Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vijana wakumbushwa kufanya uwekezaji badala ya kusubiri kuajiriwa

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru  Kitaifa, Godfrey Mnzava akiweka kipande cha  pavings ukutani wakati alipotembelea na kukagua shughuli zinazofanywa na vijana katika kiwanda cha Rock blocks wakati mwenge wa uhuru ulipotembelea kiwanda hicho. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  •  Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, Godfrey Mnzava amewataka vijana kote nchini kutumia fursa zilizopo kwenye maeneo yao kuwekeza ili kukabiliana na changamoto ya ajira nchini, kwa kuwa Serikali imeweka mazingira rafiki ya uwekezaji.

Rombo. Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Godfrey Mnzava amewataka vijana nchini kutumia fursa zilizopo kwenye maeneo yao kuwekeza ili kukabiliana na changamoto ya ajira.

Kiongozi huyo wa mbio za mwenge kitaifa ameyasema hayo Aprili 7, 2024 wakati mwenge wa uhuru ulipotembelea na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na vijana katika kiwanda cha kuzalisha tofali za mwamba cha Rock Blocks kilichopo katika kijiji cha Kinondoni, wilayani  Rombo mkoani Kilimanjaro.

“Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, ya ufanyaji biashara na ya ulipaji kodi ili kuhakikisha wananchi wote wanaiona fursa hiyo ya uwekezaji katika maeneo yetu na kuitumia kwa ajili ya ujenzi wa Taifa letu,” amesema.

Amesema kiwanda hicho ambacho kimetoa ajira kwa vijana zaidi ya 200 kinaenda kuwaondoa vijana waliopo mtaani wilayani humo.

“Mradi huu umeendelea kutoa ajira kwa vijana na tumeona hapa zaidi ya 200 zimetolewa kwa vijana wetu, kwa hiyo ni jambo kubwa sana na la kujivunia kuona  hawapo tena mtaani, wamekuja hapa na  wanafanya kazi, wanapata kipato.”

 “Tumetembelea mradi huu wa uzalishaji wa tofali za mwamba, tumeona bidhaa mbalimbali ambazo zinazalishwa na hawa wenzetu, kwa kweli wanafanya kazi nzuri, tofali hizi tumeziona ni imara na ubora wake na zimethibitishwa na wakala wetu wa Serikali.

“Wametueleza kwamba walianza na mtaji wa Sh100 milioni na sasa hivi wapo na mtaji zaidi ya Sh1 bilioni, ni hatua kubwa sana ambayo wameifikia, kimsingi tunapozungumzia uwezeshaji na ujengaji wa uwezo kwa vijana hii ndio maana yake,” amesema.

Amesema amefurahishwa kuona vijana hao wameendelea kufanya tathmini ya athari za kimazingira zinazotokana na mradi huo kupitia Baraza la Uhifadhi wa Mazingira la Taifa (Nemc.

Awali akitoa taarifa kwa kiongozi huyo wa mbio za mwenge, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Fabian Oisso amesema wakati wanakianzisha mwaka 2013 walikuwa na uwezo wa kuzalisha tofali za mwamba 30,000 kwa mwezi, lakini kwa  sasa wana uwezo wa kuzalisha tofali 200,000 kwa mwezi.

Amesema kiwanda hicho kimekuwa ni chachu ya maendeleo ya jamii katika wilaya ya Rombo ikiwamo kushiriki shughuli za kijamii kama uchangiaji wa matofali kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari na msingi, zahanati, vituo vya afya na hospitali pamoja na ukarabati wa miundombinu ya barabara.

Mwenge huo wa uhuru umetembelea, kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali inayotekelezwa wilayani humo yenye thamani ya zaidi ya Sh2.07 bilioni.