa na mchango mkubwa sana kwa sisi washiriki na kuwafanya waachane na tabia ya kukimbia kulipa kodi,”amesema Garazi